Kuna taarifa zisizo na shaka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amehakikisha anapeleka taarifa ya ‘kutungwa’ kwa Waziri Mkuu.

Amependekeza Pori Tengefu la Loliondo lifutwe, badala yake kuanzishwe Hifadhi ya Jamii (WMA). Haya ni mapendekezo yake, wala si ya wajumbe wa Kamati.

Hili jambo hatuna budi kulisema mapema kwani endapo ulaghai wake utaaminiwa na viongozi wakuu wa Serikali, huo utakuwa mwisho wa uhifadhi, si kwa Loliondo tu, bali pia kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Nimeipata taarifa ya awali ya kile kinachoitwa na Gambo kuwa ni mapendekezo ya Kamati iliyoundwa kutafuta suluhu ya mgogoro wa Loliondo. Kama haya niliyoyaona ndiyo yatakayofikishwa, au yaliyofikishwa kwa Waziri Mkuu, naomba tutoe hadhari mapema ili tusiwe sehemu ya kizazi kitacholaaniwa kwa kuushuhudia uongozi na kuamua kukaa kimya.

Taarifa hii imeandaliwa kibabe na Gambo na wafuasi wake. Naamini vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu wa kuwaeleza ‘wakubwa’ ukweli wa mambo maana Gambo amezoea kusema ‘tunatunga mambo’ au ‘tumehongwa kumchafua’.

Kwenye kile anachokiita “​Mapendekezo yaliyoridhiwa na Kamati ya Majadiliano”, bila aibu, Gambo anabariki uongo kwa kusema: “Baada ya Majadiliano na Mapendekezo ya Makundi 3 (Wizara ya Maliasili na Utalii (Wahifadhi), Wawekezaji, na Wawakilishi wa Jamii – Madiwani, Viongozi wa Mila, Wenyeviti wa Vijiji); kwa kila upande kuwasilisha hoja zake za msingi; na kufuatia maoni ya wananchi (kupitia mikutano ya dharura), Wataalamu wa Sheria za Uhifadhi, Ardhi, Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa, na Wilaya; na kwa kuzingatia maslahi mapana ya aina 3 yaliyotajwa awali (Uhifadhi, Uwekezaji, na Hatima ya Maendeleo ya wananchi). Yafuatayo yaliridhiwa na kukubaliwa kuwa Pendekezo la Msingi (jumla) ya kumaliza mgogoro:

“Eneo la km za Mraba 1500 liendelee kutumika kwa madhumuni ya Uhifadhi na Utalii chini ya Utaratibu wa Hifadhi za Jamii za Wanyampori (Wildlife Management Areas – WMAs) chini ya Kanuni za WMAs za Mwaka 2012.

“Hata hivyo, kwa sababu ya uzoefu wa mapungufu (upungufu) yaliyopatikana kutoka WMAs zilizopo nchini kwa sasa katika uendeshaji wake (hasa kifungu cha 36 & 37) imependekezwa WMA itakayoanzishwa Loliondo iwe ya kipekee, na ikifanikiwa iwe ndiyo ya mfano/kiigizo (model) cha WMAs zenye ufanisi. Hivyo, kuelekea hatua ya kuanzisha WMA ya Loliondo yafuatayo yafanyike kuanzia sasa:

(i) Wanavijiji wenyewe kwa hiari yao wamekubali kuwa wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Wilaya kuwa katika eneo lililopendekezwa na kuwekewa alama za mpaka (km za mraba 1500?); wataondoa kabisa makazi yote (maboma) kwa hiari yao, watazuia kabisa kuanzisha na kuendesha kilimo cha mazao (kwa hivi sasa hakuna kilimo).

 (ii) Wanavijiji wamekubali na kuafiki kuzuia kabisa uingizaji na ulishaji wa mifugo katika kipindi chote cha mwaka, na endapo kutatokea hali ya ukame uliokithiri, basi wananchi wakae na wawekezaji waliopo kwa sasa katika maeneo hayo (OBC, Andbeyond/Kleans Camp, na Bufallo Luxury Lodge) ili kuweka utaratibu nzuri wa maeneo ya maji na malisho kwa mifugo.

