Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Uchaguzi Kanda ya Pwani kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Stephen Elisante akizungumza na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa ngazi ya Jimbo la Kinondoni na Kata za jimbo hilo kwenye mafunzo ya maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Februari.
 Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kinondoni Boniface Lihamwike akiwaapisha wasiamamizi wasaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni na kata zake wakati wa mafunzo ya maandalizi ya Uchaguzi Mdogo.
Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni, Victoria Wihenge, akiwasilisha Mada ya Maelekezo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata kwa wasiamamizi wa Kinondoni.Picha na Hussein Makame-NEC
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewakumbusha wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kusimamia uchaguzi ili kufanikisha Uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Februari 17, 2018.
Hayo yamsemwa na Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Uchaguzi Kanda ya Pwani kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Stephen Elisante wakati akifungua mafunzo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Kinondoni na Kata za jimbo hilo la jiji la Dar es Salaam.
Alisema wasimamizi wa Uchaguzi wanapaswa kutambua kuwa Uchaguzi ni mchakato unaohusisha taratibu mbalimbali kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, taratibu, maelekezo na miongozo iliyotolewa kisheria.
“Hivyo mnapaswa kuzisoma sheria hizo ili kuweze kutekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria…,tufanye maamuzi yetu kwa kujitambua, kujiamini na kutoogopa na kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza” alisema Elisante.
Aliwakumbusha wasimamizi hao wa Uchaguzi kuwa Tume imekuwa ikisisitiza kwamba Sheria za Uchaguzi hazikuacha ombwe katika kueleza jinsi gani masuala ya Uchaguzi yanatakiwa yatatuliwe.
Kwa upande wake Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni, Victoria Wihenge akiwasilisha mada ya Maelekezo kwa wasimamizi hao, aliwataka kutoruhusu matumizi ya utambulisho mwingine mbadala tofauti na ule ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeruhusu kutumika.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 61 (3) (a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, kimeipa mamlaka Tume kuidhinisha matumizi ya utambulisho mwingine tofauti iwapo mpiga atakosa kadi ya kupigia kura” alisema Victoria na kusisitiza kuwa:
“Vitambulisho vilivyoruhusiwa na Tume ni vitatu, Kitambulisho cha Taifa, Hati ya Kusafiria kwa maana ya Passport na Leseni ya Udereva, hivyo mtu akikosa kadi ya kupigia kura au vitambulisho hivyo hakuna utambulisho wowote utakaoruhusiwa ili mtu aweze kupiga kura”
Mafunzo hayo kwa wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi kwa ngazi ya Jimbo la Kinondoni na kata zilizoko kwenye jimbo hilo, yalijumuisha viapo kwa wasiamamizi hao walioapa kutunza sira na kujivua au kukiri kuwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Kinondoni pamoja na Jimbo la Siha na Udiwani katika kata 10 za Tanzania, unatarajiwa kufanyika tarehe 17 Februari mwaka 2018.
1384 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!