NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, ameondolewa kwenye nafasi hiyo, JAMHURI limethibitishiwa.

Desemba 17, 2016 Bodi ya Wakurugenzi ya REA ilimteua Mhandisi Nyamo-Hanga, kushika wadhifa huo.

Pamoja naye, kumekuwapo mabadiliko ya baadhi ya wakurugenzi wa idara kadhaa REA; yote yakitajwa kuwa yamesababishwa na tuhuma za rushwa kwenye Awamu ya Tatu ya Mradi Kabamba wa Kusambaza Umeme Vijijini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya REA, nafasi ya Mkurugenzi Mkuu sasa inashikwa na Mhandisi Amos Masanja. Kabla ya uteuzi huo, Masanja alikuwa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Kanda ya Ziwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi REA, Dk. Gideon Kaunda, ameulizwa na JAMHURI kuhusu mabadiliko hayo, lakini amekataa kuingia kwenye undani wa suala hilo.

“Siwezi kuzungumza hayo mambo, tafuta mamlaka inayohusika,” amesema kwa mkato Dk. Kaunda ambaye Bodi yake ndiyo yenye mamkala hayo.

Kwenye matoleo kadhaa mwaka jana JAMHURI liliandika kwa kina ufisadi kwenye zabuni hizo. Toleo Na.295 kulikuwa na habari yenye kichwa cha habari, “Kampuni feki REA”; Toleo. Na. 296 “Kimenuka REA”; Toleo Na. 297 “Waghushi kuchota mabilioni REA”; na Toleo. Na. 312 “Rushwa yaifumua REA”.

Baada ya kuandika habari hizo, mamlaka mbalimbali za usalama ziliingilia kati kufanya uchunguzi.

“Tunaweza kukuhakikishia kuwa mabadiliko makubwa ndani ya REA yametokea baada ya mambo haya kuanza kuandikwa,” kimesema chanzo chetu.

Mabadiliko ya sasa yamefanywa baada ya kuwapo tuhuma nyingi za rushwa na upendeleo ndani ya REA hasa kwenye mradi Awamu ya Tatu ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, unaolenga kufikisha nishati hiyo katika vijiji 3,559 vilivyo kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara.

Thamani ya mradi huo ni karibu Sh trilioni moja ambazo asilimia zaidi ya 95 zinatolewa na walipakodi Watanzania.

Tuhuma za rushwa ndani ya chombo hicho zilimfanya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti REA, Prosper Msellem, ajiuzulu.

Msellem aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo Januari 13, mwaka jana; kwenye barua nyake ya kujiuzulu yenye kurasa saba, akiibua ufisadi uliofanywa na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya REA kwenye mchakato wa zabuni Mradi wa REA Awamu ya Tatu.

“Najiuzulu ili kutoa nafasi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuweza kufanya kazi zake za uchunguzi kwa uhuru,” alisema kwenye barua yake aliyomwandikia Injinia Nyamo-Hanga.

Pia aliigusa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, akisema ilishiriki kuweka shinikizo kwa baadhi ya mambo ambayo ni kinyume cha sheria.

Msellem alisema taratibu za ununuzi kwenye mradi huo ziligubikwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Ununuzi wa Umma, akisema bayana kuwa rushwa ilitamalaki.

Alisema Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya REA zilikuwa zikifanya kazi ya kutekeleza mchakato kwa shinikizo kubwa kutoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

“REB na Menejimenti zilikuwa zinafanya kazi kwa kupuuza Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013 na bila kuzingatia uwezo wa ndani wa REA kutekeleza kazi za ununuzi wa mradi huo wa REA Awamu ya Tatu,” alisema Msellem.

Hoja yake nyingine ni kuwa baada ya REB na Menejimenti ya REA kusaini mkataba wa makubaliano ya kutekeleza hatua za ununuzi, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kitengo cha Ununuzi (PMU) cha REA na Kamati za Uchambuzi pamoja na Bodi ya Zabuni REA zililazimishwa kufanyakazi katika mazingira magumu.

Msellem akasema kwamba kulikuwa na tofauti kubwa ya bei zilizopitishwa na Bodi ya Zabuni na bei zilizofikiwa baada ya makubaliano ya zabuni.

Akatoa mfano wa mtumishi mwandamizi wa REA alivyoomba rushwa kutoka kwa mmoja wa wazabuni kwenye Mradi wa Awamu ya Tatu.

Mengine aliyoyafichua kiongozi huyo ni kuwapo wa udanganyifu mkubwa wa makandarasi wenye madaraja yasiyokidhi vigezo, lakini walipewa kazi kinyume cha sheria. Anasema baadhi ya makandarasi, ama hawakuwa na vyeti stahiki, walighushi au kampuni hazikuwapo kabisa, lakini waliweza kupenyezwa hadi kwenye hatua ya kusudio la kupewa zabuni.

Sehemu nyingine iliyozungumzwa na Msellem, ni ile inayohusu malipo kutokana na viwango vilivyokadiliwa na makandarasi kwa kazi walizoomba, na kiwango kilichokubaliwa na Bodi.

