PARIS, UFARANSA

Liverpool inalitaka taji la saba la Ulaya pamoja na kulipa kisasi cha fainali ya Ligi ya Mabingwa 2018 dhidi ya Real

Madrid inayosaka kombe lake la 14 la mashindano hayo makubwa zaidi kwa klabu barani humo.

Liverpool watakuwa wenyeji kwenye Uwanja de France mbele ya Real Madrid inayoongozwa na mshambuliaji

nyota raia wa Ufaransa, Karim Benzema, anayesaka tuzo ya mchezaji bora wa dunia na ufungaji bora wa Ligi ya

Mabingwa msimu huu.

Msimu huu Liverpool imekuwa katika ushindani wa kiwango cha juu, ikiweka rekodi ya pekee katika mashindano haya.

Katika michezo 12, imepoteza mechi moja tu katika raundi ya 16 bora, mchezo wa marudiano dhidi ya Inter

‘Nerazzurri’ Milan, waliotoa ushindani kwa kikosi cha Jurgen Klopp.

Wengine waliojaribu kuwashtua ni Villarreal walipofunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya Liverpool kubadili matokeo kipindi cha pili na kupata ushindi wa 3-2.

Kocha wa Liverpool, Klopp, amekuwa na mafanikio makubwa na mfumo wake wa 4-3-3 akitegemea zaidi kasi

ya washambuliaji Sadio Mane, Diogo Jota, Luis Díaz na Mohamed Salah kumaliza wapinzani.

Hata hivyo, Klopp anapaswa kujifunza kitu kwa kile kilichowakuta Manchester City, PSG na Chelsea wakati atakapokuwa akishambulia dhidi ya Real Madrid.

Real, chini ya mkongwe Benzema na chipukizi Vinicíus Júnior, wamekuwa washambuliaji hatari wakitumia vema

mipira inayotengenezwa na viungo wakongwe Toni Kroos na Luka Modrić kufunga mabao.

Ikitumia mfumo wa 4-3-3, Madrid ni salama chini ya kipa Thibaut Courtois na beki wa kati Éder Militao; huku safu ya kiungo ikiundwa na wazoefu Casemiro, Modrić na Kroos wenye uwezo mkubwa wa kukaa na mipira na

kupiga pasi nzuri za mwisho.

Mbele yupo Benzema akisaidiwa na chipukizi Vinícius na Federico Valverde wenye uwezo mkubwa wa kutumia

nafasi chache wanazopata kufunga mabao.

Fainali hii inaweza kushuhudia mabao mengi zaidi yakifungwa kutokana na ubora wa safu za ushambuliaji wa timu hizi mbili kwa sasa.

Kocha Klopp na mpinzani wake Carlo Ancelotti wa Real wamekutana mara 10 katika mashindano mbalimbali,

katika Ligi ya Mabingwa mara sita, Ligi Kuu England (3), na mara moja Kombe la FA.

Muitaliano akishinda michezo minne dhidi ya mitatu ya Mjerumani huku wakitoka sare mara tatu. Hii ni fainali ya nne kwa Klopp kufuzu huku mara ya kwanza akifuzu akiwa na Borussia Dortmund (2013), kabla ya 2018, 2019 akiwa na Liverpool na kumfanya kuifikia rekodi ya makocha Sir Alex Ferguson na Marcello Lippi.

By Jamhuri