Taifa letu linakabiliwa na changamoto nyingi. Zimejitokeza changamoto ambazo kimsingi tunaweza kuondokana nazo. Sitazungumzia tishio la kitoto linaloelekezwa kwetu na taifa la Malawi. Binafsi sitaki kuamini kuwa mgogoro wa Ziwa Nyasa, ambalo Wamalawi kwa makusudi wanaliita Ziwa Malawi kwao ni mkubwa. Inawezekana Rais wa Malawi, Joyce Banda anatafuta umaarufu, lakini anaweza kuishia pabaya.

Haya mambo wakati mwingine yanahitaji kupata ushauri.

Inawezekana mchezo wanaoufanya Malawi wanalenga kufanya uchokozi wa makusudi kwa kuwa wamebaini uchumi wetu umeanza kukua na hivyo waturejeshe tulikotokea mwaka 1979. Vita ina gharama kubwa. Nasema ni kweli jeshi letu lisogezwe mpakani, lakini tusianzishe vita.

 

Sitanii, niwafahamishe Wamalawi kuwa kwa sasa hawana uwezo huo. Rais wao huyu mwanamama anatafuta umaarufu kwa kila mbinu. Ndiyo maana alidiriki kukataa mkutano wa Umoja wa Afrika usifanyike Malawi kwa kigezo kuwa atamkamata Rais wa Sudan, Omar Ali Bashir, kinyume na makubaliano ya viongozi wa Bara la Afrika.


Matendo ya mwanamama huyu, yanaanza kunitia wasiwasi kuwa huenda Afrika imepata kibaraka mpya. Bila kutumia akili mwanamama huyu, anaweza kuanzisha vita na Tanzania akitaraji kupata misaada kutoka kwa mataifa ‘changudoa’ yaliyotayari kuteketeza uchumi kidogo wa Afrika eti tu, ili wao wauze silaha zao.


Ni bahati mbaya kuwa Rais huyu, anaandaa mazingira ya kufurahisha Wazungu bila kujali historia ya bara letu na kuona kuwa wakati umefika sasa tusiishi kwa kutegeshea misaada bali tuwekeze katika uchumi wetu na nchi zetu ziweze kufanya biashara na mabazazi hawa na si kusubiria misaada yao. Ninachosema sheria za kimataifa ziheshimiwe. Ziwa Nyasa mpaka ni katikati ya ziwa na si vinginevyo.


Kichwa cha makala haya, kinasema ‘Rais Kikwete mbeleko ya Mahakama ikikatika…’ Haya maneno sikukosea katika kuyachagua. Naangalia mwenendo wa nchi yetu. Naangalia matukio yanayotuzunguka. Hofu niliyokuwanayo taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa sasa tumeubariki rasmi udini. Tumeruhusu kipengele cha dini ya mtu kuingizwa kwenye sensa.

 

Hapa sijeelewa hizo fomu zilizokwishachapishwa na makaratasi yote kwa ajili ya sensa itakuwaje. Sielewi iwapo yatachanwa au yatateketezwa. Sitaki kuamini na sitakaa niamini kuwa kipengele hiki kina tija yoyote kwa taifa letu. Narudia, hivi leo tukipata takwimu kuwa Waislamu ni asilimia 95 ya wakaazi wa nchi hii kiuchumi hili litatuongezea nini?

 

Sitanii, binafsi napenda kuamini kuwa kwa Serikali kukubali kipengele hiki imefungua mkondo wa udini nchini. Wakati mataifa mengine yakipigana vita kwa ajili ya ukabila, hapa kwetu tujiandae kupigana vita kwa ajili ya udini. Hizi chokochoko hazitatuongezea shibe wala afya. Kama ulivyokuwa msimamo wa taifa hili tangu tupate uhuru, ingekuwa vyema tukaendelea na uhuru wa kila mtu kuamini imani atakayo bila kuingiliwa.


Kimsingi leo nataka kuzungumzia mada ya migomo inayoliandama taifa letu kwa kasi. Ni hivi karibuni tumesikia mgomo wa madaktari, ambapo si siri kuwa wapo Watanzania waliopoteza maisha. Wiki hii tuliyomaliza tena umelindima mgomo wa walimu na tukashuhudia watoto wanakwenda mitaani. Nimesikia chama kingine cha wafanyakazi nacho kinaandaa mgomo.


Tumeuona utawala wa sheria, ambapo Serikali imekimbilia kwenye Mahakama ya Kazi na kupata zuio la mgomo. Tumeshuhudia Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba naye akitii amri ya mahakama na kuwambia walimu warejee kazini. Binafsi napata mashaka makubwa. Naogopa kila nikiangalia mwisho wa barabara ndefu tuliyoikanyaga. Nashindwa kuelewa iwapo wakubwa wa nchi hii wanajipa muda kupitia matukio haya.

 

Tukio la kipigo cha Dk. Stephen Ulimboka, wapo wengi wanaoihusisha Serikali kupitia vyombo vyake na kipigo hiki. Nafahamu mara kadhaa Serikali imekanusha kuhusika na utekaji huo na Gazeti la Mwanahalisi lililothunbutu kutaja majina ya hao linaodai kuwa walimteka Dk. Ulimboka sasa limefungiwa. Binafsi nasema Gazeti la Mwanahalisi linaweza kuwa na makosa, lakini utaratibu uliotumika si sahihi. Kulifungia gazeti ni dharau ya wazi kwa tasnia ya habari.