Anatolea mfano hai wa ‘lot’ zilizo kwenye zabuni namba 9 ambako viwango vilivyoidhinishwa na Bodi vilikiukwa kwa namna ambayo ilishiria rushwa.

Mathalani, kwenye lot Na. 1 iliyohusu mradi wa umeme wilaya za Chato, Nyang’wale, Bukombe na Mbogwe mkoani Geita, kampuni ya Al-Hatimy Developers Limited, kiwango cha malipo kilichopitishwa na Bodi ya Zabuni REA kilikuwa Sh bilioni 56.981; lakini kilichokusudiwa kumlipa mzabuni huyo ni Sh bilioni 59.816. Hilo ni ongezeko la Sh bilioni 2.834.

Lot Na. 2 ilikuwa kwa kampuni za Radi Services Limited Ltd, Njarita Contractor Ltd na Agwila Contractor Ltd. Kampuni hizo za ubia zilipewa kazi katika wilaya za Nanyumbu, Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara mkoani Mtwara. Kiwango cha malipo kilichokubaliwa kwenye Bodi ni Sh bilioni 29.6; lakini kwenye malipo yakawa yameandaliwa malipo ya Sh bilioni 34.083; ikiwa ni ziada ya malipo ya Sh bilioni 4.483.

Kampuni ya Nakuroi Investment ilikuwa imepewa kazi katika wilaya za Kalambo, Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa. Kiwango cha malipo kilichoafikiwa na Bodi ni Sh bilioni 31.645 lakini kwenye malipo yaliyopangwa kufanywa kiango hicho kilikuwa Sh bilioni 34.662; kikiwa kimezidi kwa Sh bilioni 3.017 ya kile kichoidhinishwa na Bodi.

Kampuni ya Sengerema Engineering Group Ltd, Bodi iliidhinishia malipo ya Sh bilioni 22.238 lakini mwishowe kwenye hatua za malipo kiasi hicho kiliongezwa hadi Sh bilioi 27.031. Hilo ni ongezeko la Sh bilioni 4.792. Kampuni hiyo ilishinda zabuni ya kusambaza umeme katika wilaya za Kibaha, Bagamoyo, Mafia, Rufiji, Kisarawe na Mkuranga mkoani Pwani.

Pia, kampuni ya Steg International iliyokuwa imekubaliwa na Bodi ilipwe Sh bilioni 25.653; ikawa imeandaliwa malipo ya Sh bilioni 29. 916 ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 4.263.

Mhandisi Nyamo-Hanga, alimjibu Msellem kwa hisia kali akisema Mwenyekiti huyo wa Bodi alikuwa na nafasi kubwa ya kuusimamia mchakato wa ununuzi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu kwa kushirikiana na wajumbe wenzake wa Bodi ya Zabuni REA ili usiende vibaya.

“Na kama haya anayoyasema ni kweli maana yake ni kwamba alijua mambo hayaendi inavyotakiwa na bado akanyamaza akisubiri yaharibike zaidi na baada ya hapo yeye ajiuzulu.

“Kitendo hicho ni cha kinafiki na kinaonyesha ukosefu wa uzalendo na kinacholenga kulitia Taifa na wananchi wake hasara kubwa na ni kitendo kinachomkosesha sifa muhimu za kuwa kiongozi.

“Hata hivyo ukweli ni kwamba taratibu zote za manunuzi [ununuzi] zilifuatwa na muda wa kutosha ulitolewa kwa ‘evaluation committee’ na Bodi ya Zabuni kufanya maamuzi [uamuzi] yake kwenye hatua mbalimbali za mchakato wa ununuzi wa mradi wa REA Awamu ya Tatu ambayo ni kutaarifa ambayo Menejimenti ya REA iliwahi kuiwasilisha kwenye Bodi ya Nishati Vijijini kuhusiana na namna mchakato wa ununuzi wa mradi huu ulivyoendeshwa.

“Ndugu Msellem alikuwa sehemu ya wakurugenzi wa REA walioandaa na kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Bodi ya Nishati Vijini kwenye kikao chake cha dharura cha Aprili 27, 2017 kwenye Ukumbi wa Bodi wa REA na hakuonyesha wala kusema kama mchakato huo ulikuwa na dosari.

“Ndugu Prosper Msellem pia kama mjumbe wa ‘Senior Management ya REA’ muda wote alikuwa na nafasi ya kushauriana na wakurugenzi wenzake na hatimaye kumshauri Mkurugenzi Mkuu juu ya jambo lolote ambalo linaelekea kuleta madhara kwa taasisi yetu ikiwamo suala zima la mchakato wa ununuzi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu.

“Kutofanya hivyo hali akijua kuwa kuna matatizo kama alivyoandika kwenye taarifa yake ya kujiuzulu kunamfanya kukosa sifa za kukaa kwenye Senior Management ya REA kama Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti,” alisema Nyamo-Hanga.

By Jamhuri