 (iii) Kwa hivi sasa Wawekezaji waliopo na mikataba yao, waendelee kuwepo na kushirikiana miongoni mwao na wanavijiji katika uhifadhi, maendeleo ya jamii, na matumizi ya miundombinu ya umma iliyopo ikiwemo Uwanja wa Ndege.” Mwisho wa sehemu ya ripoti ya Gambo.

Kuanzishwa kwa WMA katika Loliondo ni jambo lisilowezekana. Tayari mvutano mkali umeshajitokeza hata kabla mamlaka za juu zikiwa hazijaamua. Huu ni uthibitisho kuwa Pori Tengefu halikwepeki.

Ili WMA iweze kuanzishwa, ni lazima kwanza mamlaka husika ziweke matumizi bora ya ardhi ya kilometa za mraba 4,000. Kilometa za mraba 1,500 ziwe kwa ajili ya Pori Tengefu Loliondo na kilometa za mraba 2,500 ziwe kwa ajili ya matumizi ya ardhi ya vijiji vya kata saba za Piyaya, Arash, Oloosoito-Maaloni, Oloirien-Magaiduru, Oloipiri, Soit-Sambu na Ololosokwan. Baada ya hapo ndipo Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro iweze kusimamia hizo WMA.

Ili WMA ziweze kuanzishwa kwenye ardhi ya vijiji ni lazima vijiji vya kata zote saba vikubaliane ugawaji wa vijiji na kuridhia mipaka ya ardhi ya vijiji vyao ili vipimwe na hatimaye viweze kusajiliwa na kupata hatimiliki na vyeti. Bila kuwapo kwa hatua hiyo WMA haziwezi kuanzishwa Loliondo.

Kuna vikwazo vingi vya kuanzishwa kwa WMA. Hapa nitajaribu kutaja kwa ufupi. 

Mosi, ni changamoto ya kiukoo kwa kabila la Wamaasai waishio kwenye tarafa za Loliondo na Sale.

Tofauti za kiukoo kati ya koo za Loita, Purko, Kisongo, Sale na Laitayok zilizopo wilayani Ngorongoro kwenye tarafa hizo zitasababisha migogoro juu ya uanzishwaji wa WMA katika vijiji vya kata saba za Ololosokwan, Soit-Sambu, Oloipiri, Oloirien-Magaiduru, Oloosoito-Maaloni, Arash na Piyaya. Historia inaonesha kuwa migogoro ya kudumu ipo kati ya vijiji vya koo hizo popote pale zinapopakana na zimeshindwa kuelewana. 

Kwa mfano, kuhusu mipaka ya vijiji, maeneo ya malisho, vyanzo vya maji na miradi ya kushiriki pamoja vina matatizo mengi. Kama vijiji vingi vimeshindwa kuelewana, seuze kwenye hili la WMA? Ni wazi kuwa kuanzishwa kwa WMA kutapata upinzani mkali. Hivi ninavyoandika makala hii, tayari mvurugano umeshaanza. Lakini kwa kuwa DC wa Ngorongoro na RC wa Arusha wanajua walichoahidiwa pindi Serikali ikiridhia WMA, wameamua kumdanganya Waziri Mkuu kwa kumwandalia taarifa ya upotoshaji.

Changamoto za kijiografia za mipaka baina ya vijiji vya kata saba na Hifadhi ya Taifa Serengeti ni kubwa na nzito. Kuwapo kwa Pori Tengefu maana yake ni kuzuia uharibifu wa uhifadhi, mazingira, na vyanzo vya maji. Ni kuzuia uharibifu au tisho lolote la kuiua Serengeti ambayo kwa kweli ni ‘hifadhi ya dunia’.

