Mteja ni mfalme

Wiki ya pili ya Oktoba huwa tunaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja. Yawezekana huwa unapokea ujumbe wa kukutakia heri katika wiki hiyo kutoka kwa kampuni mojawapo kubwa ambayo huwa unatumia huduma zake.

Nilipokea ujumbe kutoka Vodacom uliosomeka, “Heri ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2019. Asante kwa kuchagua Vodacom. Ni matarajio yetu kuendelea kukupatia huduma bora zaidi. Yajayo yanafurahisha. Upo tayari?”

Lakini pia Benki ya NMB iliniletea ujumbe mara mbili, wa kwanza ulisomeka, “Wewe ni mteja wa kipekee! Endelea kufurahia huduma BORA na NAFUU katika Wiki hii ya Huduma kwa Wateja na siku zote. Asante kwa kuchagua NMB!”

Ujumbe wa pili ulisomeka hivi, “Mpendwa mteja, kheri ya wiki ya Huduma kwa wateja! Wewe ni mteja wa kipekee! Ni furaha yetu kukuhudumia. #Ubora Upo Hapa. #Kila kitu kwa NMB Mkononi.”

Benki ya CRDB hawakuwa nyuma, kama mteja wao nilipokea ujumbe huu pia, “Ndugu Mteja, katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, tunakushukuru kwa kutuchagua na kuwa sehemu ya mafanikio yetu. Ulipo Tupo, tupo tayari kukuhudumia.”

Inawezekana na wewe pia ulipokea jumbe kama niliopokea mimi. Imesemwa kuwa ‘Mteja ni mfalme’.

Mfalme ni mtu anayeheshimiwa sana. Sehemu zenye utawala wa kifalme watu hupita mbele yake na kumwinamia kabla hawajaanza kutaja shida zao. Hivi ndivyo mteja anavyopaswa kufanyiwa.

Tatizo kubwa lililopo kwa wafanyabiashara wengi na wajasiriamali ni kwamba wanafikiri huduma kwa wateja hutumiwa tu na kampuni kubwa. “Fanya biashara kana kwamba unashindana na kampuni kubwa,” alishauri Mark Cuban mtaalamu wa mambo ya biashara na mwandishi wa vitabu.

Katika kitabu changu cha NAMNA YA KUWA MTAALAMU UKIWA BADO UNASOMA nimeandika hivi, “Usifikiri kwamba huduma kwa wateja inatumiwa na makampuni makubwa ya simu na mabenki tu. Hapana! Wewe pia unahitaji kuwa na huduma nzuri kwa watu wanaokuzunguka. Ongea kwa ukarimu uwe mtu wa watu.”

Unapokuwa na biashara yoyote kusudia kutoa huduma ya viwango vya juu kwa wateja wako. Hakikisha watu wakija kununua bidhaa kutoka kwako wanaondoka wakitoa tabasamu na kuahidi kurudi tena.

Kuwa mtu wa tabasamu muda wote, hata mteja akikukasirisha usioneshe kuwa na hasira, mjibu kwa upole na kwa ukarimu. “Kama mtu hawezi kutabasamu, haruhusiwi kufungua duka,” ni msemo wa Kichina.

“Badala ya ‘kufokasi’ katika mashindano ‘fokasi’ kwa wateja,” anasema Scott Cook. Wateja ndio huifanya biashara yako ikue, lakini pia wateja ndio wenye uwezo wa kuifanya biashara yako ife.

Ukiwa bosi wa kampuni hakikisha timu yako yote inatoa huduma nzuri kwa wateja, siyo wale tu wanaokaa mbele katika dawati la kuwasikiliza wateja.

Mhudumu wa mgahawa anaweza kuwa anatoa huduma nzuri kwa wateja, lakini mpishi anapaswa kuhakikisha anapika chakula kitamu ili wateja wakila siku moja watamani kurudi, hivyo mpishi asichukulie ‘poa’ kitengo chake kwani kina mchango mkubwa kwa wateja.

Nakubaliana na Tony Hseih aliyesema, “Huduma kwa wateja lisiwe dawati tu linalohudumia kwa wateja, bali kampuni nzima.”

Ukiwa umeajiriwa katika kampuni fulani hakikisha unatoa huduma ya viwango kwa wateja wenu, wakaribishe watu katika biashara ya kampuni yenu. Kuwa mzalendo pia wa kutumia bidhaa za kampuni yenu na jisikie huru kabisa unapozitumia.

Nimewahi kukutana na vijana wawili ambao walikuwa wakifanya kazi katika kampuni ya kuuza simu, lakini wao walikuwa wakitumia simu za kampuni nyingine. Swali lililokatiza kichwani kwangu ni hili, kama hawa wanatumia simu za kampuni nyingine, mimi nitaaminije simu za kampuni yao?

Binafsi, nimejiwekea utaratibu wa kutangaza kila Jumanne ya wiki katika mitandao yangu ya kijamii kwamba makala yangu itatoka katika Gazeti la JAMHURI. Najua wazi kuwa mimi pia ninao wajibu wa kutafuta wateja wa gazeti ninaloliandikia. Hilo ni jambo jema ambalo ukilifanya mahali pako pa kazi litazaa matunda mengi na bora. Jaribu sasa, utakuja kunishukuru siku zijazo. Biashara ni matangazo.

Sally Gronow anasema, “Huduma nzuri kwa wateja huwa na gharama ndogo kuliko huduma mbaya.”

Mteja siku zote ni mfalme. Daima kumbuka, “Unamtumikia mteja, sio kifungo cha maisha. Jifunze kufurahia kazi yako.” (Laurie Mclntosh).

By Jamhuri