Ni muhimu sana kujali tunavyoyatekeleza malengo yetu

Ndugu Rais, haiwezekani kila jambo linalofanywa na Serikali liwe ni jambo baya au halifai! Kwamba Serikali isiwe hata na jema moja inalolifanya? Haiwezekani! Swali muhimu hapa ni kwanini Serikali wakati mwingine inajifikisha mahali mpaka kuonekana hivyo kwa baadhi ya wananchi?
Serikali ya watu mara nyingi inakuwa imejiwekea malengo yake. Malengo
 kwa ajili ya ustawi wa wananchi na nchi yao. Kujiwekea malengo mema ni jambo moja. Kuyatekeleza hayo malengo mema ni jambo lingine! Hapa ndipo umuhimu wa kujali namna tunavyotekeleza malengo yetu mema unapojidhihirisha. Utekelezaji mbovu wa malengo mema huyafanya malengo yenyewe kuonekana ni upuuzi na hivyo kuonekana mabaya au hayafai kabisa. Hilo likitokea ndipo Serikali huonekana kila jambo inalolifanya kuonekana baya au halifai mbele ya macho ya wananchi.
Mwishowe Serikali itaonekana haifai.


Lengo la kuhakiki vyeti vya wafanyakazi lilikuwa ni lengo jema na muhimu sana. Lakini lilivyotekelezwa limeacha aibu kubwa kwa Serikali.
Kumbuka Serikali ni Rais! Angella Kairuki, waziri mwenye dhaman amelitibua lengo zima la kuhakiki vyeti vya wafanyakazi. Kuwa na wafanyakazi wa vyeti feki au vyeti vya kugushi ni jambo la aibu. Jambo la aibu halianikwi hadharani! Dunia itawaonaje Watanzania wanaokwenda kuomba kazi huko nje? Ni nchi gani haina wafanyakazi wenye vyeti vya kugushi? Lakini je, wao wanatutangazia?


 Kairuki, waziri wetu, amediriki kumwambia mkuu wa nchi tena hadharani kuwa; “Kigezo cha elimu cha wanasiasa ambao ndiyo viongozi wetu ni kujua kusoma na kuandika, basi!” Na kwa kigezo hicho aliamua kuto hakiki vyeti vya wanasiasa pamoja na vyake!
Wanasiasa anaowajua kwa ufahamu wake aliwataja kuwa ni mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na madiwani. Lakini hawa ndiyo viongozi wanaoingoza nchi hii kwa sasa! Kwa kigezo cha elimu yao ya kujua kusoma na kuandika basi, wataweza kweli kutujengea Tanzania ya viwanda? Kutarajia Tanzania ya viwanda ni sawa na kulala chini ya mnazi ukisubiri embe lidondoke!


Ndugu Rais, kutokana na orodha ya wanasiasa alionao kichwani mwake ameonyesha hata hafahamu kuwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya si wanasiasa. Yawezekana aliyasema hayo kuficha nia yake ya kumbeba mtu. Hii kwake imekuwa ni bahati mbaya kwa sababu ametumia nguo alizovaa mwilini akazifanya mbeleko, akabebea gunia lake la misumari!
Ndugu Rais, ulipomzima haraka Waziri Harrison Mwakyembe alipokuja na ndoa zake za vyeti vya kuzaliwa, uliwathibitishia wananchi wako kuwa uko kwa ajili ya kulinda ustawi wao. Viongozi wa wananchi lazima watambue kuwa heshima wanayoitaka kutoka kwa wananchi, haitengenezwi na wananchi. Inatengenezwa na viongozi wenyewe. Kiongozi anayewapelekea wananchi upuuzi, wananchi watamrudishia upuuzi!


Baba, ni kipi kilikupa ukakasi hata usitengue ya huyu mama kama ulivyotengua ya Harrison Mwakyembe? Lengo jema la Serikali njema, limetekelezwa kwa kuiachia nchi sononeko kwa kiwango cha mwisho!
Katika karne tuliyomo, ya sayansi na teknolojia, huku ni kuwakebehi wananchi masikini na wanyonge wa nchi hii! Na kama ni kweli hicho ndiyo kigezo cha elimu kwa viongozi wetu, basi viongozi wajinga katika nchi hii hawatakwisha!
Ndugu Rais, ili upate kutekeleza vema malengo mema uliyonayo kwa nchi hii na watu wako, ulisukumwa na dhamira yako njema, ukawaendea viongozi wako wa kiroho, ukawaomba wakuombee, ili urais usikufanye uwe mwenye kiburi! Lakini, huja ni kwa udhaifu wa kibinadamu, hawakuiona dhamira yako hiyo njema! Kama hawa viongozi wa dini wangekuwa wanamtegemea Mungu peke yake kwa kila jambo, katika hili, angewajaza ujasiri nao wangekwambia baba, tuache kiburi! Hao washauri ulionao ambao unawalipa mshahara mwema, ni Mungu ndiye alikupatia! Bado amekupa na wengine wa ziada ambao anawalipa mshahara mwenyewe, ili waendelee kukushauri kwa ajili ya ustawi wa waja wake. Kama yeye anawasikiliza, iweje wewe usiwasikilize?


Kama viongozi wako wa kiroho wangetambua kuwa kukushauri ni moja kati ya majukumu yao, wangekushauri kuiheshimu Katiba ya nchi katika ukamilifu wake. Nchi bila Jaji Mkuu haijawa na mihimili mitatu.
Mwenyezi Mungu ameijalia nchi hii majaji wema wengi, iweje asifae hata mmoja kuwa Jaji Mkuu? Hata huyu anayekaimu, naye hafai? Badala yake Baba Askofu akasema atamwomba Mungu akupatie washauri wazuri. Baba Askofu angekuambia hao washauri wazuri huyo Mungu atawatoa wapi? Kamwe, Mungu hawezi kukuletea malaika wakukushauri!


Ndugu Rais, hata tukiwakubalia hao wanaosema washauri wako si wazuri, lakini wewe mwenyewe baba, je, kwa ubinadamu wako, kelele zote hizi, zilizoijaza nchi; huku za kuvunja katiba kwa kupiga marufuku mikutano; kule kilio cha wananchi wanataka Bunge lao ‘live’; hapa yuko
Bashite na vyeti vyake; vyombo vya habari vinavamiwa na watu wenye silaha za kivita; wananchi wanatekwa na kuteswa bila hatia yoyote; kweli unaona yote haya ni sawa sawa tu? Ah! Baba, haya! Na sisi hapa tunaandika nini kama siyo ushauri kwa Rais wetu? Iweje Muumba atulipe pa kubwa hivi kama hatumpendezi?
Ndugu Rais, namuomba Muumba wangu anapozuru wengine na mimi asinipite!
Aniguse ili haya niandikayo yawaguse watawala wetu aliotupatia kama Kristu alivyomgusa Batimayo akaona, nao wapate kuona madhila wanayowafanyia waja wake!

919 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons