Ole wenu mnaokaa kimya!

Mwanzo nilidhani tunaopinga usaliti wa
wanasiasa wanaojiuzulu udiwani na ubunge
na kwenda vyama vingine, tu wachache.
Sikuwa sahihi.
Baada ya kuliandika suala hili kwa mara ya
tatu wiki iliyopita, nimepata mrejesho
mkubwa. Wapo Watanzania wa kutosha
wanaopinga hiki kinachoendelea.
Vyama vya siasa vilivyo nje ya ulingo wa
madaraka ni kama kioo. CCM itakuwa
ikifanya jambo la maana sana endapo
itaendelea kuvitumia vioo hivi ili iweze
kujitazama na kuona wapi panapostahili
kurekebishwa.
Chama cha siasa kinaposema mahali fulani
kuna ufisadi, kwa kauli hiyo kinakisaidia
chama kilicho madarakani kuelekeza nguvu
hapo panaposemwa. Ashakum si matusi,
naomba nitoe mfano ambao si mzuri sana,
lakini una maana njema. Mniruhusu niseme,
chama cha upinzani ni kama mbwa
anayefugwa. Mbwa anapobweka anasaidia
kuwasilisha taarifa au hatari inayomsogelea
anayemlinda. Tajiri anayemchukia mbwa wa

aina hiyo anafanya makosa. Huu ni mfano
tu. Simaanishi kuwa wapinzani ni mbwa, la
hasha!
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza
uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani.
Kama misukule, tunatakiwa tujaze nafasi
tatu kwa majimbo yaliyo wazi. Majimbo
hayo ni Korogwe Vijijini, Monduli na
Ukonga. Uchaguzi wa haki ni wa Korogwe
Vijijini, maana unafanyika kuziba nafasi
iliyosababishwa na tukio la asili – kifo.
Uchaguzi wa Ukonga na ule wa Monduli, ni
uchaguzi wenye sifa zote za kuitwa
uchaguzi batili. Tunateketeza mabilioni kwa
sababu watu wawili wameamua iwe hivyo.
Kwenye mijadala ya watetezi wa dhambi hii
wapo wanaojitahidi kwa nguvu zote
kuaminisha umma kuwa wanaohama,
wanahama kwa sababu ndani ya Chadema
kuna matatizo ya uongozi.
Wanamzungumzia Freeman Mbowe kama
chanzo cha kudorora kwa chama hicho.
Wanazungumza kuhusu upendeleo,
udikteta, ukabila na ukanda ndani ya chama
hicho. Kuna viji-sababu vingi vinavyotolewa.
Haya ndiyo matokeo ya kuvamia chama au
kufuata mkumbo badala ya kufuata itikadi.
Ukiwasikiliza ndugu zangu Kalanga na

Waitara sababu wanazotoa huwezi
kushawishika kwamba ndizo zinazowafanya
‘waususe’ mshahara wa karibu Sh milioni
12 kwa mwezi, posho zote za vikao ndani
na nje ya Bunge na kiinua mgongo
kinachoanzia Sh milioni 200.
Ndugu zangu, kwa hali ya uchumi ya mtu
kama Waitara kuachia Sh milioni 200 kwa
sababu tu nyepesi za ‘udikteta’ wa Mbowe,
ni jambo gumu kuliafiki. Hawa kuna dalili
zote kuwa wameshapokea mafao yao!
Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph
Warioba, alipata kusema kitendo cha
‘wageni’ kupewa nyadhifa haraka haraka
pindi wanapojiunga CCM kunawavunja
moyo baadhi ya makada. Wahamiaji
waliposikia kauli hiyo wakaona wamjibu Jaji
Warioba. Wakatumia hoja dhaifu kwamba
wao wanapewa madaraka kutokana na
mazingira ya sasa ya kisiasa nchini.
Kwa kuwa walikuwa katika kambi ya
upinzani, wanasema wao ndio wanaoujua
upinzani na wapinzani. Wanasema hoja zao
zitaiimarisha CCM. Wanajiona kuwa ni
silaha makini katika vita ya kuudhoofisha na
kuutokomeza upinzani.
Chama Cha Mapinduzi kiliitwa chama cha
mapinduzi si kwa bahati mbaya. Kiliitwa

hivyo kutokana na historia ya kuundwa
kwake na malengo yaliyosimama katika
misingi ya aina ya taifa lililokusudiwa
kujengwa. Kuna kundi kubwa la makada
ndani ya CCM walioamua kuvumilia hali na
misukosuko yote ya kisiasa. Hawa ni wafia
chama kama walivyo wafia dini.
Watu waliokitumikia chama kwa miaka
mingi, wakiongozwa na uadilifu na utii wa
hali ya juu, leo wanaonekana si lolote, si
chochote. Wahamiaji waliokuwa
wakikitukana chama, hata kikaonekana
hakifai, leo wanajidai kuwa wamebadilika na
sasa wanatumiwa na viongozi wetu eti
kufanya kazi za uenezi na propaganda za
kukipa chama ushindi.
Mtu aliyesimama jukwaani, akaanza
kukitukana chama tawala kwa nguvu zote,
akakosoa siasa ya chama, sera za chama,
ilani ya chama, leo hii mtu huyo atakuwa
ameshukiwa na malaika gani wa kumfanya
awe muumini mzuri wa chama
alichokitukana?
Leo kila mtu anajua kwamba ukitaka
mambo yakunyookee jiunge CCM. Kama
uliitukana CCM, tubu, na ukirejea
utapokewa na utapewa uongozi. Tunaweza
tusiwe na ujasiri wa kuyasema haya leo,

lakini huko tuendako yatasemwa tu.
Siasa hizi nyepesi, za kupokea watu wa kila
aina, ndizo zinazokifikisha chama katika
namna ya kuonekana yeyote anaweza
kukitukana na mwishowe akapewa
madaraka. Hizi siasa ndizo zimeifanya CCM
ionekane ni chama ambacho anayetaka
kufanikiwa sharti akihame, akitukane,
ajiunge nacho kisha apewe madaraka.
Sioni ni kitu gani kitawazuia Waitara,
Kalanga na wengine ambao wako kwenye
foleni ya kurejea CCM kutopitishwa kuwania
tena ubunge. Nimejitahidi kuuliza wajuzi wa
siasa kama wameshawahi kushuhudia au
kusoma kwingineko duniani hiki
kinachoendelea sasa nchini mwetu,
sikupewa mfano wa aina yetu.
Hapa ieleweke vema kuwa tunachopinga si
kuhama vyama, bali tunapinga mtu
aliyechaguliwa kwa fedha za umma, kusaliti
wapiga kura na kurejea kutaka achaguliwe
tena. Matumizi haya haramu ya fedha za
umma kwa kigezo cha demokrasia ndiyo
tunayopinga. Hatupingi mtu kuhama.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
alipata kusema kuwa CCM ilikuwa
imebadilika na kuwa kama dodoki. Kama
angekuwa hai leo, Mwalimu angesema

CCM imeongeza sifa. Si dodoki tena, ni
kokoro. Swali la kujiuliza, ni je, wote
wanaorejea kweli wana nia njema?
Watu hawa wana umalaika gani? Wanataka
kujilinganisha na Paulo katika Injili – yule
aliyewaua wafuasi wa Yesu? Je, hawa nao
wameshukiwa na maono gani, kiasi cha
kuwa watu wa kutumainiwa kuwa washauri
wa moja ya vyama vikubwa kabisa barani
Afrika?
CCM imefanywa kuwa ni chama-ngazi.
Yeyote anayetaka kunyookewa mambo
yake anaona hana sababu ya kuhangaika.
Kama haya yote yanajitokeza, kuna sababu
gani ya kuwa na kadi za uanachama? Leo
tunawashuhudia watu wakijiunga CCM huku
wakiwa wapinzani wakuu, walioitukana
CCM na kuidhalilisha mbele ya umma.
Wengine waliongopa kwamba CCM imeleta
umaskini nchini. Wengine walisema CCM ni
mafisadi. Hawa wote leo ni viongozi ndani
ya CCM. Wale makabwela waliohangaika
na chama – waliopigwa jua na mvua,
waliovumilia matusi ya kila aina, wanabaki
kuwa watazamaji.
Mwalimu Nyerere, kwenye kitabu chake cha
Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania,
anasema maneno haya kuhusu

