Lingekuwa tukio la ajabu kweli kweli endapo wabunge wetu wasingemshangilia Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, alipozuru bungeni.
Tena basi, ingekuwa ajabu mno kama wabunge wa kumshangilia wangekuwa wa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee! Kwa wale wanahabari wanaojua maana kweli ya habari, kumshangilia Rais Kikwete haikuwa habari! Kama wasingemshangilia, hiyo ingekuwa habari.
Tena basi, kinachovutia zaidi hapa ni kuona hata wale waliomkosoa wakati wa uongozi wake, na kufikia hatua ya kumwona kuwa ni kiongozi dhaifu, nao walisimama kumshangilia.
Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (wakati huo akiwa mbunge wa Ubungo), alifukuzwa bungeni mwaka 2012 kwa kusema: “Mimi nasikitishwa na jambo moja, tumefika hapa kutokana udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na wabunge na tumefika hapa kutokana na upuuzi wa CCM, nasema hivi nina ushahidi.”
Kabla ya kumpata Rais wa Awamu ya Tano, wana-CCM, wanachama wa vyama vya upinzani, wasomi na wananchi wa kada zote – waliomba wampate rais wa kuinyoosha nchi. Karibu wote walitumia maneno haya: “Tunahitaji kuwa na rais dikteta”.
Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, Mei 2015 alihojiwa na JAMHURI. Maneno yake ndiyo yaliyokuwa maneno ya Watanzania wengi walioukosoa uongozi uliokuwapo.
Alisema: “We need someone like a dictator person. Anayetafuta majibu kwa haraka. Hii ni kwa sababu mfumo wa sasa hauleti majibu stahili kwa wakati. Kwa sasa, Tanzania haihitaji Rais wa kutoa hotuba na badala yake ipate mtu mwenye kuamua na kukabiliana na matatizo kulingana na sasa.
“Sasa tuombe Mungu labda tutapata viongozi wenye zero tolerances ya ufisadi, rushwa na mambo mengi mengi. Hata kwenye utendaji wa Serikali mambo kwa sasa siyo mazuri hata kidogo. Mpaka ukiona rais naye analalamika ujue kwamba system is not delivering.  Kwa hiyo, anayekuja itabidi kweli alitikise hili.
“Wananchi sasa wanatafuta mtu ambaye anaonekana kuwa na mlengo wa kutoa utumishi, siyo kula. Maana kuna watu wanataka kwenda Ikulu ili aite rafiki zake, ili wagawane mali.
“Kusema waende pale wakawahudumie Watanzania wana shida zao. Watu wanatafuta mtu aina ya akina Julius Nyerere hivi. Ni mtu gani huyo? Ahangaike, atuhudumie sisi. Tuondokane na shida zetu na matatizo yetu.
“…Upate mtu ambaye akikaa mbele ya wasomi, anaweza kusema jambo. Kazi ya kukuza uchumi ni fundamental (muhimu) na kama tukikosa mtu huyo anayeweza kukuza uchumi haraka kwa kuelewa mifumo mbalimbali ya uchumi na kushirikisha njia mbalimbali…Watu wanatafuta watu wa namna hiyo. Msije kuweka mtu jambazi au fisadi. Hii nchi itapasuka. Inaweza kuwa kama Nigeria au Jamhuri ya Afika ya Kati au Zaire (DRC) wakati wa Mobutu Sese Seko.
“Tunataka tupate mtu mwenye mwelekeo wa ki-Nyerere Nyerere hivi. Mwadilifu, asiye na ubinafsi, asiye mlaji wa mali na umma, asiye mpendeleo hivi vyote.
“Tunahitaji regime yenye zero tolerance juu ya ufisadi na rushwa. Kwamba mtu yeyote anayeshughulika na rushwa asihurumiwe na Taifa hili.
“Kamata mara moja, ashughulikiwe mara moja kama anahukumiwa…ijulikane. Singapore wako makini katika hili. China wanapiga watu mpaka risasi akipatikana na hatia ya kula rushwa.
“Hapa kwetu tuna vitu vya ajabu sana hapa. Mtu anapatikana na rushwa, tena zilizo wazi badala ya kuchukua hatua, mnaanza kubishana.
“Hapa ilikuwa ifunguliwe hata mahakama ya kijeshi ya kushughulikia masuala haya ya rushwa. Unaweka majenerali hapo. Na kwamba kesi ikiletwa hata isichukue muda, jibu litoke.
“Mtu ana kesi ya kujibu au kutiwa hatiani anachukuliwa hatua na kama mtu hahusiki aachiwe. Hapo watu wanaweza kuwa na imani, lakini Mahakama zetu hizi za kubishana…Mnabaki mnabishanabishana tu. Mtu anaweza kuhangaikia haki yake miaka nenda rudi. Hakuna kinachofanyika. Sasa hivi shida iliyopo ni kwamba watu wanasema, matatizo yanajulikana, lakini matokeo hawayaoni. Hawaoni hatua dhidi ya wanaokula rushwa. Wanaokamatwa zaidi ni viongozi wa vijiji tu.
“Hawaoni watu wanakamatwa na dawa za kulevya na wanarudi mtaani tu. Watu wanasema wako matajiri hapa. Wanawajua, mnakaa kimya.
“Wakimbizi wanakamatwa Mbeya. Ama kweli hii nchi ya ajabu sana, yaani watu wanavuka Namanga na kukamatwa Mbeya. Wamevukaje hapo katikati? Mtu anapita nchini kwetu, bila kufahamika kweli?” Mwisho wa kunukuu.
