Paulo Sozigwa hakustahili kutendewa namna ile (2)

Mzee Sozigwa alikwisha-tekeleza alichoambiwa. Ilikuwa wajibu wa ofisa wa Ikulu kumshughulikia ipasavyo. Kama kweli wahusika wamezi-misplace zile nyaraka humo humo ofisini mwao, basi wao wawajibishwe lakini siyo mzee wa watu alaumiwe na kudaiwa apelike nyaraka hizo.

Waingereza wanaita hali hiyo ‘gross negligence’ by Ikulu Officers. Mzee Sozigwa angetoa wapi nyaraka nyingine? Si kumsulubisha mzee bila sababu za msingi?

Ndiyo maana wazee tunaona tunadhalilishwa na hii tabia ya ofisi za Serikali kutokujali inayoitwa ‘Leisure taire’. Hii inatia doa sifa za utawala bora katika Serikali.

Sasa mimi nimesaidia kuthibitisha data hiyo katika kitabu cha UTUMISHI data kamili mnayo. Sasa mlipeni basi kwa uzito wa data hizo maana ni ‘anthentic’ kwa maana ya kutolewa na ofisi kuu ya utumishi serikalini.

Mzee Sozigwa hakustahili kusumbuliwa na mwajiri wake. Utumishi kuna Establishment Officer kaweka wazi status ya mtumishi tena ni Principal Secretary, ameapishwa na Rais wa Jamhuri kutunza siri za Serikali. Leo kumdai eti alete nyaraka husika ni documents gani zaidi ya zile alizokwisha kukabidhi ofisini Ikulu? Isitoshe rekodi za utumishi ndiyo hizo.

Naomba maafisa vijana wasipende kudhalilisha wazee, bali wawasaidie wapate haki zao mara tu wanapostaafu. Hata kama Mzee Sozigwa alipelekwa Ikulu au kwenye chama tawala, tarehe yake ya 1stappointment inabaki ile ile, salary grade hizi fixed zinabaki vilevile sielewi yule ofisa aliposema, namnukuu tena “…alikuwa mfanyakazi ofisi binafsi ya Rais hiyo pekee haikuwatosha kumfanya kuwa mtumishi wa Ikulu, kwa sababu hakuna nyaraka zake ambazo zingeweza kutumiwa na Hazina kumlipa mafao” soma hayo toka (JAMHURI Toleo Na. 294 la tarehe 16 – 22 Mei 2017 uk. 17 ibara ya 4 aya ile ya kwanza kutoka chini. Hebu jamani tuelimishane. Kuna ikama ya watumishi wa Ikulu? Staff List inaorodhesha toka jina la Mwalimu Julius K. Nyerere mpaka karani katika kila idara. Hakuna neno mtumishi wa Ikulu as such.

Hapa natoa uthibitisho wa kiserikali kuwa Mzee Sozigwa alikuwa mtumishi wa Ikulu. Katika STAFF LIST (CONFIDENTIAL) ya Januari 1972 namna hii:

PRESIDENT’S OFFICE

STATE HOUSE AND CABINET SECRETARIAT uk. 5

Jina la kwanza na majina yanayofuata yanasomeka hivi nanukuu:-

1.  Mwalimu JK Nyerere MA, LLD (Ediub). PRESIDENT

Date of Birth : 1922

Date of 1st Appt. : 09.12.1962

Present Station : DSM

Salary  : ……….

2. Jina la pili ni la Sheikh A. A. Karume

3. Jina la tatu ni la A. Jumbe

Present Station zao Zanzibar

4.  Jina la nne ni Sheikh A. H. Mwinyi(Minister)

Present Station zao Dar es Salaam

5.  D.A Nkembo

Principal Secretary

Present Station ni DAR

6. Jina la 6 ni P. A Sozigwa (BA Lond)

Date of Birth : 23.02.1933

Date of 1st Appointment :  15.04.1964

Present Post  : PRESS SECRETARY
Present Station : Dar es Salaam

Basic Salary : 46,800 sh. p.a

Appt. to present Post : 27.09.1967

Baada ya jina la Paulo Sozigwa yanafuata majina ya Private Secretary J. W Butiku na Personal Secretaries majina ya (a) I. M. Bhoke Mnanka (b) A. K. Tibandebage na majina ya watumishi wengine kama yanavyosomeka katika Staff List ile nakala ya 1972 nimeambatanisha hapa kwa uthibitisho. Mzee Sozigwa hakufanya kazi katika ofisi binafsi ya Nyerere, bali alikuwa mwajiriwa wa Serikali Kuu.

