JIJI hili sasa hivi hakuna kingine kinachozugumzwa wala kusikilizwa kupita michezo ya Olimpiki. Nimekubali kwamba ni michezo mikubwa na faida yake kwa waandaaaji si ndogo.

Ukishaona watu wanafanya kampeni kubwa kama Uingereza ili tu waandae kitu hiki kwa mara ya tatu, lazima ujue kuna manufaa.

Kama mnavyojua wapenzi wasomaji wangu, Waingereza ni watu wanaopenda kujitangaza wanapofanya jambo lao, hata kama ni kunywa chai na watu fulani. Hii ina msingi wake katika historia na utamaduni wa taifa hili. Ndilo tunaloweza kusema ni mama wa mataifa mengine mengi, kwa sababu iliyatawala, ikayaongoza na kuyasimamia kabla ya ama kuyaandaa yajitawale na mengine yakapigana kujitoa kwenye makucha yake.


Yote kwa yote tunakaa pamoja na kusema adumu mfalme, adumu malkia! Mpaka sasa hata baada ya kuachia uhuru wa nchi nyingi, bado malkia ana nguvu na ni mkuu wa mataifa kadhaa hapa Ulaya na Amerika.

Olimpiki ilipambwa ikapambika bwana, watu walicheza na kweli nilifurahia dansi na mashamushamu ya wasanii wale 15,000 waliokuwa chini ya uratibu wa msanii Dany Boyle.


Sherehe zile za ufunguzi zilizochukua zaidi ya saa tatu kurushwa, zimesikilizwa na kutazamwa na watu zaidi ya bilioni nne. Mungu akupe nini tena kama unataka kuitangaza nchi yako na utajiri wake? Nakumbuka watu waliokuwa wakipiga vijembe uandaaji wa mashindano haya wakati uchumi unayumba walinyamazishwa vizuri. Waziri Mkuu, David Cameron alikatisha tambo zao na kuwaambia haya ni matangazo makubwa kabisa kuwahi kutokea, akataka wajipange wawasaidie wanamichezo watwae dhahabu.


Angalia jinsi ufunguzi ulivyojenga taswira ya Uingereza tangu enzi zile hakuna teknolojia kama ya leo. Uliona wale kondoo walivyokuwa wamezubaa kijijini? Mimi niliwaona kikavuta hisia mpaka miaka hiyo ambayo sikuwa nimezaliwa. Yaani msanii Boyle na kundi lake walijenga mazingira kama ya ujima, watu wakiwa vijijini na kondoo na mbwa ambao sijui kama wamebaki tena wengi sasa. Vibanda vya makuti na hali ya kudumu ya mawingu ya mvua.


Baada ya hapo ikaja awamu nyingine, ambayo huwa nasema ndipo Uingereza ilipata nguvu. Kwa wale wa kwetu wangesema ndio ilitoka jando na baada ya kufundwa ikaanza uzalishaji mkubwa wa viwanda aina nyingi tu.


Hii nguvu ya viwanda, uzalishaji na kadhalika ndiyo iliwafungua akili na kutoka nje ya kisiwa hiki kikubwa kuangalia huko duniani kuna nini. Wakaiona Amerika, Afrika na Asia wakaingia na kuendeleza kazi za uzalishaji na kuhakikisha wanapata vitu vyote vinavyotakiwa kwa ajili ya uchumi – watu, zana za kazi na maeneo ya kazi. Mitaji si walikuwa nayo bwana!

 

Igizo liliishia kwa kutuonesha Ulaya ya kisasa, enhe, Uingereza ya leo yenye majengo makubwa ya ghorofa za juu na chini, treni za kasi za juu na chini ya ardhi – wenyewe wanaita ‘tube’. Tukaiona ‘Big Ben’ ikigonga na kila aina ya teknolojia. Ujumbe gani mwenzangu ulipata kama ulitazama? Nasema kutazama kwa sababu waliofanikiwa kuhudhuria ni wateule. Kama hukutazama wala kusikiliza bado hujachelewa, unaweza kupata nakala. Kuna mbongo yako, jitume na ujifunze ufunguzi huu una maana gani kwako na kwangu.

 

Taifa kubwa limetumia zaidi ya paundi milioni 27 kuandaa sherehe ile ya siku moja ya ufunguzi.

Wewe unafikiri ni hasara? Angalia matangazo ya biashara zinayopata televisheni na redio, wakuu 120 wa nchi na serikali walifika na labda kulala walau siku mbili kama si zaidi. Unajua bei ya vyumba vyao? Vyakula vyao je? Kinywaji wanachopata na vile vya wapambe wao, askari wao na wake au waume zao? Bado kuna msafara wa kitaifa, na wote unakula Uingereza, vya Waingereza.

 

Mamilioni ya watu wameingia Uingereza, kwa hiyo wameinunua paundi. Kanuni ya uchumi inasemaje mwanangu? Kukiwa na mahitaji zaidi bei hupanda, kwa hiyo pauni inazidi kuimarika.

Hapo ilipo tu pauni ndiyo sarafu ya thamani kubwa zaidi inayotumika maeneo mengi zaidi duniani kote, sasa uitafute na shinikizo za Olimpiki ukiwa na madafu yako ya Burkina Faso, sijui Cape Verde au Afghanistan, si itapanda tu?


Jingine lililojitokeza hadi sasa ni dhahiri kuwa ukiwa na utajiri mkubwa, basi unaweza kila kitu. Tunachoshuhudia sasa ni mashindano kati ya China, Marekani na Uingereza. Medali walivyozipata inadhihirisha pasi shaka kuwa nchi hizi zinashindanisha uchumi wao kama inavyoonyesha orodha hii.

Nafasi haitoshi leo, lakini tungeweza kujadili mengi yanayosaidia kiuchumi kwa michezo kama hii na kisha tuangalie sisi hiyo Kagame Cup, Challenge Cup na mengine hatuwezi kupanda zaidi na kuandaa ya Afrika nzima tukidhamiria? Penye nia pana njia, hebu tuamke. Tuwasiliane.


leejoseph2@yahoo.com


893 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!