‘Ni bajeti ya neema kwa wananchi’

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wakati mwaka mpya wa kiserikali, maarufu kama mwaka mpya wa fedha ukianza, Watanzania wanapeleka matumaini yao katika utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Julai ya kila mwaka huwa ndio mwezi wa kwanza wa kuanza kutekelezwa kwa yale yaliyopitishwa bungeni ambayo aghalabu hubeba mwelekeo na matumaini ya Watanzania kwa miaka kadhaa ijayo.

Bajeti ya 2022/23 inatajwa kuwa ya viwango, ikitarajiwa kulainisha na kupunguza makali ya maisha kwa wananchi wengi kama si wote. 

Hali hii inatokana na vipengele kadhaa vilivyoainishwa na serikali kupitia mawaziri wa kisekta na kujumuishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.

Bajeti hii imejadiliwa na kuchanganuliwa ndani na nje ya Bunge kwa siku kadhaa; utaratibu ambao umekuwa ni wa kawaida sana nchini. 

Mitazamo ya wanazuoni wengi imedhihirisha kuwa Tanzania, taifa lenye shauku ya kukua kiuchumi, imejizatiti kikamilifu kwa kubuni, kusimamia na kupitisha bajeti inaelekea kutoa ahueni kwa wananchi wake na kuongeza kazi ya ukuaji wa uchumi, ajira na kipato.

Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Watanzania wanatarajia kuyapata majibu ya matatizo yao katika nyanja kadhaa zilizowagusa moja kwa moja.

Miongoni mwa vipengele vya Bajeti vilivyowagusa sana wananchi vipo katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, uwekezaji na biashara.

Hizi ni sekta za uzalishaji zinazowagusa na kutegemewa na Watanzania wengi.

Kutokana na umuhimu wake, sekta hizi zilijadiliwa kwa kina bungeni huku serikali sikivu chini ya jemedari wake, Samia, ikipokea na kurekebisha kila palipotakikana.

Mengi yamechukuliwa na kufanyiwa kazi kwa faida ya Watanzania.

Na sasa serikali inahakikisha kuwa mikopo ya ndani na nje inayochangia ukuaji wa deni la taifa ambalo bado ni himilivu, inaelekezwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo kupunguza makali ya maisha. 

Kwa maana hiyo hata ulipaji wake si mgumu kwa sababu upo katika mzunguuko wa kawaida ndani ya serikali.

Ieleweke kwamba deni hili ni ishara ya uwepo wa jitihada za kuleta maendeleo kwa taifa, kwa sababu fedha zinakwenda kwenye ujenzi wa miradi ya kimkakati kama barabara, madaraja, miradi ya umeme, maji na reli.

Katika kupunguza makali ya maisha, bajeti hii itachochea uchumi, ajira, kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, uwekezaji na biashara. 

Kujikita katika maeneo haya ni sahihi kwani kuzorota kwa sekta hizi kumezorotesha pia uchumi wa taifa.

Ama! Hakuna kilichoachwa katika bajeti hii kwani mbali na miundombinu na huduma za kijamii kama elimu, afya na maji; kaya maskini hazikusahaulika.

Kwa kupitia TASAF, kaya hizi zitanufaika na hili ni miongoni mwa mambo yenye tija yaliyozingatiwa kama chanzo cha kuongeza kasi ya ufufuaji na uimarishaji wa sekta ya uzalishaji na kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa mara ya kwanza, serikali inabeba mzigo kwa niaba ya Watanzania, kwa kutoa ruzuku katika huduma za kimkakati kama mafuta ya kula, ngano, mbolea na petroli. 

Ni maeneo haya ambayo yakiachwa kama yalivyo husababisha mfumko wa bei na kuongeza makali ya maisha kwa wananchi.

Ni mara kadhaa nchi imeingia kwenye uhaba wa mafuta ya kula. Imeshatokea pia mafuta kupanda bei maradufu kiasi cha kupandisha nauli kwenye vyombo vya usafiri. Kwa kupitia bajeti ya 2022/2023 ambayo serikali imetenga Sh bilioni 100 kwa mwezi kama njia ya kupunguza mfumko wa bei ya mafuta ya nishati nchini Tanzania.

Sasa wakulima wa korosho, mtama, mahindi, chai na wote katika nchi hii, watafanya kazi ya kuzalisha mazao yao pasi na changamoto kama zile zilizozoeleka.