 

Mbona walimu walipotangaza mgomo kitu kilichoiudhi Serikali haikukimbia kukifungia au kukifuta CWT? Badala yake imekimbilia mahakamani kuomba amri ya mahakama kusitisha mgomo? Kimeshindikana nini Serikali kwenda mahakamani kuomba gazeti la Mwanahalisi lisiendelee kuchapisha taarifa za Dk. Ulimboka, lakini likaendelea na masuala mengine? Kilichopo hapa ni ushahidi wa wazi kuwa Serikali inadharau taaluma ya uandishi wa habari. Haina hofu kufanya hicho ilichokifanya, isichoweza kuthubutu kukifanya kwa Chama cha Walimu Tanzania.

 

Nieleweke vyema hapa, sisemi naunga mkono kila kilichofanywa na Mwanahalisi, isipokuwa kufungiwa si utaratibu unaokubalika katika utawala wa sheria. Huu ni mwendelezo wa sheria za kikoloni zilizotumiwa na Wakoloni kutugawa sisi wazawa kisha tukatawaliwa kiulaini kuliko mchicha kukaangwa kwa mafuta. Sitanii, kati ya matatizo ninayopata ni kufahamu iwapo migomo hii inawakera wakubwa na wanafahamu chimbuko lake.

 

Leo ukiwa na Sh 10,000 mkononi ni sawa na petroli. Ukinunua hata sindano ya Sh 50, fedha iliyosalia inayeyuka sawa na petroli iliyoachwa wazi juani. Mfumuko wa bei unatisha. Wafanyakazi hawana uhakika wa maisha. Hasira za wafanyakazi zinaazia mbali. Spika wa Bunge Anne Makinda, anawambia Watanzania kuwa maisha yamepanda mno Dodoma hivyo mbunge anastahili kulipwa posho ya Sh 200,000 kwa siku, wakati mwalimu anachapa kazi kwa siku 30 mwisho wa mwezi anakinga mkono kupata Sh 246,000. Upo hapo?


Kwa sisi tuliojaliwa kumiliki bajaji, tunakwenda sheli kujaza mafuta ya Sh 5,000 kwa tabu maana ni lita mbili, ila wakubwa hawa wanatanua na mashangingi yanayomeza lita mbili kwa kilomita 10. Kumbuka hii inafanywa hivyo kwa kodi zetu. Tunaambiwa kwa sasa Serikali inamiliki magari yenye thamani ya Sh trilioni 5, sawa na nusu ya bajeti nzima ya Serikali yetu.

 

Kiroba cha unga hakishikiki. Sikukuu za Iddi (zote elftri na elhaji), pasaka, krismasi na mwisho wa mwaka hazina tofauti na tarehe yoyote ya mwezi wowote ndani ya mwaka kwa sasa. Tulizoea sikukuu hizi zikiwadia wazazi wanajikusulu wanawanunulia nguo mpya watoto wao na kupika japo pilau au filigisi zinaonjwa angalau mara moja kwa mwaka katika familia nyingi, leo bila kujali ni mwaka mpya ugali kwa maharage mtindo mmoja.


Kariakoo ilikuwa zamani ukipita wiki kabla ya siku kuu msongamano unatisha, lakini sasa unaweza kusukuma mkokoteni ukapita Mtaa wa Kongo wote bila kumuomba mtu radhi, maana huna wa kukwaruzana naye. Maduka hadi ya nguo wameweka wapigadebe kuvutia japo senti tano. Kwa bahati mbaya sina uhakika kama viongozi wetu wanayajua haya. Wako kimya wanaendelea na maisha yao. Wakitaka kwenda uwanja wa ndege barabara zinafungwa, wanapita kasi utafikiri wanapeleka barua ya chui. Tena siku hizi hata magari yao wameweka makaratasi ya kuzuia aliyeko nje asione ndani, wenyewe wanaita tinted, wakati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa anapanda nyuma ya Landrover 109 na kupunga mikono mtaa hadi mwingine.

 

Najua hapa kwetu walau tuna usataarabu. Hata hivyo, wakati umewadia. Viongozi wenye kutegemea mbeleko za mahakama watafika mahala wananchi watachagua kutumia sanduku la kura. Tunachohitaji sisi ni maisha bora na wala si maelezo ya kuwa bei ya mafuta imepanda duniani. Kama wao wamepandisha bei ya mafuta na kwao ni jangwani kwa nini sisi tusiweke mkakati wa kuwa na mahindi, mchele au viazi vya kutosha nasi tukapandisha bei ya vyakula tukaona kama wao watakula mafuta yao?


Sitanii, tumeingiza siasa kila pahala. Hatukusanyi kodi. Hatuna mpango madhubutu wa kuhakikiksha tunatoka hapa tulipo. Wasiwasi wangu ni kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimekubali matokeo. Sioni tena matamko ya chama hicho ya Siasa ni Kilimo, Uhuru na Kazi au Azimio la Musoma. Wapendwa wananchi tunzeni shahada zenu. Muda si mrefu tutaangalia nani ana ahadi yenye nia njema kwa taifa letu, nasi tutamwingiza huyo kwenye mjengo bila kujali itikadi. Akichemsha naye tutamwondosha.


 

By Jamhuri