Barcelona imetangaza kuwa wamekamilisha usajili wa Philippe Coutinho kwa mkataba wa miaka mitano kutoka Liverpool

Miamba hao wa La Liga walimkosa Mbrazili huyo dirisha la uhamisho wa majira ya joto licha ya kutoa ofa tatu nono, lakini baada ya tetesi za muda mrefu hatimaye wamfanikiwa kuipata saini yake kwa dili linalokadiriwa kuwa £142m.

Liverpool wamethibitisha kuwa wamefikia makubaliano na Barcelona kumuuza mchezaji huyo wa miaka 25, na dakika chache baadaye miamba hiyo ya Hispania waliainisha taarifa za mchezaji huyo kutua Camp Nou.

Coutinho amemwaga wino kusaini mkataba ambao utamweka katika klabu hiyo hadi 2023, na klabu yoyote itakayotaka kumnunua italazimika kutoa €400m (£354.6m) kiasi kilichowekwa kwenye mkataba wake.

Coutinho amefunga magoli 54 katika mechi 201 katika kipindi chake cha miaka mitano Liverpool, baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Inter Milan kwa kiasi cha £8.5m tu mwaka 2013.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazili amekuwa mchezaji wa pili ghali wa muda wote nyuma ya Neymar, ingawa hilo litabadilika mara Kylian Mbappe atakapokamilisha uhamisho wake kwenda Paris Saint-Germain mwisho wa msimu huu.

1547 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!