Katika hili, serikali kupitia Wizara yake ya Fedha imeamua kwa dhati kupunguza makali ya maisha kwa vitendo sanjari na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Sekta za kipaumbele zinazogusa idadi kubwa ya watu kama kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na biashara zimefanyiwa kazi na kupatikana ufumbuzi kwa kiasi kikubwa.

Wakati anahitimisha bajeti yake bungeni mjini Dodoma, Waziri Nchemba alisema ni matumaini yao kuwa nchi itasonga mbele kwa kutatua kero nyingi na kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata ahueni katika maisha yao kwa namna moja ama nyingine.

“Serikali inalenga kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni tatu katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2025. Hii itafanyika kwa kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 8,500,000, sawa na asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifikapo mwaka 2030,” alisema Waziri Nchemba.

Aidha, imeongeza pia uboreshaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, miundombinu bila kusahau mkazo uliowekwa kwenye mradi wa kuhudumia kaya maskini chini ya mfuko wa TASAF.

Ilichofanya serikali ni kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa fedha kwenye vyanzo vyake pamoja na kuipanua bajeti yake kadiri iwezavyo. Kwa mfano, serikali ilitenga bajeti Sh trilioni 34.88 kwa mwaka 2020/2021.

Mwaka wa bajeti 2021/202 ilitenga Sh trilioni 36.3. Kama hivyo haitoshi, mwaka wa 2022/2023 imeweka bajeti ya Sh trilioni 41.48, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh trilioni 5.

Haya ni mapinduzi makubwa katika bajeti ya nchi yetu. Walau dhamira njema inaonekana. Ikumbukwe kuwa ni trilioni 2 tu zilizoongezwa katika bajeti ya 2021/2022 kutoka kwenye kiwango cha Sh 34.88 kutoka kwenye bajeti ya 2020/2021.

Katika mwaka huu 2022/2023 mapato ya ndani ni asilimia 68, wakati mikopo ya nje na ndani ikiwa ni asilimia 21, huku fedha za misaada zikitarajiwa kuwa asilimia 11 tu.

Hii inaonyesha kuwa serikali imewekeza zaidi katika ukusanyaji wa mapato yake kutoka kwenye vyanzo vya ndani. Na kwenye zile fedha za mikopo zitakazopatikana, zitakwenda moja kwa moja kwenye ujenzi wa miundombinu, madarasa na vituo vya afya ili kupunguza kama si kuondoa kabisa uzoroteshaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Miradi itasaidia kufungua uchumi na kuongeza kipato kwa nchi, ambacho asilimia ndogo inalipa deni huku faida kubwa ikienda kwa wananchi kutokana na kasi ya maendeleo.

Serikali haikopi kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ila kutumia mikopo hiyo kujenga miradi ya maendeleo. Katika hoja za baadhi ya watu kuwa serikali ina mpango wa kuileta upya kodi ya kichwa ni upotoshaji na ukosefu wa uelewa.

Kinachofanyika ni uboreshaji na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili nchi iweze kujiendesha kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani.

Mapato hayawezi kuongezeka endapo mkakati madhubuti hautawekwa wa kuwajua na kuwaelimisha wale wanaostahili katika suala zima la ulipaji wa kodi. Serikali haifanyi biashara. Kazi yake ni kuweka mazingira rafiki ya ulipaji wa kodi.

Kilichofanyika ni kuibua mchakato wa usajili wa wenye umri wa kulipa kodi na si kuwa na mpango wa kutoza kodi ya kichwa kama baadhi yao wanavyojaribu kupotosha.

Kodi itakusanywa kwa kuzingatia kipato kutoka kwa wale waliotambuliwa na aina ya biashara wanazofanya. Wale wenye vipato vikubwa nao watatozwa kodi kulingana na sheria zilizopo. Hili likifanyika kwa ukamilifu, litaongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi kwa kiwango cha juu.

Kazi ya serikali itasaidia kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kufanya makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawana uwezo wa kutunza kumbukumbu na kutengeneza hesabu za biashara zao.

Kwa kuliangalia hilo, utagundua kuwa serikali inajibu maswali yote kutokana na uwapo wa bajeti bora na shirikishi kwa viongozi wa wizara na wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi wao.