Leo nimeona niandike mada inayogusa maisha ya kila Mtanzania –  biashara. Naandika mada hii kutokana na mwenendo usioridhisha unaoonesha kuwa biashara nyingi hapa nchini zinakufa. 

Kwa muda mrefu tumekuwa tukiambiwa kuwa Tanzania ni taifa la wakulima na wafanyakazi. Ni kwa bahati mbaya, hao wakulima na wafanyakazi wanastahili heshima, ila uchumi una misingi yake.

Kwa siku za karibuni wafanyabiashara wengi hapa nchini wamefunga biashara. Nasikiliza kauli zinazotolewa na baadhi ya wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, akiwamo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuwa wanaofunga biashara walikuwa wapiga dili.

Nimepita maeneo mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam, biashara zinazohusiana na vinywaji kama kwenye baa, vioski na vibanda vya kuuza bidhaa ndogo ndogo nyingi zimefungwa. Hata kampuni nyingi ndogo zimefungwa. Zipo kampuni kubwa ambazo hazijalipa mishahara hadi hivi ninavyoandika makala hii – si ya mwezi Februari tu, bali hadi Novemba, mwaka jana.

Sitanii, ukipita katika maeneo mengi ya nchi hii ujenzi wa nyumba umesimama. Nyumba nyingi zilizokuwa katika ngazi ya madirisha zimepigwa ganzi. Idadi ya mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda mikoani imepungua, na hili tumelishuhudia mwisho wa mwaka. Hoteli nyingi zimefungwa na baadhi zimegeuzwa hosteli.

Ninao marafiki zangu waliokuwa wemeanzisha biashara ya kufuga kuku na samaki, hivi ninavyoandika makala hii tayari mabanda wameyafunga. Madhara ya baa kufungwa mahitaji ya kuku yameshuka, na kushuka kwa mahitaji ya kuku kumefanya bei ya kuku ishuke pia. Leo, kuku wa (kizungu) anauzwa hadi Sh 4,500 kutoka wastani wa Sh 8,000 mwaka mmoja uliopita.

Sitanii, nchi inaendeshwa kwa kodi. Kodi zinapatikana kwa njia moja tu ya msingi, makato yatokanayo na faida ya iliyopata biashara. Ipo kodi nyingine inayolipwa ni ile ya wafanyakazi kukatwa kodi ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE). Mishahara ya wafanyakazi hutokana na ama faida kwa kampuni binafsi au makusanyo ya kodi kutokana na faida zilizotengenezwa na kampuni kwa Serikali.

Nchi zilizoendelea duniani kama Marekani, Uingereza, Japan zinakusanya kodi kubwa kutokana na kampuni za watu binafsi au zinazomilikiwa na Serikali kama GM Motors, General Electric, Boeing, Sony, Suzuki, Toyota na nyingine kutengeneza faida kubwa na zikalipa kodi kubwa serikalini. Hapa kwetu kampuni kama TBL ilikuwa inalipa kodi ya wastani wa Sh bilioni 95 kwa mwaka, ila sijui kwa baa nyingi kufungwa italipa shilingi ngapi zamu hii.

Jumapili nimekutana na rafiki yangu mmoja ambaye kampuni yake haijalipa mishahara hata ya mwezi Januari, 2017 anahaha kutafuta mkopo aweze kulipa Kodi ya PAYE na SDL kabla ya tarehe ya mwisho leo, ambayo ni kila tarehe 7 ya mwezi mpya. Ameniambia Januari alikopa akalipa kodi hiyo, Februari anakopa, ila ikifika Aprili biashara haijaonesha matumaini, atalazimika kufunga biashara.

Sitanii, hali hii imenitisha. Imeniogopesha. Hata sisi hatuna tofauti kubwa na ndugu huyu. Kwa sasa uwezo wa watu kununua bidhaa na huduma umepungua kwa kiasi kikubwa. Wadeni wetu kila tukiwaendea wanakuonesha nao wanakodai. Ni katika hatua hiyo kushindwa kupata mishahara si jambo la kushangaza kwa sasa.

Hofu yangu kubwa ni iwapo mkondo huu utaendelea, nchi itasimamia miguu ipi! Ikiwa kampuni na watu binafsi watafunga biashara wakashindwa kulipa kodi, maana yake ni kwamba Serikali itabaki na njia mbili tu. Moja ni kutumia akiba yote iliyonayo na ya pili ni kutegemea wafadhili watoe misaada kuendesha miradi kuziba pengo linalotokana na ukosefu wa kodi.

Sitanii, zamani nchi yetu ilikuwa inakusanya kodi ya kichwa si kwa sababu nyingine. Nchi haikuwa na viwanda. Tumekuwa kwenye Ujamaa kwa muda mrefu, hivyo hakukuwapo mtu anayefanya biashara na matokeo yake ilibidi kuwakamua wananchi kwa kutoza kodi ya kichwa bila kujali wataipata wapi. Napata shida kuwa tukiendelea na kasi hii ya biashara kufungwa, Serikali itashtuka makusanyo yameshuka na njia rahisi itakuwa ni kuanzisha tena kodi ya kichwa kuziba pengo.

Naomba kushauri kuwa tulipofikia pametosha. Kama wapo wapiga dili watafutwe wadhibitiwe, ila watu wachache wasio waadilifu wasiwe chimbuko la kuua uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kukata mzunguko wa fedha na hatimaye Taifa zima kwa kukosa mahala pa kukusanya kodi. 

Hatua ya Benki Kuu kushusha riba kutoka asilimia 16 hadi 12, inaweza kuwa heri au ni ishara kuwa kengele zinalia. Naomba Serikali isifurahie biashara binafsi kufa, maana wanaoajiriwa huko ni wengi na kodi zinazolipwa si za kubeza.

By Jamhuri