Rais Magufuli umeokoa elimu

Jumamosi Aprili 15, 2017 imekuwa ya burudani kwangu. Nimeburudishwa na hotuba aliyoitoa Rais John Magufuli wakati akizindua mabweni ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Kwanza ameniburudisha kwa kujenga mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 kwa gharama ya Sh bilioni 10. Hii ina maana majengo 20, kila jengo limejengwa kwa gharama ya Sh milioni 500.

Hakika, gharama iliyotumika kujenga majengo haya na thamani halisi ya majengo ukiyaangalia, huwezi kuamini. Hii imethitisha kuwa kwa muda mrefu wakandarasi wametuumiza katika sekta hii ya ujenzi. Wametuumiza si kwa sababu nyingine, bali kwa kutowaamini wakandarasi wazawa. Wageni wameitwa, wakachuma.

Sitanii, nimefurahi mno kusikia kauli ya Rais Magufuli akisema nchi yetu inapaswa kujenga dhana ya kuamini wakandarasi wazawa. Nimefurahi kuwa sasa Serikali imeanza kuzungumza lugha ya kuamini watu wetu. Haijapata kuniingia akilini na miaka yote nimekuwa siridhiki kutokana na kasumba ovu iliyojengeka miongoni mwa Watanzania, kuwa Watanzania hawawezi.

Dhana hii imehubiriwa kitambo. Kila tukishindwa kesi katika mahakama za kimataifa tunaambiwa wanasheria wetu hawawezi. Wanasiasa wanaingia mikataba inayonuka rushwa, lakini baadaye wanasema wanasheria wetu hawana ujuzi. Mzawa akifungua kampuni kupata mkopo ni mbinde. Mtu anakuwa hajaanza biashara anatozwa kodi.

Niombe Serikali yetu iliangalie hili. Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) naomba wapewe fursa ya kufanya biashara kabla hawajapangiwa kazi ya kutoza kodi. Walio wengi wanawachukulia wafanyabiashara kama wezi. Mfanyabiashara akifika mbele yao, badala ya kumwongoza, kila kauli anayoitoa mfanyabiashara wanaitafsiri katika kodi.

Utaratibu huu utaua mitaji. Kwa mfano, huwezi kumchukulia mfanyabiashara mwenye mtaji wa Sh milioni 200 anayeuza mbao, ukamkadiria kodi sawa na mchuuzi anayeuza mbao akiwa na mtaji wa Sh milioni 5. Hii inawafanya wenye vioski wasijitokeze kulipa kodi stahiki. Unakuta mtu ana uwezo wa kulipa Sh 50,000 kama kodi kutokana na biashara yake, lakini anakadriwa 520,000. Unategemea nini?

Tukiendelea na mtazamo huu, hakika hata hii sera ya viwanda inayozungumzwa tutaisoma namba. Tutabaki kuwa watazamaji na kufanikisha mipango ya wageni kutoka nchi za nje. Yatupasa kufanya juhudi za makusudi kuwezesha wazawa kumiliki viwanda na si kuwachimbia mashimo na kuwawekea vigingi.

Sitanii, naombe radhi kwa kutoa mifano hai, ambayo naitoa kwa nia njema si kwa nia ya kubagua mtu yeyote kwa utaifa, vinasaba, rangi wala dini yake. Hapa kwetu nchini Watanzania tunacheleweshana katika maendeleo. Ikitokea akaenda benki Mchina au Mhindi kuomba mkopo, ikimchukua muda ni siku tatu mkopo utakuwa kwenye akaunti.

Akianzisha kampuni Mhindi au Mchina, hakuna anayeuliza hata chembe ya swali. Ngonja Balile na Jackton Manyerere wakusanye nguvu waseme wanaanzisha JAMHURI, utashangaa. Hapo yataanza maneno ya kufa mtu. Kampuni yao itamilikishwa kwa wafanyabiashara wenye asilia ya India, wataambiwa wametangulizwa mwenye mali ni mwanasiasa fulani, na mengine mengi. Ni masikitiko. Tuaminiane Watanzania.

Sitanii, kabla sijaenda kwenye mzizi wa makala ya leo, niweke ‘baashraf’ kidogo kwa kugusia usalama wa Taifa letu. Niseme kwa ufupi tu, kuwa mchezo wetu ni mauti yetu. Wiki iliyopita wameuawa askari wanane pale Mkuranga. Haya ni masikitiko makubwa.

