Wiki iliyopita makala hii iliishia katika aya iliyosema: “Mkakati wake [Raila Odinga] kuitisha kura za maoni kubadilisha Katiba nadhani umefikia tamati. Asante rais kwa kutia mkono wako katika uteuzi wa Odinga na kumshawishi akaukubali,” anasema Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro.” Je, unafahamu kuwa kabla ya uteuzi huu Odinga alikataa uteuzi mara kadhaa? Endelea…

Odinga aliwahi kuukataa Ubalozi Maalumu wa Umoja wa Mataifa aliokuwa ameteuliwa wakati nchi ikiwa katika hali tete ya kisiasa na kiuchumi baada ya uchaguzi wa Agosti, mwaka jana uliotenguliwa na Mahakama ya Juu nchini humo.

“Sasa kipaumbele chake kitakuwa ni kuliletea maendeleo Bara la Afrika, si kuhangaikia Katiba,” anasema Mbunge wa Bomachoge, Alpha Miruka, ambaye pia ni mpambe wa Ruto.

“Anakwenda kutuweka karibu na taasisi za kimataifa kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na nyingine nyingi. Sasa si mtu wa hapa. Hatutarajii kumwona tena kwenye mikutano ya hadhara na maandamano,” anasema Msaidizi wa Kiongozi wa Chama cha Ford Kenya, ambacho ni chama tanzu katika muungano wa NASA.

Hata hivyo, uhusiano wa chama hicho unalegalega kutokana na kiongozi wake mkuu, Moses Wetangula, kutofautiana na Odinga baada ya kuanzisha ushirika na Uhuru Kenyatta. Mfuasi mwaminifu wa Rais Kenyatta na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, David Murathe, anawashangaa wapambe wa Ruto na kusema mbio hizo sasa ndiyo zimeshika kasi huku Odinga akiwa kwenye chati.

“Majukumu yake mapya yamempandisha hadhi yeye na nchi yetu,” anasema Muthare na kuongeza: “Tumewaona wengi ambao nafasi zao kimataifa zimewabeba sana kuingia ikulu.” Katibu Mkuu wa Chama cha ODM cha Odinga, Edwin Sifuna, anasema: “Hatimaye jitihada zake zimeonekana hata nje ya mipaka ya nchi yetu. Hii ni sifa ya nchi ya Kenya… anaungana na kina Dk. Kituyi (Dk. Muksa Kituyi – waziri wa zamani katika serikali ya Rais Mwai Kibaki) sasa ni mkurugenzi wa moja ya mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UN).

Kiongozi wa Upinzani katika Bunge la Seneti na Seneta wa Siaya, Kaunti ya Siaya, James Orengo, anasema: “Kwa kuteuliwa kwake Kenya imepata sifa ya siasa kimataifa. Hili ni jambo la kushukuru. Ndiyo kabisa atakuwa kinara zaidi katika siasa zetu. Kama hakuna mtu aliyemwita afanye siasa, hivyo hivyo hakuna atayemlazimisha kung’atuka siasa kwa sasa.”

“ Raila ni mzalendo na mwana mapinduzi wa kweli. Afrika inamhitaji na Kenya inamhitaji pia,” anasema mbunge mwingine anayetajwa kwa jina moja la Wadanyi.

Rekodi ya kifisadi anayodaiwa kuwa nayo Makamu wa Rais, Ruto, ndiyo inamtia tumbo joto. Kwa sasa anapambana kusafisha kashfa ya kuvamia na kumega sehemu ya Uwanja wa Ndege wa Wilson katikati ya Jiji la Nairobi. Katika kiwanja hicho kilichopo eneo la vibopa, Ruto amejenga hoteli ya kifahari inayoitwa Weston. Wakurugenzi wa hoteli hiyo wanadaiwa kuwa ni Ruto, mkewe Rachel na binti yake, Charlene Chelegat.

Taasisi ya kupambana na Rushwa ya Kenya inachunguza sakata la kujimilikisha kijanja, na imefungua jalada la uchunguzi. Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, zinadaiwa kubariki ujenzi wa hoteli hiyo miaka 16 iliyopita, lakini mamlaka nyingine zinasema huo ulikuwa mchongo uliofanywa na Ruto. Siasa za Kenya ni moto. Odinga wengi wanamwita “Baba”. Dalili za mvua…

By Jamhuri