ukigeugeu: “…Wewe huyo huyo huwezi
kushindwa kuutetea ushauri wako wa awali,
halafu umshauri rais akubali ushauri ulio
kinyume cha ule wa kwanza, na utazamiwe
kuwa huo sasa utautetea. Utakuwa Saulo
aliyeona mwangaza akageuka kuwa Paulo!
Lakini hata yeye wale aliokuwa akiwatesa
awali waliendelea kuwa na mashaka naye
kwa muda mrefu sana, mpaka akasaidiwa
kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu. Katika
siasa hatuwezi kutegemea miujiza hiyo.
Lazima tuhukumu kwa kutumia akili zetu za
kawaida.”
Wale wanaobaki CCM kwa uadilifu, si ajabu
wakawa wanafanya tafakuri. Wataamua
kukihama chama, watajiunga upinzani.
Watatukana kwa nguvu zao zote.
Wakishajiridhisha kwamba wametukana
hadi waliotukanwa wamesikia, watarejea
CCM kupata uongozi.
Huko watapokewa kwa mbwembwe.
Wataandaliwa mapokezi mazito. Redio na
televisheni zitatangaza. Hawa ndio
wanaotarajiwa wawe makada na wapiga
propaganda majukwaani. Hawa eti ndio
wanaokidhi siasa za sasa. Huku ni
kujidanganya. Huku ni kukidhoofisha
chama. Chama hakiwezi kustawi kwa njia
hii, maana huwezi kujua nani wamerejea

kwa nia ya dhati, na nani wamerejea kwa
sababu ya masilahi binafsi.
Namwelewa sana Mwenyekiti wa CCM
anaposema maendeleo hayana vyama. Hii
ni kauli nzuri. Inalenga kuwafanya
Watanzania wajione wamoja linapokuja
suala la ujenzi wa nchi. Hata hivyo, ujenzi
wa nchi si lazima kuwa ndani ya chama
kimoja. Tunaona Kenya namna Raia
Odinga na Rais Uhuru Kenyatta
wanavyofanya mambo. Mbona Raila
hajasema hawezi kumsaidia Rais Kenyatta
bila kuwa kwenye chama cha rais huyo?
Msuguano wa mawazo, hasa yanayolenga
kulipeleka taifa mbele ni jambo jema. Watu
hatari ni wale wanaoligawa taifa, lakini
wanaosema kwa namna ya kuboresha
mambo, wanaokosoa, hao ni watu muhimu.
Wanaokejeli au kubeza mafanikio ndio watu
hatari.
Kunguru hafugiki. Ni vigumu sana kumfuga
kunguru. Hawa wanaoonekana leo wapenzi
na watetezi wa CCM, ndio hao hao
watakaokuwa watoboa siri za chama. Hawa
watakiua chama. Lazima wenye CCM
wajiulize, haya mahaba ya ghafla
yanasababishwa na nini? Yanalenga kupata
nini ambacho wamekikosa huko waliko?

Jambo kama hili la kutumia fedha za umma
kuendesha uchaguzi wa marudio wenye
kukidhi tamaa za watu binafsi, sharti
likemewe. Nayasema haya kama Mwana
CCM mtiifu ninayeamini katika ile ahadi ya
“Nitasema kweli daima, fitina kwangu
mwiko.” Mwalimu Nyerere
anasema: “Vyama makini huundwa kwa
sababu na shabaha makini. Umoja wa
chama ni umoja wa shabaha, si umoja wa
nasaba. Ni mbinu au nyenzo ya kufikia
shabaha fulani. Tukitelekeza shabaha
yenyewe iliyotufanya tukaunda umoja ili
tuitekeleze, umoja au mshikamano mtupu
utakuwa hauna maana.”
Huko tuendako CCM inaweza kuwa kwenye
hali mbaya kwa sababu itakuwa ni kundi la
watu wenye shabaha na matamanio tofauti.
Hawa wanaorejea CCM kwa kutoa hoja
nyepesi, ambao wengi wao waliisaliti na
kuikimbia, ni kitu gani kitawazuia kuurejea
usaliti? Je, waachwe wasipokewe? Hapana,
wapokewe, lakini muhimu ni kuwa na
hadhari nao maana yaelekea
kinachowarejesha CCM si itikadi na
shabaha ya kuundwa kwa CCM, bali ni
masilahi binafsi. Ndiyo maana tunasikia
wakisema: “Narejea kwa sababu
nafurahishwa na utendaji kazi wa Rais John

731 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons