Na Aziza Nangwa
Baadhi ya wakazi wa Pugu Kinyamwezi wanalia kwa kupoteza viwanja, nyumba zao na kanisa walilokuwa wakilitumia kuabudu baada ya mtu waliyemtaja kwa jina moja la Shabani na kundi lake kuwavamia mara kwa mara usiku na mchana.
Wakizungumza na JAMHURI wakitoa kilio chao hicho, wanadai mtu huyo na kundi lake lisilojulikana amekuwa akifahamika hata katika serikali ya mtaa lakini mwenyekiti wao hamchukulii hatua.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao, Zaina Saidi – mmoja wa wahanga wa kuvunjiwa eneo lake, anadai yeye na mume wake walinunua eneo hilo mwaka 2020 kwa gharama ya Sh 3,500,000 kutoka kwa Frida Kessy. Anasema walinunua kwa kufuata taratibu zote kwa kupitia serikali ya mtaa na mwenyekiti aliwahakikishia eneo hilo halina mgogoro ni la mama Frida.
“Lakini baada ya kujenga nyumba ya vyumba viwili nilifika kuangalia eneo langu nikakuta nyumba imebomolewa na imejengwa nyumba nyingine,” anasema Zaina.
Anasema baaada ya kuona hivyo alikwenda serikali ya mtaa na kumweleza mwenyekiti lakini hakuna msaada alioupata.
Anasema alikwenda kwa aliyemuuzia eneo na kumweleza kuhusu kadhia hiyo lakini alimkuta tayari anapambana na mtu huyo katika vyombo vya sheria.
Anadai watu wengi waliouziwa eneo hilo pamoja naye maeneo yao yamevamiwa. Katibu wa Kanisa la Shekemu, Fortunate Mrisho, anasema walianza kuabudu katika kanisa hilo miaka mingi, eneo la kanisa ekari moja lilitolewa msaada na aliyewauzia viwanja.
Anadai baada ya Rais John Magufuli kufariki dunia walianza kuona watu wasiojulikana wakija kanisani na wakati mwingine wakiwafanyia fujo waumini.
“Waumini wengi waliacha kuja kanisani kwa hofu. Ndani ya mwezi mmoja ambao waumini waliacha kufika, akawekwa mchungaji mwingine anaendesha ibada, haijulikani alifika hapo kwa ridhaa ya nani.
“Eneo la kanisa lilitengwa tangu mwaka 2011 na mchungaji wetu anaitwa Anthony Walter,” anasema.
Yusta Ayola anasema alinunua uwanja na mumewe, John Chambo, mwaka 2021 walijenga wakahamia lakini baada ya muda aliibuka mtu mwingine akasema aliuziwa eneo hilo, akajenga ukuta hatua moja kutoka kwenye mlango wa nyumba yao.
“Aliyetuuzia maeneo, Frida, anajitahidi kuhakikisha migogoro iliyopo inakwisha japo tunaishi kwa hofu, hatujui kwa nini watu wanaamua kutusumbua,” anasema.
Mkazi mwingine aliyepoteza eneo lake, Aldo Mkili, ambaye anadai mwezi mmoja baada ya kununua eneo hilo akaondoka, aliporudi alikuta nyumba imekwisha kujengwa, hivyo amekuwa miongoni mwa watu wenye mgogoro.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Pugu Kinyamwezi, Kassim Mfinanga, alipoulizwa kuhusu mgogoro huo anasema anaufahamu, anawataka wananchi kuwa watulivu kwa sababu aliyeuza maeneo hayo ana kesi amefungua mahakamani.
“Aliyewauzia akipata ushindi watakuwa salama lakini akishindwa wanaweza kurudishiwa fedha au wakapewa maeneo mengine,” anasema.
Anasema masuala ya kuvunjiwa nyumba hayapo, kwani kama yangekuwapo yangeripotiwa Polisi, kwani ni kosa la jinai.
Mwisho




By Jamhuri