Kuwapo kwa Pori Tengefu maana yake ni kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji vya mito mikuu ya Grumeti na Pololeti inayounganika na kumwaga maji ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ajili ya mamilioni ya nyumbu na wanyama wengine wanaohama kutoka Pori la Akiba la Maasai Mara nchini Kenya kwenda Hifadhi ya Taifa Serengeti. Pia ni kunusuru uangamizaji wa misitu na viumbe wengine wenye faida kubwa kwa uchumi wa nchi yetu. 

Kwa ufupi kabisa ni kuwa kuendelea na Pori Tengefu maana yake ni kuhifadhi ikolojia ya Serengeti na Loliondo na kuifanya rasilimali hii iendelee kuwa tegemeo la kiuchumi kwa wana Loliondo, Ngorongoro, Arusha, Taifa na dunia.

WMA zitakapoanzishwa kwenye mpaka na Hifadhi ya Serengeti bila kuwekwa ushoroba au buffer zone, Wamaasai ni lazima wataingiza ng’ombe hifadhini. Hakuna wa kuwazuia. Hawataishi kwenye mifugo tu, bali tujiandae kuona maboma yakijengwa ndani ya Serengeti. Hapa ieleweke kuwa kuna genge la wanasiasa na watu wenye NGOs wanaowashawishi Wamaasai kudai ardhi ‘yao’ wanaodai kuporwa tangu miaka ya 1950.

Njia sahihi ya kukabiliana na tishio hili ni kutenga kilometa za mraba 1,500 ili ziwe ushoroba/buffer zone. Hatua hiyo itasaidia kuzuia ng’ombe kuingizwa hifadhini, itazuia shughuli za binadamu ndani ya Pori Tengefu Loliondo na kwa kweli ni kuzuia kifo cha Serengeti.

Changamoto za kiikolojia kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti na Loliondo ni nyeti kuliko vitu vyote. Kwa hali ilivyo sasa jamii ya kifugaji ya Kimaasai imeshindwa kusimamia na kuendeleza Pori Tengefu. Idadi ya wanyamapori imepungua mno, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira na vyanzo vya maji vilivyosababishwa na wingi wa mifugo, makazi ya watu na kilimo cha kibiashara.

Changamoto za kimfumo: Kumekuwa na mivutano na kutoelewana baina ya wadau kwa kila mmoja kushikilia mfumo wake ambao anaona unafaa kadri ya maslahi yake binafsi. Kwa mfano, wapo wanaopendelea mfumo wa ardhi ya kimila, mfumo wa ardhi ya kijiji, mfumo wa ardhi kata saba/mfumo wa Hifadhi ya Jumuiya (WMA), mfumo wa ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo (LGCA) na mfumo wa Pori la Akiba. Sharti upatikane mfumo mmoja wenye tija kwa uchumi endelevu  na utakaokidhi uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti na Loliondo. Ni wazi kwamba Pori Tengefu Loliondo ndiyo uvumbuzi kati ya mifumo yote hii.

Mfumo wa Pori la Akiba ni mgumu kwa jamii na mwekezaji, WMA ni mfumo mgumu kwa mwekezaji, Serikali na jamii kwa ajili ya migogoro itakayokuwapo baadaye. Pori Tengefu ni mfumo shirikishi na wenye manufaa kwa wadau.

WMA hazijaonesha mafanikio yoyote ya maana kwenye uhifadhi, na ndiyo maana hapo juu Gambo anasema: “Imependekezwa WMA itakayoanzishwa Loliondo iwe ya kipekee, na ikifanikiwa iwe ndiyo ya mfano/kiigizo (model) cha WMAs zenye ufanisi.”

Sentensi hii ukiisoma inathibitisha wazi kuwa hakuna WMA iliyofanikiwa! Ndiyo maana ‘anaota na kuomba’ hii itakayoanzishwa ifanikiwe na iwe ya mfano!

Nimeelimisha, nimehadharisha na nimeonya kuhusu nia ovu ya Gambo na wenzake Loliondo. Nimetekeleza wajibu wangu.

By Jamhuri