Katika mikakati ya kuinua uchumi wa nchi na mikakati ya uanzishaji wa viwanda, Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu imetoa mafunzo kwa vijana 9,120 katika fani mbalimbali na kukuza ujuzi.
Fani hizo ni stadi za kushona nguo kupitia viwanda vya TOOKU na MAZAVA vijana 3,000, stadi za kutengeneza bidhaa za ngozi vijana 1,000 walinufaika kupitia taasisi ya DIT, urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa vijana 4,050 kupitia VETA.

Mafunzo mengine ni uanagenzi katika sekta ya utalii na hoteli kwa vijana 250 kupitia VETA na mafunzo ya stadi za ushonaji nguo, ufundi bomba, useremala, uchomeleaji, utengenezaji wa vipuri vya mitambo, na ufundi wa kompyuta kwa vijana 820 kupitia taasisi ya Don Bosco.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema katika eneo la Usimamizi na Kuratibu usajili wa vyama vya wafanyakazi na Waajiri jumla ya maombi saba ya kusajili vyama vya wafanyakazi yamepokelewa na yanaendelea kushughulikiwa.

Amesema maombi sita yametoka kwa wafanyakazi na katika usimamizi wa vyama vya wafanyakazi jumla ya migogoro minane iliyohusu vyama vya wafanyakazi kunyang’anyana wanachama katika baadhi ya maeneo na kutoridhishwa na taratibu za uchaguzi mkuu ilishughulikiwa kwa njia ya maridhiano ‘dialogue’ na kukamilishwa na jumla ya kesi mbili zinaendelea kushughulikiwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Pamoja na hayo amesema chama cha ‘Tanzania Agro Forestry Workers (TAWU)’ kimefutwa kwa amri ya Mahakama kwa kukiuka Katiba yake na Sheria na kufanya idadi ya vyama vilivyofutwa kwa kukiuka masharti ya usajili kufikia vinne.
Katika kusimamia na kuratibu maendeleo ya vijana, Wizara hiyo iliratibu mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2016 na kuhimiza shughuli za maendeleo ambako jumla ya miradi 1,387 yenye thamani ya sh 498,892,879,808 iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa.

Pia iliratibu maonesho ya Wiki ya Vijana kuonesha shughuli za kiuchumi. Maonesho hayo yalifanyika mjini Bariadi ambako taasisi 162 zilishiriki na kati ya taasisi hizo 109 zilikuwa za vijana.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imewawezesha kiuchumi Vijana 284 kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu inayofikia sh 1,630,796,520.
Katika Kusimamia na Kuratibu Huduma za Wenye Ulemavu, mafunzo ya stadi za kazi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu 124 wanaume 34 na wanawake 28 yalitolewa katika vyuo vya Yombo jijini Dar es Salaam na Chuo cha Wasioona cha mkoani Singida.
Hata hivyo utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye ulemavu Na.9 ya Mwaka 2010 ilizingatiwa na Baraza la Watu Wenye Ulemavu liliwezeshwa ili kufanya kazi zake na kuratibu uundwaji wa Kamati za Watu Wenye Ulemavu katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata, Mitaa na Vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na.9 Kifungu cha 14(1).

Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu pia ilisimamia taasisi ambazo ziliendelea kutekeleza majukumu mbalimbali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambako jumla ya sehemu za kazi 2,101 zilisajiliwa sawa na asilimia 90 ya lengo la kusajili sehemu 2,335 kwa kipindi cha Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu.
Jumla ya sehemu za kazi 288 zilipewa leseni za kukidhi viwango vya usalama na afya kwa mujibu wa sheria ya Usalama na Afya Mahali pa kazi na kufanya kaguzi 6,294 za kawaida (General Workplace Inspection) ambazo ni sawa na asilimia 47.2 ikilinganishwa na kaguzi 13,335 zilizopangwa kufanyika.

Kaguzi maalumu 58,272 (Specific Workplace Inspection) zilifanyika zikiwamo za umeme, mitungi ya gesi na hewa, zana za kunyanyulia vitu vizito na vipimo vya mazingira ambazo ni sawa na asilimia 137 ikilinganishwa na kaguzi 42,529 zilizopangwa kufanyika.
Pia Wakala uliwachukulia hatua za kisheria waajira ambao hawakufuata Sheria na Kanuni za Usalama na Afya Mahali pa Kazi huku waajiri 534 wakipewa ‘Improvement Notices’, Waajiri 90 walitozwa faini za papo kwa hapo, wengine 76 walifungiwa maeneo yao ya kazi na mmoja alifikishwa mahakamani.
Kupitia Taasisi ya Huduma za Ajira Tanzania (TaESA), Mhagama amesema jumla ya watafuta kazi 303 waliunganishwa na waajiri wenye fursa za ajira hapa nchini na watafuta kazi 762 waliunganishwa na waajiri nje ya nchi katika nchi za Oman, Dubai na Qatar.
Hata hivyo kupitia kwa Taasisi hiyo, ushauri ulitolewa kwa watafuta kazi 667 juu ya uchaguzi wa fani, mafunzo ya kazi wanazostahili kulingana na sifa zao ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika (Vocational Guidance na Counseling).
Kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii yaliyotekelezwa ni jumla ya kaguzi 30 za mifuko ya hifadhi ya jamii zilifanyika ambako kati hizo, kaguzi nne ni ‘on-site supervision’ katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya GEPF, LAPF, PPF na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Ukaguzi huu ulilenga katika kuhakikisha kuwa mifuko husika inafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na kaguzi zilizobaki zilifanywa kwa njia ya TEHAMA (Off-site inspections) kwa mifuko sita ambayo ni GEPF, LAPF, NSSF, PSPF, PPF na NHIF na vilevile Mamlaka ilifanya kaguzi kwa Mameneja Uwekezaji (Fund Managers) 17 na Wahifadhi 6.
Pamoja na hayo amesema Mifuko ya Hiari (Supplementary Schemes) mitatu ya LAPF DC, Mfuko wa Wafanyakazi wa SUMATRA na Mfuko wa Wafanyakazi wa PPF imesajiliwa ili kupanua wigo wa hifadhi ya jamii na pia Mifuko ya Afya ya Jamii (CHF) 12 nayo imesajiliwa.