Nimeyarejea maneno haya marefu ya mtu aliyepata kuwa kiongozi wa juu kabisa katika nchi yetu ili kuonesha wapi nchi yetu ilishafika. Tulikuwa kwenye hali mbaya.
Wabunge wanajua namna walivyokuwa wakifaidi fedha na rasilimali za nchi hii bila hofu. Kuna waziri mmoja alishawahi kuwaandalia ziara wajumbe wa kamati kwenda Afrika Kusini kama njia ya kuwapoza! Ukiacha fedha walizokuwa wakilipwa na Bunge, fedha nyingine – mamilioni kwa mamilioni – zilitolewa na taasisi au idara zilizo chini ya wizara husika. Huu ulikuwa wizi. Leo sayansi hiyo haipo. Je, tutarajie nini kutoka kwa wabunge ambao mrija huo umekatwa? Mwaka wa fedha ulipokaribia ukingoni, wizara au taasisi za umma zilizokuwa bado zina fedha, ziliandaliwa semina kwa wabunge. Kwa siku moja kuliweza kuandaliwa semina mbili au tatu au zaidi na wabunge wakalipwa mamilioni alimradi tu kuzikomba fedha hizo zisirejeshwe Hazina.
Wabunge kadhaa walijitungia ziara na vikao ili wajipatie fedha. Wakalipwa mamilioni na kufurahi katika hoteli ghali kwa kodi za wananchi. Watu wa aina hii kwa nini wasimlilie aliyewawezesha kuipata pepo hiyo?
Tunatambua namna wabunge na wakubwa wengine walivyojitungia safari za kwenda kutibiwa nje ilhali makabwela waliachwa wafie sakafuni Muhimbili. Hata maradhi yaliyoweza kutibiwa hapa nchini, wakaona yapelekwe India! Gharama zikabebwa na walipa kodi ambao hata ‘panadol’ hawakupata. Leo kwenda nje kutibiwa au kutembea kumedhibitiwa.
Kitu gani hasa kilikuwa kwenye ubunge kama si ulaji? Je, kuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kwamba wengi waligombea ubunge kama njia ya kutimiza kiu ya kuwawakilisha wananchi? Je, si kweli kuwa bungeni kulikuwa sehemu ya mavuno? Wangapi miongoni mwao leo wana hamu ya kuwania ubunge mwaka 2020? Mtu aliyetumia Sh milioni 200 kupata ubunge yeye alitarajia kuvuna ngapi?
Ukiacha haya, hivi ni kweli kuwa bindamu tu wasahaulifu kiasi cha kutoyakumbuka mengi mabovu ya Awamu ya Nne yaliyoiumiza nchi?
Sijui, lakini inawezekana wabunge walioimba “tunaku-miss” walikuwa wakikejeli. Walikuwa wakikejeli kwa sababu haiwezekani kiongozi mweledi ‘amisi’ madudu kama Escrow, Richmond/Dowans, EPA, mkataba mgodi wa Buzwagi, kashfa ya makontena, wizi wa madini, mishahara kwa watumishi hewa, safari za nje ya nchi, kushamiri kwa ujangili, dhuluma kwa makabwela, matumizi mabaya ya mali za umma; na nyingine nyingi.
Wabunge wetu wameshasahau hata namna walivyopigwa mabomu ya machozi na kuuawa kwa wafuasi kadhaa wa upinzani kama ilivyotokea Tarime, Morogoro na Iringa? Wamesahau UKAWA mwanzo wake ni msimamo wa Serikali iliyopita wa kuyazika maoni ya wananchi kupitia Tume ya Jaji Warioba? Tayari wamesahau mamilioni yaliyotafunwa bila kufanikisha upatikanaji Katiba?
Kwamba yoooote haya yamefutika akilini na sasa kuna watu wanatamani hata kubadili Katiba ili aliyeondoka arejee kuongoza?
Mheshimiwa Kikwete, pamoja na dosari kadhaa kwenye uongozi wake, anayo mazuri. Ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma ni mfano mmoja wa mazuri. Pamoja na ukweli huo, bado alifeli maeneo mengi. Aliiacha nchi ijiendeshe yenyewe. Aliacha kila mwananchi afanye walau alilopenda kulifanya. Ajali za barabarani; Ikulu iliishia kutoa rambirambi tu! Wanakufa watu 40 wanaliliwa kwa rambirambi. Madereva wa mabasi wakaota mapembe. Leo walau misiba hii imepungua. Utawala wa sheria maana yake ulikuwa kwa maskini na wasio na vyeo au ndugu serikalini. Sasa tunaona madereva wa magari ya Serikali nao wakikamatwa!
Rais John Magufuli si malaika. Ana makosa yake. Tumpe muda. Anahangaika kuijenga nchi iliyokwishapoteza mwelekeo. Anapambana na wezi na wafujaji. Anapambana na mfumo mbovu uliowekwa na mtangulizi wake. Miongoni mwa walioifaidi sana nchi ni wabunge ambao baadhi wanamkumbuka ‘starring’ wao leo.
Kiongozi aliyezuia safari zisizo na tija, aliyezuia posho mbili mbili, aliyeziba mianya yote ya ufujaji, hawezi kushangiliwa. Leo hatuoni mabasi yenye ‘wageni wa mbunge’. Hatuioni Dodoma iliyojaa wapambe wanaostarehe baa wakati mbunge akiwa bungeni. Zimebaki mbwembwe za halali. Hayo yalikuwa maisha ‘artificial’. Tunalalamika kwa sababu tumerejeshwa kwenye maisha halisi. Lingekuwa jambo la ajabu sana kama wabunge wangeshindwa kumshangilia mtu aliyewapa pepo hiyo.

955 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!