Rais Magufuli, matumizi ya mkaa ni janga la kitaifa

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na rehema zake nyingi anazotujalia kila kukicha. Nimshukuru pia Mungu wetu aliye hai kwa kutujalia kumpata Rais wa Jamhuri ya Tanzania anayeonekana kuwa msitari wa mbele kwa kuyajali maslahi ya Watanzania wa mijini na vijijini.

Rais John Magufuli, ameonyesha kuwa yeye ni kiongozi thabiti na aliyedhamiria kuwaondoa watanzania katika ‘ngome’ ya umaskini uliokithiri.

Kusema kweli Mheshimiwa Rais amekuwa mfano nzuri wa kuigwa na viongozi wengine siyo tu ndani ya Tanzania, bali duniani.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema” “Kuongoza ni kuonyesha njia”. Hata hivyo yawezekana zikawapo njia kadhaa za kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Mathalani, kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza. Mhusika wa safari anaweza kufika Mwanza kutoka Dar es Salaam kwa kupitia Moshi-Arusha-Nairobi-Musoma na hatimaye kufika Mwanza.

Anaweza pia kupitia Morogoro – Dodoma – Singida – Shinyanga na hatimaye kufika Mwanza. Vilevile, anaweza kupitia Morogoro – Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Tabora – Nzega – Shinyanga na mwishowe akaingia Mwanza. Isitoshe mhusika anaweza akatumia usafiri wa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza; kutoka Dar es Salaam kupitia Kilimanjaro hadi Mwanza; au kutoka Dar es Salaam hadi Nairobi na kupitia Kilimanjaro hadi kufika Mwanza.

Mfano huu nimeutoa kuonyesha kuwa zipo njia kadha wa kadha na zenye gharama tofauti. Hivyo, anayeongoza anatakiwa kuwa makini katika kuchagua ni njia ipi iliyo rahisi na yenye gharama nafuu ili wasafiri anaowaongoza waweze kufika huko waendako bila ya kuwa na uchovu mwingi, lakini pia kwa gharama nafuu.

Baba wa Taifa aliposema “kuongoza ni kuonyesha njia” alimaanisha kwamba viongozi tutakaowaweka madarakani iwe kwa njia ya kupigiwa kura au kwa kuteuliwa; wanayo dhamana kubwa ya kuwaongoza Watanzania wote ili waweze kupambana na maadui ambao ni Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Vilevile Baba wa Taifa aliongeza kuwa pamoja na hayo yote tunahitaji “siasa safi na uongozi bora”; kwa maneno mengine uongozi uliotukuka na wenye kujali maslahi ya Watanzania wote mijini na vijijini.

Nayasema haya kuashiria kuwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano inazo kila aina ya dalili zinazoashiria kuwa sasa Mwenyezi Mungu ametuinulia  kiongozi atakayetuongoza kupitia njia iliyo sahihi na itakayotusaidia kuinua uchumi wa Taifa letu kwa kutumia rasilimali na fursa tulizonazo.

Kwa pamoja inatupasa tumwombee Rais wetu ili Mwenyezi Mungu amlinde na hatari zote. Njia za maadui wake ambao ni maadui wetu ziwe ni za utelezi mtupu. Mashimo watakayoyachimba ili Rais atumbukie hayo watumbukie wenyewe na badala yake Mheshimiwa Rais azidi kujazwa moyo wa hekima na busara pamoja na kuwa na nguvu za ki-Mungu. Mkononi kwake aishike fipo kama vile Nabii Mussa alivyoishika fimbo akaunyosha mkono wake akayapiga maji yakagawanyika mara mbili hivyo kukapatikana njia katika Bahari ya Sham na Wana wa Israel wakaweza kuvuka. Maadui walipowafuatilia ili wawaaangamize na walipofika katikati ya bahari wakidhani kuwa nao watavuka salama, Nabii Mussa aliunyosha mkono wake tena na kwa kutumia fimbo aliyokuwa nayo akayapiga maji na bahari ikarejea katika uhalisia wake. Maadui wote wakaangamia bila kubaki hata mmoja.