Angalizo: Katika Staff List kuna herufi P kuonesha status kiajira ni confirmed in pensionable appointment. Mimi kwa ufahamu wangu Katibu Mkuu wa kwanza Ikulu alikuwa Administrative Officer Dunstan Omari tu.Wengine wote waliokuwa Ikulu walichomolewa na rais kutoka wizara mbalimbali. Mzee Joseph Namata alitokea Ualimu Chidya, Dixon Nkembo alitokea Ushirika Masasi, Timothy Apiyo alitokea Kilimo Pamba House, Lumbanga alitokea Maliasili, Dar Luhanjo katokea Mambo ya Nje, Sefue katokea Mambo ya Nje na huyu wa sasa Mhandisi Kijazi katokea ubalozini India.

Hivyo hao wote wana status za Katibu Mkuu; iweje Sozigwa, Katibu Mkuu toka mwaka 1964 leo mtu ambague eti hakuwa mfanyakazi wa Ikulu? Katibu Mkuu ni Presidential Appointment na mtu anatoka na mshahara wake staff grade fixed. Sisi tunaelewa utawala wa nchi hii. Hapa Ikulu wanawajibika kumtengenezea mafao yake Mzee Sozigwa hata kama amefariki dunia.

Labda nitoe mfano hai wa namna mafao ya mtu kama haki yake hayawezi kupotea. Mzee Jenerali Sarakikya alikuwa mwajiriwa wa Wizara ya Ulinzi na ndiye aliyejenga Jeshi letu la Wananchi likawa kama lilivyo sasa. Alikuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi (CDF) wa kwanza tangu Januari 1964 baada ya maasi ya KAR mpaka mwaka 1974 pale Rais na Amiri Jeshi Mkuu alipomteua kuwa Waziri wa Michezo na Utamaduni – “a Presidential Political Appointment”. Huko baadaye Mwalimu akamteua kuwa Balozi wetu kule Nigeria. Na alimalizia utumishi wake na kustaafu kwa umri akiwa Balozi wetu nchini Kenya.

Serikali kwa maana ya wizara alipostaafia “Mambo ya Nje” walimtayarishia mafao yake ya uzeeni, alilipwa kiduchu, lakini “Mambo ya Nje” (kwa maana ya Serikali Kuu ndiyo iliyomlipa HAZINA kwa maandishi yaliyotoka Mambo ya Nje).

Kwa vile taratibu za kijeshi zilionyesha alikuwa bado katika Holding List (kuazimwa nje ya uongozi wa JWTZ) walijenga hoja mwaka ule 2004 tarehe JWTZ linasherehea miaka 40 tangu liasisiwe, Rais Mkapa pale Uwanja wa Taifa alimtangaza Mzee Jenerali Sarakikya kuwa kapandishwa cheo kutoka Meja Jenerali na kuwa Jenerali kamili (Four Star General) na kwa mantiki ile alistaafu akiwa kama CDF mwasisi wa JWTZ. Leo hii anakula mafao ya uzeeni ya CDF mstaafu. Huo ni mfano mzuri wa utawala bora na wa sheria.

Je, Utumishi kweli walishindwa kumlipa Mzee Paulo Sozigwa kama Principal Secretary mstaafu? Ni uzembe au roho mbaya ya maafisa utawala maana Paulo alifikia Supper Scale ya mshahara kama Katibu Mkuu anakuwa Administrative Officer Grade I katika utumishi wa nchi hii katika Staff List ya watumishi. Wangepaswa kumjengea HOJA kama JWTZ walivyofanya kwa mtumishi wao mkuu namna ile. Hawakufanya. Why?

Nimeonyesha tu kuwa utaratibu ungeweza kabisa kufanyika mzee huyu akapatiwa mafao yake ya uzeeni. Bado nafikiri Taifa halikumtendea haki mtumishi huyu.

Bado naona Mzee Sozigwa alibaguliwa kimizengwe tu maana hakuna utaratibu wa mtiririko wa utumishi uliotumika kumkatili mafao yake ya uzeeni. Hivyo hakustahili kutendewa hayo aliyotendewa na watawala vijana. Alistahili na bado anastahili kulipwa mafao yake kama makatibu wakuu wengine waliostaafu na wakalipwa kwa misingi ile ile ya date of 1st appointment na date of retirement, mamlaka husika inazo. Mbona mzee Apiyo, Ikulu ilimjengea hoja na akapata stahili ya makatibu wakuu? Kwa nini haikuwa hivyo kwa Katibu Mkuu Sozigwa?

Mwalimu Nyerere aliwateua maafisa aliowaona wanafaa kufanya nao kazi na wala hakuwa na mfuko wa pekee kulipa watu awapendao. Wote ni watumishi wa Serikali Kuu na Hazina inawajibika kuwalipa. Wengine wote mbona wamelipwa?

>>ITAENDELEA

1059 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons