Rais Magufuli fungua milango zaidi

Na Deodatus Balile

 

Wiki iliyopita Rais John Pombe Magufuli amefungua milango ya kukutana na viongozi wastaafu. Amekutana nao Ikulu na akasema utaratibu huu ataundeleza. Akasema atakutana nao mara kwa mara na katika kukutana nao hakuwabagua. Amekutana na wale walioko Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata wale waliohamia upinzani kama Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Sitanii safu hii ni fupi. Kwa maana hiyo sina uhakika kama nitachambua mawazo ya viongozi wote aliokutana nao nikamaliza, ila nitagusia wanne tu; Rais Benjamin Mkapa, aliyesema anatamani kuona Serikali ikijitambulisha kama “Serikali ya CCM”, badala ya “Serikali ya Magufuli”. Nitagusia kauli ya Lowassa juu ya kutopuuza “uonevu kwa baadhi ya watu na tishio la amani kupotea.” Nitamzungumzia pia kauli ya Jaji Mkuu (mstaafu), Barnabas Samatta, aliyetaka uwepo “utawala wa sharia”.

Pia nitazungumzia kauli ya Jaji Mkuu (mstaafu), Augustino Ramadhani, aliyesema: “Amani ni tunda la haki, kama utakuwa na haki hakuna matatizo, amani itakuwepo, lakini kama haki itatetereka kidogo hapo tutakuwa na wasiwasi wa amani. Tukiangalia haki, amani yenyewe itajiangalia, sasa hivi nazungumza hii habari ya haki, Mheshimiwa Rais katika ngazi zote, kuanzia kwako Mheshimiwa Rais tutekeleze haki, uje kwa mawaziri, uje kwa (wakuu wa mikoa) Regional Commissioners uje kwa (wakuu wa wilaya) DC na kila ngazi zote tutekeleze haki.”

Sitanii, kwanza nikiri tangu mwanzo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Magufuli imerejesha nidhamu katika utumishi wa umma. Nayakubali mapambano dhidi ya rushwa inayofanya serikali hii, na kwa sababu Rais amesema yuko tayari kupokea ushauri, namshauri mapambano haya yasibague. Hata askari aliosema wanachukua za “kubrashi” viatu, sasa wamegeuka kero. Wanalazimisha rushwa. Ukikamatwa hata kama gari limetoka dukani, utaambiwa limeoshwa lakini halikutakata. Hawa ni kero.

Nikushukuru Rais Magufuli kwa kukubali kupokea ushauri. Najua wewe umewasikiliza vyema viongozi hawa wastaafu, ila na sisi waandishi tunawasikia wananchi huko mtaani wanavyosema. Utafiti wa Twaweza umeonyesha umaarufu wako umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 hadi asilimia 55, mwaka 2018. Utafiti huu si wa kupuuza. Taweza nimeona wameanza kubezwa na baadhi ya watu, lakini Twaweza wamefanya kazi ya kioo.

Sitanii, sisi wenye mapenzi mema na nchi hii na hasa tuliopata bahati ya kuzaliwa enzi za Chama cha TANU, tunazikumbuka ahadi za mwana-TANU zinazosema:

  1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
  2. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote.
  3. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.
  4. Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa.
  5. Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.
  6. Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.
  7. Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu.
  8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.
  9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika.
  10. Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.​

Sitanii, ahadi Na. 8, naamini wastaafu wameitumia vyema. Binafsi nimezikumbuka ahadi hizo tangu enzi za ujana wangu na naziishi. Maneno ya Lowassa, Samatta na Ramadhan, si ya kupuuza. Amani ni tunda la haki. Nchi zote unazoziona zimeendelea zimepitia wakati mgumu. Ulaya wamepinga vita kwa miaka zaidi ya 600. Marekani walikuwa watumwa. Uingereza na Warumi wamepata kuwa vijogoo wa dunia.

Dunia hii imepigana Vita Kuu ya Dunia mara mbili. Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilikuwa mwaka 1914 – 1918 na miaka 11 baadaye ikatokea Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mwaka 1939 hadi Mwaka 1945. Vita hii ilitokana na wakubwa duniani kupuuza utawala wa sheria. Kila mtu aliamua kutoa amri iliyompendeza, wakajikuta wanaingiliana si tu katika makoloni, bali hata ndani kwa ndani wakazisigina haki za raia wao na kuzalisha upinzani mkali.

Baba geuza shingo upande wako wa kuume uwaangalie baadhi ya wateule wako wanavyosigina sheria kwa sasa. Mhe. Rais, haijapata kuwa sifa kwa nchi yoyote kuwapo kwa kundi la “watu wasiojulikana” au baadhi ya wananchi kupotea na taifa likaishi kwa hofu. Tunayo vita ya kuondoa ujinga, maradhi na umaskini, tuunganishe nguvu kupigana vita hii na si kutafutana!

Sitanii, baada ya dunia kuchoka migogoro ya utawala usio wa sheria, kwa viongozi kuongoza mataifa yao kwa matamko na kuzaa vita isiyokoma, Siku ya Jumatatu, Desemba 10, mwaka 1948 nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) walipitisha Azimio la Haki za Binadamu. Ndani ya Azimio hili zimesheheni haki mbalimbali ambazo zimekuwa chimbuko la sheria kwa kila nchi. Leo tuna miaka 70 dunia haijapigana tena vita tena.

Tanzania iliridhia tamko hili kupitia mabadiliko ya 5 ya Katiba ya Tanzania, mwaka 1984 yaliyoingiza ibara ya 12 hadi ya 29 inayohusu haki za binadamu katika Katiba ya Tanzania. Sasa nikwambie Mzee Magufuli, huku mtaani vyuma vimekaza. Uchumi wa mtu mmoja mmoja ni mgumu haijapata kutokea. Wiki ijayo, nitaeleza tufanye nini kujenga msingi wa kudumisha amani, serikali kupata kodi nyingi zaidi na wananchi kujinasua katika lindi la kufilisika.