Nathubutu kusema kuwa Mwenyezi Mungu ametuinulia kiongozi ambaye yuko tayari kwa dhamira ya kuwaongoza Watanzania bila yujali itikati au imani zao

Desemba 17 hadi 21 mwaka huu nilitembelea maeneo ya Sumbawanga na Mpanda. Nikiwa Mpanda niliweza kufika katika Kata ya Katuma ambako nilikutana na baadhi ya wananchi. Ilitokea kuwa tukiwa katika matembezi kwenye eneo la msitu wa kijiji tukakutana na mwanaume aliyekuwa akitoka mahali fulani akiwa na baiskeli na redio kifuani mwake.

Tulimuuliza kama anatoka kununua redio; yeye alijibu: “Hapana, hii ni radio yangu na nimekuwa nayo kwa siku nyingi”. Ni kwa nini alikuwa nayo katika matembezi yake, alijibu kuwa anatembea nayo ili aweze kusikiliza taarifa mbalimbali na kikubwa aweze kujua nini Mheshimiwa Rais Magufuli anakifanya.

Aliongeza: “Navutiwa sana na utendaji wake haswa kwa ujasiri wake wa kupambana na mafisadi”. Vilevile, tukiwa Mpanda mjini majira ya saa moja jioni tulikutana na akina mama watatu waliokuwa wakiuza mahindi ya kuchoma. Tulipozungumza nao mmoja akasema: “Muda si mrefu tutafunga shughuli za kuchoma mahindi ili turejee nyumbani kuangalia TV zetu na kusikiliza taarifa ya habari saa mbili usiku”.

Walisema kuwa ni muhimu wasiikose taarifa ya habari maana wanapenda kufahamu nini kimejiri kwa siku na hasa kufahamu Mheshimiwa Rais amefanya nini kwa siku husika katika kupambana na maovu katika nchi yetu na ni hatua gani anazozichukua ili kuwanusuru Watanzania wasiendelee kukandamizwa na mafisadi na wala rushwa.

Kitendo chake cha kupambana na maovu kama hayo kinamfanya Rais Magufuli akubalike kwa Watanzania wengi. Kinanchotakiwa ni kuwa asilegeze kamba. Ajue Watanzania wengi wako nyuma yake kwani mafanikio atakayoyapata ni mafanikio ya Watanzania wote.

Kusema kweli inavutia sana unaposikia baaadhi ya watu wa hali ya kawaida na walio wengi vijijini na mijini wanasema: “Sasa Watanzania tumepata kiongozi aliye na nia ya kutuondoa katika dimbwi la umasikini”. Nisemeje juu ya hali kama hiyo?

Kwa mimi ni ishara tosha kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli pamoa na msadizi wake Waziri Mkuu Majaliwa Kassim. Ni matarajio yetu kuwa hata Baraza la Mawaziri litakuwa mstari wa mbele katika kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi na kupiga vita uharibifu wa misitu ya asili na mazingira.

Rais ameonyesha njia na nia ya kweli kwamba uchafu sasa basi.  Iweje tuendelee kuukumbatia uchafu katika sehemu zetu za kazi na mahali tunapoishi? Vilevile, suala la uchafuzi na uharibifu wa misitu kutokana na matumizi makubwa ya mkaa kwa kupikia na shughuli nyingi za kibiashara, ni changamoto kubwa ambayo inahitaji msukumo na utashi mkubwa kisiasa (political will) na kijamii (social responsibility).

Nichukue fursa hii kwa heshima na taadhima, kumwomba Mheshimiwa Rais, alitupie jicho la karibu sana suala la matumizi ya mkaa katika nyumba zetu kama chanzo cha nishati ya kupikia.

 

>> ITAENDELEA

934 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons