Dar es Salaam

Na Christopher Msekena

Wiki chache zilizopita zimekuwa mbaya kwa rapa gwiji nchini, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, ambaye amekuwa akipatiwa matibabu ya maradhi yanayomsumbua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Licha ya kuwapo kwa ufaragha wa familia kuhusu kinachomsumbua rapa huyo ambaye pia ni mwanasiasa, mashabiki na wadau mbalimbali wamekuwa na kiu ya kutaka kufahamu maendeleo yake kwa njia mbalimbali.

Ndiyo maana wiki jana familia ikaona kuna ulazima wa mashabiki na wadau mbalimbali kumpa mkono wa pole Profesa Jay kwa kushiriki kuchangia gharama za matibabu za rapa huyo ambazo ni zaidi ya Sh milioni 4.

Mbali na michango ya fedha ambayo familia iliwaalika Watanzania kumchangia, familia ya mzee Haule ikawapa nafasi mashabiki hao kufanya maombi maalumu kwa ajili ya Profesa Jay yaliyofanyika Jumamosi iliyopita kwenye viwanja vya Leaders Club na kuhudhuriwa na wasanii, viongozi wa kisiasa, ndugu, jamaa na marafiki kufanya dua.

Katikati ya hayo serikali kupitia Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akaweka wazi kuwa kuanzia sasa (Ijumaa wiki iliyopita), serikali itagharamia matibabu yake yote mpaka atakapopona na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Kwa hili serikali ‘imeupiga mwingi’ na inastahili pongezi kwa kuchukua hatua ambayo kila mdau wa sanaa alikuwa anasubiri ukilinganisha na hadhi na ukubwa wa Profesa  Jay ndani na nje ya sanaa.

Hii ndiyo heshima ambayo Profesa Jay alistahili kuipata kutoka kwa serikali kutokana na ukweli ambao hakuna anayeweza kuupinga juu ya mchango mkubwa wa rapa huyo kwenye muziki nchini kwa muda wote aliokuwa na afya njema.

Kila mmoja anaweza kuuona mchango wa Profesa kwa namna yake. Ukiwauliza wasanii watakwambia jinsi Profesa alivyokuwa na mchango kwenye sanaa kwa namna mbalimbali.

Wapo wasanii wakongwe wenzake wanaosema jinsi Profesa alivyowapa msukumo mkubwa kwenye harakati mbalimbali za kutafuta nafasi ya kufahamika enzi muziki wa Bongo Fleva ukiwa hauna heshima.

Mara kadhaa wasanii mbalimbali wakongwe wamekuwa wakimwelezea Profesa Jay kama chachu ya wao kuingia kwenye muziki na kuruhusiwa kufanya muziki huo na wazazi wao.

Mfano ni Chid Benzi ambaye amekuwa akisema kwamba mama yake alimruhusu kufanya muziki kwa sababu ya Profesa. Pia aliweza kuwaaminisha wazazi wengi kuwa Bongo Fleva si uhuni kama ilivyokuwa ikiaminiwa hapo mwanzoni.

Pia wapo wasanii wa miaka ya hivi karibuni ambao Profesa Jay kwao ni kioo, wanamtazama kama ‘role model’ kwa namna mbalimbali ambazo kila msanii anamtazama rapa huyo.

Miongoni mwa wasanii hao wanamtazama Profesa katika suala zima la utunzi wa mashairi yanayoishi na kudumu miaka na miaka kama ambavyo rapa huyo alifanya kwenye ngoma zake zinazodumu kama Chemsha Bongo, Ndiyo Mzee na nyinginezo.

Huyu ni aina ya wana ‘hip hop’ wachache ambao tungo zao hazina matusi, ndiyo maana muziki wake unaweza kusikilizwa na watu wa rika zote hata kama wimbo unahusu mapenzi. Namna alivyoweza kutunga nyimbo safi zisizo na ukakasi.

Pia wapo wasanii ambao wanamtazama Profesa kama ‘role model’ kwenye suala zima la nidhamu kama msanii. Huyu ndiye msanii ambaye kwa miaka yote aliyofanya muziki amekuwa hana skendo.

Amekuwa akifanya muziki wake na kuacha uongee na mashabiki, si aina ya msanii aliyependa skendo ndizo ziongoze muziki wake, bali muziki wake ndio umtambulishe.

Na mashabiki wamekuwa wakimfahamu hivyo, ndiyo maana hata lilipokuja suala la kuchangia matibabu yake, mwamko umekuwa mkubwa na wengi walitarajia serikali iweke mkono wake kwa rapa huyo ili kufanikisha matibabu yake.

Mbali na muziki, Profesa Jay amegusa maisha ya wengi hata kwenye maisha yake ya kisiasa. Ukiacha kugusa wananchi wake wa Mikumi ambao amewahudumia kama mbunge kwa miaka mitano kupitia Chadema, Profesa amekuwa kioo kwa vijana wengi.

Licha ya kuwapo kwenye chama cha upinzani lakini rapa huyo amekuwa akiwavutia wasanii na vijana wengi kuingia kwenye ulingo wa siasa kwa sababu ameonyesha kuwa inawezekana kijana kutumia uwezo alionao kulitumikia taifa.

Profesa Jay amekuwa hana makundi, licha ya kuwapo Chadema amekuwa hajengi uadui zaidi ya kuwa na mchango chanya kwenye chama chake na taifa kwa ujumla.

Ndiyo maana unaweza kuona hata ziliposambaa taarifa za kuumwa kwake, si Chadema pekee wameguswa bali hata CCM na vyama vingine wamekwenda kumpa mkono wa pole.

Hivyo niipongeze serikali kwa kuona umuhimu wa kumpa heshima Profesa Jay kwa kulipa gharama zote za matibabu kwa sababu ya mchango wake mkubwa kwenye muziki, siasa na mambo mengine ya kijamii.

By Jamhuri