Lengo ni kupunguza gharama za miongozo yenye lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii – Social Security Schemes (Administrative Expenses) Guidelines ya 2016 ili kuiwekea Mifuko utaratibu wa kuhakikisha wakati wote inakuwa na ukwasi wa kutosha wa kulipa mafao wanachama.
Akizungumzia Elimu kwa Umma kuhusu Sekta ya Hifadhi ya Jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama magazeti mara 148, redio mara 63, televisheni mara 49 na maonesho 6 amesema iliendelea kutolewa ambako SSRA imeandaa na kushiriki katika jumla ya semina 22 za kuelimisha makundi maalumu ya wadau kama wafanyakazi wapya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wahariri wa Vyombo vya habari, Umoja wa Wabangua Korosho, Vyama vya Wafanyakazi na pia kutoa elimu kwa Viongozi wa Vijiji na Mitaa 1,380 katika Halmashauri 15 nchini.

Kupitia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), yaliyotekelezwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato yanayofikia Sh. milioni 533,821.01 sawa na asilimia 67.3 ya lengo kutoka katika vyanzo mbalimbali na kutumika katika kulipa mafao ya wanachama, kuwekeza katika vitega uchumi, gharama za uendeshaji na miradi ya maendeleo, utoaji wa elimu kwa wanachama, waajiri na umma kwa ujumla ili waweze kuelewa vizuri mfumo mpya wa hifadhi ya jamii na jumla ya semina 8,591 zimetolewa kwa waajiri na wajasiliamali katika sekta isiyo rasmi.

Watu 29,959 walihudhuria semina hizo na watu 62,733 waliandikishwa kuwa wanachama wapya wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambayo ni sawa na asilimia 43.87; kuanza ujenzi wa barabara ya njia sita kilomita 1.2 kutoka Daraja la Kigamboni, kuelekea Kigamboni Kibada. Kuendelea na ujenzi wa nyumba 439 katika eneo la Dungu “Farm” na nyumba 131 eneo la Tuangoma. Kuendelea na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zipatazo 300 mkoani Dodoma, ujenzi huu uko katika hatua ya upembuzi yakinifu.
Amesema katika kuitikia wito wa Serikali wa ujenzi wa viwanda, Shirika hilo limetoa mikopo yenye tija pamoja na kushiriki kwenye ujenzi wa viwanda. Viwanda hivyo ni pamoja na Kiwanda cha Viuadudu Kibaha, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ya Shirika la Usagaji la Taifa, Kiwanda cha Matairi (General Tyre) Arusha na ujenzi wa kiwanda cha sukari katika Mkoani Morogoro.
Pia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kutekeleza majukumu yake umefanya kazi mbalimbali ikiwamo kupokea madai ya malipo ya fidia 37 na kati ya madai hayo umelipa madai 20 yenye jumla ya sh. milioni 400, madai matatu yamefungwa kwa kutokuwa na vigezo vya kulipwa.

Madai 14 yalikuwa hayajakamilika kwa sababu ya kukosa viambatisho na kurudishwa kwa waajiri ili kukamilisha vielelezo. Mfuko huo pia umekusanya michango inayofikia sh. bilioni 37.41 kutoka kwa waajiri 6,448 na kuwekeza michango katika amana za benki kiasi cha sh bilioni 6.68 na sh. bilioni 34.87 katika Hati Fungani za Serikali.
Mhagama katika taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2016/2017 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/2018 kwa mafungu.
Katika mpango wa maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitengewa jumla ya Sh 159,174,011,629 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hadi Februari 28 mwaka huu jumla ya sh 70,484,634,036 ikiwa ni asilimia 44 ya bajeti zilikuwa zimepokelewa.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake imetengewa jumla ya sh 83,565,372,763 kwa ajili Mpango wa Maendeleo na kati ya fedha hizo sh 22,000,000,000 ni fedha za ndani na sh 61,565,372,763 ni fedha za nje

By Jamhuri