Na Joe Beda Rupia

Sina hakika kama hili bado linafanyika, lakini zamani akina mama walikuwa wakiwabembeleza watoto wao kwa kuwaimbia nyimbo.

Kwa namna yoyote ile, nyimbo zilizokuwa zikitumika kuwabembeleza watoto ni lazima ziwe nzuri na za kuvutia. Nyimbo tamutamu!

Ni kutokana na hilo ndiyo maana Waswahili wakaja na msemo huu; nyimbo mbaya habembelezewi mwana.

Msemo huu unaweza kufananishwa kwa namna fulani na ule unaotumika mara kwa mara siku hizi, kwamba; mdomo huumba.

Sherehe za miaka 60 ya Uhuru zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, zilifana na kunoga kweli kweli. 

Shughuli ni watu, na siku hiyo watu walikuwapo! Tena wengi kweli. Maelfu walikuwapo uwanjani, mamilioni wakitazama na kushiriki kupitia runinga na redio. Tupo milioni 60 sasa.

Raha ya shughuli kama ile ni kuwapo kwa wageni. Nao walikuwapo. Tena wengi tu. Viongozi wa juu wa mataifa jirani au wawakilishi wao walikuwapo. 

Hivi utajisikiaje ukifanya sherehe huku majirani zako wakiendelea na shughuli zao kana kwamba haiwahusu? Kwa kuwa miaka 60 ya Uhuru inawahusu pia majirani, sherehe zilinoga zaidi kwa ujio wao.

Katikati ya sherehe akaibuka Masanja Mkandamizaji ambaye siku hizi anajiita mchungaji. Masanja akaandamana na mchekeshaji mwingine aliyemtambulisha kama Lucas Nyerere.

Wale watoto wa halaiki walisema ‘Taifa bila utamaduni ni taifa mfu’. Utani na vichekesho ni sehemu ya utamaduni wa Kiafrika. Kwa hiyo, haikuwa vibaya wachekeshaji hawa kushiriki kwenye shughuli ile.

Wengi tunamfahamu Masanja. Tunaheshimu kipaji chake. Ni mchekeshaji haswa, hilo kila mmoja analifahamu. Lakini kwa kweli Siku ya Uhuru, hakukitendea haki kipaji chake, hakututendea haki Watanzania, wala hakuwatendea haki wageni wetu.

Masanja anasema kwa miaka 60 Tanzania tumekuwa tukinunua vifaru na vifaa vya kivita lakini havitumiki, sasa anataka ‘tuombe shoo’ na Rwanda ili ‘tutesti mitambo’

Kuomba shoo ni lugha ya mtaani. Masanja anataka tukajaribu mitambo na Rwanda? Kweli! Hata kama ni utani, pale hapakuwa mahala pake!

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alikuwapo uwanjani kama mgeni wetu. Alisikia maneno yale. Je, yalimfurahisha? Kwa nini kutesti mitambo na taifa lake? Ni dharau au? Kwa nini isiwe na Kenya? Kwa nini isiwe na taifa jingine ila Rwanda?

Maneno haya yakizungumzwa kijiweni si tatizo, lakini siku rasmi kama Desemba 9! Hapana. Haikuwa sahihi na kwa kweli Masanja atuombe radhi kwa kutia doa sherehe zetu.

Vita si lelemama. Vita si suala la masihara. Hata wanajeshi wenyewe hawapendi vita. Huu ni wimbo mbaya, hauwezi kulelea mwana. Maneno haya, Mungu apishe mbali yasije yakaumba.

Kana kwamba haitoshi, Masanja akamkaribisha ‘Nyerere wake’. Naye akazidi kutuharibia sherehe kwa utani wa kitoto siku kubwa kama Desemba 9.

Anaiga sauti ya Baba wa Taifa (Mungu amrehemu) kwa kuingiza utani ambao hauendani na siku yenyewe. Anawataja Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kama vijana wenzake eti kwa sababu tu anaiga sauti ya Mwalimu! Hii haikubaliki.

Utani ni sehemu ya utamaduni wetu, lakini uendane na mazingira. Hapa kuna makosa yalifanyika na lazima tukubaliane kama taifa lenye utamaduni wa kuheshimiana.

Waandaaji wa sherehe walipaswa kuyafahamu maudhui yatakayotolewa na wachekeshaji hawa na kuyachuja. Kama hayana maana, wasiruhusiwe kushiriki, kwani lazima? Kwa nini kuwalipa upuuzi tu?

Masanja ana kipaji kama nilivyosema awali. Iwapo angeelekezwa na waandaaji nini cha kufanya, kwa hakika asingeteleza kwa kiwango cha kutishia kumvunjia heshima.

Kwa nini yeye na mchekeshaji mwenzake wasiigize namna Mwalimu Nyerere alivyokuwa au alivyozungumza Desemba 9, 1961?

0679 336 491

By Jamhuri