NINA NDOTO (18)

Taa nyekundu na kijani za maisha

 

Zamani nilipokuwa nikisafiri na kupita katikati ya jiji palipokuwa na taa na kukuta taa nyekundu inawaka nilikasirika. Nilitamani muda wote taa ya kijani iwake ili tupite.

Siku hizi nikifika na kuona taa nyekundu inawaka nafurahi na kuona inaelezea hali halisi ya maisha.

Tupo katika zama ambazo kila mtu anataka kila kitu anachokifanya kifanikiwe mara moja. Anataka akianza kuimba, basi kila mtu amjue, kila mtu acheze wimbo wake, kila mtu asikilize wimbo wake, au akiandika kila mtu amkubali na kusema yeye ni mwandishi bora ambaye hawajawahi kumuona. Hawa ni watu wanaopenda taa za kijani muda wote.

Taa za kijani huonyesha ishara ya ruhusa kwa watu wanaotumia barabara fulani. Wakati taa nyekundu huonesha alama ya simama (STOP).

Kwenye safari ya mafanikio yoyote lazima utambue kuna taa nyekundu pia, hizi ni zile nyakati ambako unakumbana na changamoto, unashindwa, unakumbana na vigingi au mambo hayaendi kama ulivyotarajia.

Ukipenda taa za kijani lazima ukumbatie na taa nyekundu pia. Wanasema bahari shwari haitoi wanamaji hodari. Wajapani wanasema, anguka mara saba simama mara nane. Hawa ni watu waliojua kuwa barabara ya mafanikio si tambarare.

Ukiona mtu kafanikiwa jua kuna taa nyekundu alizipitia zilimwambia STOP ndiyo maana leo hii anatembelea taa ya kijani.

Siku hizi watu wanapenda mafanikio ya haraka maana watu wengi tunaowaona kwenye mitandao ya kijamii kuanzia huko Instagram, Whatsapp, Snapchat, Facebook na kadhalika; au kwenye ‘muvi’ na tamthilia za Kikorea tunawaona wamefanikiwa kwa urahisi kumbe nyuma yake kuna changamoto na misukosuko tusioiona.

Austin Kleon, mwandishi wa vitabu na mtunzi wa mashairi anasema, “Watu wengi wanapenda kuwa nomino na hawapendi kuwa vitenzi.”

Mwalimu wangu wa Kiswahili darasa la sita, Padre Kanuti Jumbe, alinifundisha kuwa; nomino ni neno linalotaja jina la mahali, mtu, kitu, hali au tendo.

Tena akanifundisha pia kuwa kitenzi ni neno ambalo huarifu tendo linalofanyika.

Watu wengi wanapenda kuitwa wanamuziki, lakini hawaimbi. Kuna watu wanapenda kuitwa waandishi, lakini hawaandiki. Kuna watu wanapenda kuitwa wapishi bora, lakini hawapiki. Kuna watu wanapenda kuitwa wabunifu, lakini hawajawahi kubuni chochote.

Unachokiandika kwenye bio (maneno ya utambulisho yanayowekwa kwenye kurasa za kijamii) zako za mitandao kiendane na kile unachokifanya. Hautudanganyi sisi, unajidanganya mwenyewe.

Usipende mafanikio ya haraka haraka. Si kila kitu utakachofanya kitaleta matokeo unayoyataka hapo hapo.

Kumbuka, vitu rahisi hufanywa na wengi, na vinavyofanywa na wengi havina thamani au huwa na thamani kidogo.

Yusufu pamoja na kuwa kiongozi wa juu sana, alipitia taa nyekundu, kuna wakati aliona foleni aliyokuwapo haisogei kabisa, aliuzwa na ndugu zake utumwani Misri, alifungwa gerezani ambako bila shaka alipitia shida nyingi, lakini mwishowe anakuja kuwa waziri mkuu.

“Ili kuwa mkuu, mtu lazima afanye kazi kubwa, na kufanya kazi kubwa ni jambo gumu.

Lazima iwe fokasi yetu ya kwanza,” anatukumbusha Ryan Holiday mwandishi wa vitabu.

Kubali kufanyia kazi wazo lako, kubali kupitia changamoto, mashujaa hupatikana kwa kufanya vitu ambavyo wengine wanashindwa kuvifanya.

Edward Sheeran, anayejulikana kwa jina maarufu kamaEd Sheeran ni mwanamuziki, mtunzi na mpiga gitaa, kabla ya kuwa maarufu alikuwa ni mtu asiye na makazi maalumu. Alipiga gitaa lake na kuimba katika mitaa ya Jiji la London. Alitumbuiza pia kwenye mabehewa ya treni. Hizo zilikuwa nyakati ambako taa nyekundu zilimwakia

Anasema, “Sikuwa na mahali pa kuishi kuanzia katikatiya mwaka 2008, mwaka 2009 wote na mwaka 2010. Nilijua wapi ningepata kitanda cha kulalia usiku fulani na nilijua ni nani naweza kumpigia muda wowote ili nipate baraza nilale. Kuwa mtu wa watu ilinisaidia.”

Ed Sheeran alikubali kupitia taa nyekundu ili afikie taa za kijani. Mtandao wa Digital trends unautaja wimbo wake unaoitwa“Shape of you” kama wimbo wa pili kutazamwa zaidi duniani katika mtandao wa Youtube ukiwa umetazamwa zaidi ya mara bilioni 4.5.

Ili kipepeo awe kama alivyo lazima awe kiwavi kwanza.Maisha yana taa nyekundu na za kijani. Kubali kupitia taa zote.