Nini maana ya utumishi wa umma?

Tukio la hivi karibuni limenisukuma kutafakari ni nini maana nzuri ya utumishi wa umma, na ni nini unapaswa kuwa uhusiano wa mtumishi wa umma na jamii yake.

Kwenye hoja yangu najumuisha watumishi wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa kwa sababu, aghalabu, cheo kinawainua na kuwapa hadhi na mamlaka yaliyo juu ya wapiga kura na walipa kodi. Wote hawa nitawaita watumishi wa umma, au viongozi.

Hivi karibuni nimeendesha gari kutoka Dar es Salaam hadi Butiama. Nilisimamisha gari kwenye mji mmoja katikati ya nchi kupata chakula, lakini niliporudi barabarani kuendelea na safari nilisimamishwa na polisi na kuarifiwa barabara imefungwa kupisha msafara wa kiongozi.

Mimi, pamoja na madereva wengine wengi, tulitii amri na kusubiri zaidi ya saa moja na tuliendelea baada ya msafara kupita.

Sifahamu alikuwa kiongozi yupi na wala si muhimu kufahamu kwa sababu mjadala si wa kiongozi mwenyewe ila wa utaratibu uliyopo juu ya uhusiano tulionao na watumishi wa umma.

Maana ya utumishi wa umma inaweza kuwa imepata tafsiri zaidi ya moja, kutegemea ni upande upi wa shoka umeshika. Ukishika mpini unaweza kusahau hali halisi ya upande wa pili.

Wakati mwingine utofauti huu ni suala la kisheria, lakini mara nyingi huwa ni uamuzi wa kiutendaji unaofanywa na watumishi katika ngazi mbalimbali za utumishi wa umma.

Miaka mingi iliyopita nilikuwa ofisini kwa afisa ardhi mwandamizi wa Jiji la Mwanza kwa shida ya kikazi na aliingia diwani wakati bado nasikilizwa. Yule afisa aliniomba nimpishe yule diwani ili ashughulikie suala lake kwanza. Nilipolalamika kwanini asimalize kwanza kunihudumia alinikumbusha kuwa yule ni diwani. Nilimpisha, nikijikumbusha kimya kimya kuwa sikuwa hata mjumbe wa nyumba kumi na nikifahamu fika kuwa ningezua zogo, basi uwezekano wa kutimiziwa shida yangu ungetoweka.

Ni mfano unaojirudia kila siku nchini unaotumika kupanga hadhi ya Mtanzania kwa kutumia uzito wa cheo chake. Huna cheo huna chako. Kwa yule afisa ardhi, diwani ni mtu muhimu kuliko mpiga kura wake.

Mtazamo wa aina hii unasahau kabisa ni nani mwajiri na nani mwajiriwa, ni nani mtumishi wa umma na ni nani aliyemuweka pale alipo – ama kwa kupigiwa kura, au kwa kuajriwa. Wasiobaini hii hitilafu watakuwa waathirika wa kurudiwa kosa kwa muda mrefu mpaka likazoeleka kuwa ni sawa.

Zipo sababu nzuri za kuharakisha huduma kwa mtumishi wa umma, na mamlaka zinazotambua hivyo huweka utaratibu ambao hauathiri sana huduma kwa mwananchi wa kawaida. Baadhi ya benki zinatoa huduma za upendeleo kwa baadhi ya wateja wake kwa kuwahudumia peke yao kwenye chumba maalumu chenye huduma ya chai, kahawa, vitumbua, na visheti.

Sababu moja muhimu ya upendeleo kwa viongozi ni usalama. Watanzania hatujasahau kwamba si zamani sana tulimpoteza Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine, kwenye ajali ya gari iliyosababishwa na gari lililoruhusiwa kutumia barabara wakati msafara wake unapita. Leo hii haihitaji utaalamu mkubwa wa somo la usalama kuona mantiki ya kufunga barabara mpaka msafara wa kiongozi upite, hasa ukizingatia muongezeko mkubwa wa magari na madereva wasioheshimu hata kidogo sheria za kutumia barabara.

Lakini ni muongezeko mkubwa huo huo ambao unaibua hoja ya athari kubwa na kwa watu wengi inayojitokeza kwa kufungwa, hata kwa muda mfupi tu, barabara kubwa kama inayounganisha Dar es Salaam na Mwanza.

Pamoja na ulazima wa tahadhari ya usalama, upo umuhimu wa kuangalia upya jinsi gani watumishi wa umma wanaweza kutumia huduma mbalimbali bila kuathiri sana wananchi wengine. Kuna kikomo cha uwezo wa kuwatengea mfumo maalumu watumishi hawa. Mathalani, hatuwezi kujenga barabara zao maalumu. Lakini kwenye matumizi ya barabara, badala ya kufungia wengine, inawezekana kutumia usafiri wa anga, kama helikopta, ili kuzingatia usalama wa kiongozi na kupunguza kero kwa wengine.

Sina hakika kama yupo mtumishi wa umma ambaye atafurahi kusikia kuwa kuna mgonjwa aliyekuwa akipelekwa hospitali akapoteza maisha akisubiri msafara upite. Wapo wagonjwa wengi wanaofikishwa kwenye huduma bila kutumia magari ya wagonjwa kwa hiyo upo uwezekano mgonjwa mahututi akakwamishwa kwa sababu yuko ndani ya gari la kawaida.

Njia nyingine ya kupunguza adha kwa wananchi ni kupunguza utitiri wa watumishi wa umma ambao wamepangiwa au wamejipangia upendeleo katika kupata huduma za umma. Si kila kiongozi atapanda ile helikopta. Hali kadhalika, si kila msafara uwe sababu ya kuwafungia watu barabara.

Kwa kawaida, haya matatizo hayaletwi na viongozi wenyewe, bali huletwa na watumishi wanaowazunguka ambao hudhani kuwa heshima ya kiongozi inaimarishwa kwa kadiri anavyotofautishwa na watu anaowatumikia.

Kimantiki kiongozi wa kuchaguliwa au wa kuteuliwa hawezi kuwa wa hadhi kubwa zaidi ya watu waliomuweka madarakani – wapiga kura na walipa kodi. Ila tunatambua tu kuwa yapo mazingira kama ya kiusalama ambayo yanalazimu kuwapo tofauti hiyo.

Watumishi wanaoweka utengano huo pasipo kuwepo sababu muhimu kama za kiusalama wanajisahau. Itakuwa kosa kubwa kwa viongozi nao kuingia kwenye mtego huo.

Maoni: [email protected]