Rais Magufuli naomba uniazime sikio

Wiki iliyopita nimesikia mambo mengi, ila mawili yaliniingia akilini. La kwanza ni hotuba ya Rais John Pombe Magufuli akiadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo kwa mara ya kwanza yameadhimishwa upande wa Tanganyika. 

Hii ni historia ya pekee, ambayo haitakaa ifutike. Watanganyika wamethibitisha kwa dhati kuwa wanathamini kilichotokea Zanzibar Januari 12, 1964.

Sitanii, katika maadhimisho haya yaliyofanyika katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Rais Magufuli alizungumza na kuchambua ahadi alizotoa wakati wa kampeni na jinsi Serikali ilivyotekeleza hadi sasa. Amezungumzia ununuzi wa ndege, ambapo kwa sasa tayari ndege mbili mpya zinafanya biashara hapa nchini na mashirika kama Fastjet na Precision yameanza kuisoma namba.

Sishabikii mashirika haya kukosa wateja, ila kiuhalisia bei waliyokuwa wanatutoza sisi wateja, ilikuwa inasikitisha. Fastjet hawakuwa wakiona aibu kukutoza hadi dola 700 kwa tiketi ya Dar es Salaam-Mwanza, na ukichelewa sekunde nne katika muda wanaopanga wao, fedha zote hizo zinapotea bila kurejeshwa. Precision wao wanafuata taratibu za kuheshimu wateja, ila nao bei zao ni tishio.

Januari 11, 2017 nikitokea Bukoba kuja Dar nilishtuka. Kwa mara ya kwanza nimeona ndege ya Bombardier ikipakia abiria karibu 60 hivi, wote wakitoka Bukoba kuja Dar. Kipindi cha nyuma usingeona hili. Bei ilifikia Sh 980,000 kwa safari ya ndege ya Dar-Bukoba-Dar, ila kwa sasa imeshuka kwa zaidi ya nusu kwani hadi Sh 499,000 unapata tiketi ya njia hiyo.

Sitanii, katika hili la usafiri wa anga, wakati Rais Magufuli anazungumza pale Shinyanga nilifarijika. Ametaja kuwa ndege nyingine nne zipo njiani zinakuja Tanzania, ikiwamo Boeing 787-400 Dreamliner inayochukua abiria 262. Hongera katika hili Mheshimiwa Rais. Hata hivyo, usiwapuuze wanaoomba uwapatie wananchi maji pia. Maji ni uhai. Si Watanzania wote wanaopanda ndege.

Nimefurahishwa na hoja kwamba meli zitanunuliwa katika maziwa ya Victoria na Nyasa, ingawa zipo taarifa kuwa mv Victoria inatafutiwa injini na huenda hiyo ndiyo ikawa meli mpya. Ni kwa heshima kuu na taadhima nawiwa kusema ukweli, kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi ya kupigiwa mfano katika kujenga miundombinu na kununua vyombo vya usafiri.

Hata hivyo, sitanii, napata tabu kidogo. Ni katika hatua hii nimelazimika kumwomba Rais Magufuli aniazime sikio hata kama huenda ninayotaka kusema hayapendi. Akiwa Shinyanga, amesema kuna magazeti mawili yanachochea na siku zao zinahesabika. Nimejaribu kufuatilia, unaoitwa uchochezi ni habari zilizochapishwa na magazeti mawili – moja likiwa la Mtanzania juu ya baa la njaa linaloikabili nchi.

Gazeti jingine sijalifahamu vyema, maana habari hii imeandikwa na magazeti mengi, juu ya suala la umeme. Kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amempotosha Rais Magufuli katika suala la kuongezwa bei za umeme hadi Rais akamtumbua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Feleschemi Mramba, siyo siri.

Sitaki kuamini iwapo suala hili lililowasilishwa hadi Benki ya Dunia, iwapo halikupata kujadiliwa katika Baraza la Mawaziri. Ikiwa lilijadiliwa na pengine Serikali ikakataa ushauri wa kuongeza bei ya umeme, sina uhakika kama Prof. Muhongo alipeleka mrejesho Tanesco kuwataka wasitishe ombi lao kwa Ewura. Inawezekana pia kuwa yaliyowakuta Tanesco alilenga yawakute Ewura ila kwa dua la kuku.

Sitanii, Mheshimiwa Magufuli unafanya kazi nzuri. Yanayokwaza Watanzania ni kauli unazotoa kama utani. Mfano, kusema sikuahidi tetemeko katika kampeni. Kagera nanyi mmezidi, ukimwi, ninyi…, tetemeko ninyi, mto ngono, kata ya Katerero… Wakati wewe unafanya utani, wengine wanajua hutanii. Neno pole halirejeshi thamani ya aliyefariki, ila linatarajiwa kutoka kwa wafariji.

Mwisho, naomba kuhitimisha kwa jambo moja. Baadhi ya taarifa ukiletewa juu ya magazeti, zipime na uzichuje. Suala la kudhani magazeti yapo kuihujumu Serikali yako yanapokutahadharisha kuwa nchi ina njaa au Prof. Muhongo amekwambia uongo, lifikirie mara mbili kabla ya hizo siku zinazohesabika unazosema hazijaisha.

Mimi nikiwa Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ninaposikia unasema magazeti mawili siku zinahesabika, tena bila kutaja majina, inawezekana ni hili langu la JAMHURI. Shida si kufuta magazeti, bali kuwakosesha huduma wananchi na watumishi walioajiriwa na magazeti husika. Mheshimiwa Rais chonde chonde, hili la magazeti kuhesabiwa siku naomba ulifikirie mara mbili.

Baraza Katoliki la Maaskofu Tanzania (TEC), kupitia Rais wa TEC, Askofu wa Jimbo la Iringa, Tarcisius J. M. Ngalalekumtwa, ametoa waraka wa kuyaomba makanisa nchini kuombea mvua. Katika waraka huo kwa makanisa nchini, amesema bayana kuwa kuna tishio la njaa, hivyo akataka hadi waumini kufunga na kuimba. 

Mungu ibariki Tanzania.