Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli“Hayawi, hayawi, yamekuwa”. Kweli hayo ndiyo mapenzi yake Mwenyezi Mungu. Ulimtanguliza mbele wakati wa kampeni zako na sasa yametimia.

Kusema kweli kumtanguliza na kumweka mbele Mwenyezi Mungu kuna faida nyingi.

Nimezoea kuwaambia watoto wangu kuwa “kama baba awahurumiavyo watoto wamchao”, ndivyo na Mwenyezi Mungu awavyowahurumia wamchao.

Kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa. Napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumuinua Mheshimiwa Dk. Magufuli kuwa kinara wa nnchi yetu kati ya wagombea wanane kwa kiti cha urais kupitia vyama vyao.

Sifa na Utukufu tumrudishie yeye aliye hai daima na mwenye uwezo kwa mambo yote duniani na mbinguni; yeye aliye mfalme wa amani.

Naamini kuwa kupitia Dk. Magufuli, akiwa Rais wa Awamu ya Tano ya utawala wa nchi yetu, amani itaendelea kutawala maana ataliongoza Taifa kwa mapenzi makubwa kwa watu wote bila ubaguzi wala upendeleo wa aina yoyote. HONGERA SANA RAIS MTEULE WA JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA.

Baada ya utangulizi huo, niseme kwamba wakati wa kampeni ulitoa ahadi nyingi. Cha msingi ni kuziweka katika vipaumbele mbalimbali kwa maana kwamba ipi uanze nayo na zipi zifuate.

Kwa mtazamo wangu elimu ni ufunguo wa maisha na kumwezesha kila Mtanzania kufanya mengi ya kimaendeleo anapokuwa ameelimika. Hili ndilo la kuvalia njuga kwanza- yaani elimu kwa ngazi zote; walimu na vifaa shuleni.

Kuna suala la usaalama wa chakula. Tunataka kila mwenye nguvu afanye kazi. Hakuna kuzembea.  Hii itawezekana iwapo mtu ana hakika ya kupata chakula. Lakini asiye fanya kazi, basi na asile. Wavivu wasipewe nafasi au wazururaji nao ni adui kwa maendeleo yetu.

Kuna suala la upatikanaji wa maji safi na salama. Tunahitaji maji kuzalisha umeme, tunahitaji maji kwa umwagiliaji na hili linaendana na usalama wa chakula; tunahitaji maji kwa viwanda; tunahitaji maji hospitalini, vituo vya afya, kwenye zahanati; tunahitaji maji kwa ajili ya mifugo yetu; tunahitaji maji kwa ajili ya wanyamapori wetu.

Suala la upatikanaji maji liunganishwe na suala la kuhifadhi misitu ya asili ambayo ni muhimu mno kwa upatikanaji wa maji nchini.

Hali ya misitu si nzuri na ndiyo maana ukame unatuandama. Chemi chemi, vijito na mito sehemu kadhaa nchini ni tupu maana hakuna hata tone la maji. Miti inakatwa hovyo, matumizi ya mkaa yamekuwa makubwa sasa; usimamizi katika misitu yetu ni duni.

Ili mazingira ya nchi yetu yasiendelee kuharibika, utashi wa kisiasa hasa kwa ngazi za juu kama aliyoipata Dk. Magufuli ni budi uwepo: MISITU NI UHAI – TUITUNZE, ITUTUNZE.

Afya na matibabu ni mambo ya msingi sana. Pia uliahidi viwanda ili kupatikane ajira kwa vijana na wasomi wetu na hatimaye kuboresha maisha kwa Watanzania wote nchini kote.

Kwa upande wa miundombinu, wewe ni mjuzi katika eneo hilo.  Yapo mengine mengi uliyoyaahidi kuyatekeleza na miaka mitano si mingi.

Utaona kwa maisha ya kila siku yaani “funga (jioni) fungua (asubuhi)” miaka imekwisha na kama hukujipanga vizuri unabaki kushanga umefanya kitu gain. Usiwape mwanya wapinzani na maadui wako kuweza kupenya na kwa maneno yako; “SASA KAZI TU” tusonge mbele na iwe mbele kwa mbele, kurudi nyuma mwiko.

Nimalizie pongezi zangu kwa kuyasema masuala matatu: Mosi, msingi wa maendeleo ni kwa kila mtu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Hili liwekewe mkazo sana maana kwa nyakati hizi wengi tumekuwa wavivu. Tunakimbilia kupata fedha kirahisi (easy money). Usomaji mitandao na magazeti ya udaku katika ofisi nyingi za umma unachukua nafasi kubwa kuliko kazi. 

Nidhamu kazini pia imedorora kwa kiasi fulani na hii inasababishwa kwa kuajiri watumishi kwa kujuana, kupendeleana, wakubwa kushinikiza watoto wao au ndugu zao wa karibu waajiriwe wakati hawana ujuzi wa kazi husika au elimu ya kutosha.

Udanganyifu umeongezeka hivyo ukweli katika utendaji wetu umepotea; bora uongo katika siasa kuliko kuongopa katika shughuli za utendaji.

Mheshimiwa Rais Mteule, msemo wako: “SASA NI KAZI TU” uwe ndiyo msingi wa kuimarisha utendaji serikalini. Viongozi wote wawajibike ipasavyo bila woga au kumwonea mtumishi. Watumishi wote watimize wajibu wao ipasavyo. Asiye na kazi za kumtosha apewe kazi za kutosha. 

Matumizi ya simu za mkononi wakati wa kazi yaangaliwe maana hupoteza muda mrefu kwa ku-chart; na matumizi ya mitandao ya kijamii bila kufanya kazi ni mbaya kwa uhai wa Taifa letu na watu wake.

Pili, ni kupambana na mafisadi na wala rushwa. Hili ni tatizo la siku nyingi. Wakati umefika liwe ni jambo la kihistoria. Watanzania wana imani na wewe. Sasa fanya kweli. Mianya yote ya rushwa na ma-pipe yote ya mafisadi vifungwe au vikomeshwe mara moja. Usione haya katika hili.

Wanzania wamekuchagua wewe kama Magufuli na si kwamba wamechagua chama, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kama wangeaangalia chama usingepita. Wengi wanasema wamechoka na chama kutokana na ufisadi, wizi kwa fedha za umma na rushwa, lakini pia na suala la dawa za kulevya. Mateja yamekuwa mengi kutokana na ulegevu katika kudhibiti uingizaji.

 Katika kushughulika masuala haya; umuhimu wa tingatinga ndipo unapoonekana maana utapasua sehemu zilizoshindikana.

Jambo la tatu; ni kuimarisha usimamizi katika sekta zote na kwa ujumla wake. Tatizo letu ni kulegalega shughuli za usimamizi. Kwa mfano, Jiji la Dar es Salaam ni chafu karibu maeneo yote kwa nini?

Usimamizi haupo wala anayejali hayupo. Mazingira ya Jiji yanaleta kichefuchefu karibu kila mahali. Tabia za kutupa taka hovyo au kumwaga na kutiririsha majitaka zimekithiri sana. Je, Jiji halina wasimamizi wake? Kama wapo, kulikoni huko?

Mimi naamini kwamba kila mmoja wetu akiwajibika ipasavyo, na usimamizi ukiimarishwa pamoja na viongozi kutimiza wajibu wao bila shuruti; hatutaona uchafu katika maeneo yote ya Dar es Salaam, majini na miji mingine nchini.

Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akujalie baraka zake nyingi uwe na BUSARA na HEKIMA kama alivyokuwa Mfalme Suleiman na ukaweze kuliongoza Taifa la Mungu vizuri. Yote yawezekana kwake aaminiye. Nina imani yatawezekana chini ya uongozi wako.

Mwenyezi Mungu akujalie uunde timu nzuri ya kukusaidia katika harakati za kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Tanzania. Hakuna shaka tutafika bila shida yoyote.

“HAPA NI KAZI TU” TUCHAPE KAZI TUSONGE MBELE IPASAVYO,  MWENYEZI MUNGU AWE PAMOJA NAWE UWEZE KUCHANGIA MAENDELEO ENDELEVU KATIKA NCHI YETU”

 

Mwandishi wa makala hii, Dk. Kilahama ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, mstaafu katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Anapatikana kupitia simu: 0783 007 400.

By Jamhuri