Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ndani ya miezi sita umetumia Sh trilioni 1.1 kulipa pensheni za wastaafu.

Kiwango hicho kinajumuisha jumla ya Sh. bilioni 880 ambazo wamelipwa wastaafu 10,000 ambao pensheni zao zilisimamishwa katika Mfuko wa PSPF kupisha shughuli ya kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ya GEPF, LEPF na PPF, huku Sh bilioni 300 zikitajwa kulipwa kwa wastaafu  waliostaafu tangu Agosti, mwaka jana.

Afisa Mkuu wa Uhusiano PSSSF, Eunice Chiume, amelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa thamani ya mfuko huo baada ya mifuko kuunganishwa imefikia Sh trilioni 5.5. Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali, kiwango hicho kinakaribiana na thamani ya mtaji wa Benki ya CRDB – Sh trilioni sita.

“Mfuko kwa sasa umekuwa mkubwa kuliko hata NSSF. Wanaosema kwamba mfuko hauna fedha si kweli …. kuna utaratibu wa kufanya malipo, si tu kwamba hela tunazo basi unalipa tu, hapana. Unatakiwa ufuate taratibu, ukizikamilisha tunakulipa,” amesema Chiume alipofanya ziara katika ofisi za Gazeti la JAMHURI jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Amesema kuna wastaafu 227 kati ya wastaafu 10,000 ambao wameondolewa kwenye orodha ya malipo (pay roll) kutokana na kuwa na mapingamizi mbalimbali kama kushindwa kuwasilisha vyeti.

“Nikisema cheti, nafikiri wote mnanielewa, kuna mtu unakuta muda wa kustahili kulipwa umekaribia lakini wakati ule wa kuhakiki vyeti hakuleta vyeti. Unakuta mpaka anastaafu hajaleta cheti.

“Sisi tunashindwa kumlipa kutokana na sheria kutubana, kwa sababu matakwa ya kisheria ni kwamba yeyote atakayestaafu lakini akawa anakabiliwa na masuala ya kijinai au nidhamu hawezi kulipwa hadi awe amesawazisha kasoro zake na mwajiri wake,” ameeleza Chiume.

Amesema makosa hayo yameondolewa katika Sheria mpya Namba 2 ya mwaka 2018 ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma na kwamba ambao wamestaafu katika kipindi cha utekelezaji wa sheria hii watalipwa.

“Kila kitu huja na zuri lake na baya lake, kwa waliostaafu kwa mujibu wa sheria ya zamani hao watalipwa kwa mujibu wa sheria hiyo. Hatuwezi kuhamisha mabaya yao na kuyaingiza katika sheria hiyo mpya kisa sheria imeruhusu hata wenye makosa kulipwa, kama alivyoagiza Rais John Magufuli na sisi tunaitekeleza sheria hiyo kwa kipindi cha mpito cha miaka mitano tuliyopewa katika kulipa wateja wetu,” ameeleza na kuongeza kuwa huduma za PSSF zimeboreshwa kote nchini kwa kuhakikisha ofisi zinafunguliwa katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wastaafu hawahangaiki kufuatilia pensheni zao.

By Jamhuri