Nimesikia mauaji ya viogozi wa kisiasa Ikwiriri Rufiji. Habari yetu kuu katika gazeti la leo inaeleza chimbuko la mgogoro huo unaoendeleza mauaji. Nafahamu kwa sababu ya ukakasi wa tukio lenyewe, wahusika wanaitwa majambazi. Uhalisia wakubwa hawa wanachofanya ni zaidi ya ujambazi.

Sina mamlaka ya kuwaita magaidi, ila watendayo hayana tofauti na magaidi. Najiuliza polisi wanamiliki fedha kiasi gani hadi wavamiwe na majambazi? Kwa kawaida majambazi hufika kwenye nyumba yenye ukwasi wapate kupora fedha na kujikimu maisha yao.Leo maaskari wanauawa? Inawezekana baadhi ya watu wakasema ni kwa kutaka kupata bunduki. Ndiyo, ila ili wazifanyie nini? Naamini tulipofika inatupasa kufanya utafiti wa kina. Wakati tunaendeleza mapambano ya kiserikali, ni vyema tukaanzisha uchunguzi wa kijamii.

Kinachotokea Ukanda wa Kusini katika hii mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara hakikubaliki duniani na mbinguni. Amani yetu ni kipaumbele. Tujilinde, tuzuie wahalifu na tupambane na waovu. Wakati umefika kwa nchi yetu kushirikiana. Tusiruhusu nchi yetu kupoteza tunu ya amani.

Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema: ‘“Rais Magufuli umeokoa elimu”. Katika uzinduzi wa mabweni hayo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli ameagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) iache kupangia wanafunzi vyuo vya kwenda. Rais Magufuli amesema hii ina mkono wa mtu.

Amefafanua kuwa wapo watu wanaofaidika na mfumo huo. Amesema mfumo huu unawakosema wanafunzi uhuru wa kuchagua vyuo qavitakavyo. Binafsi nimekuwa nikiishangaa nchi yetu. Duniani kote elimu ya juu inasimamiwa na Baraza la chuo.

Mamlaka ya elimu ya juu inafanya kazi moja tu, ya kudhibiti ubora wa mitaala. Mimi nimefata fursa ya kusoma Shahada ya Uzamili (MSc) katika Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza. Sikupeleka maombi yangu kwa Mamlaka ya Vyuo Vikuu nchini  Uingereza ndiyo inipangie chuo nikitakacho.

Kidunia, inafahamika kuwa sifa za mtu kuingia chuo kikuu ni ‘Principle Pass’ mbili. Kwa kidato cha sita Principle Pass ni A, B, C, D na E. Ukipata S, inaitwa subsidiary. Kwa maana hiyo hadi leo duniani kote, mtu aliyepata ‘Principle Pass’ za E, mbili anaruhusiwa kuingia kwenye chuo.

Hapo ndipo Rais Magufuli naomba usimamie vyema. Agizo ulilotoa liendane na kurejesha mamlaka kamili kwa vyuo. Mabaraza ya Vyuo Vikuu yana nguvu kubwa. Ndiyo yenye kustahili kufanya udahili kama ulivyosema. Wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina uwezo wa kufikisha wanafunzi 22,000 au Chuo Kikuu cha Dodoma kikiwa na uwezo wa wanafunzi unakuta wanapangiwa wanafunzi nusu ya uwezo wake.

Binafsi naamini hili si sahihi. Vyuo vikuu viachwe viwe na mipango yake ya kuimarisha miundombinu. Viwe na haki ya kuajiri wahadhiri wengi kadri ya mahitaji na kwa kufanya hivyo vitafikia uwezo wa juu. Viwe na mamlaka ya kudahili wanafunzi kadri ya uwezo wake.

Elimu ya juu si sawa na sekondari. TCU wamejipa jukumu la Baraza la Mitihani Tanzania. Ni kawaida kwa wanafunzi wanapohitimu selimu ya msingi kuchaguliwa kuingia elimu sekondari, lakini si vyuo. Vyuo ni taaluma. Mwanafunzi anakuwa na uhitaji wake.

Ni kwa bahati mbaya chini ya udahili wa pamoja, TCU imelazimisha watu waliotaka kusoma udaktari wa binadamu kusomea mazingira, na waliotaka kuwa waandishi wa habari wakapelekwa kuwa wahasibu au kozi ambayo hawakuomba. Hili kamwe halikubaliki.

Sitanii, kama alivyosema Rais Magufuli kwamba tuwaache wanafunzi wawe na uhuru wa kuchagua vyuo wavipendavyo na vyuo viwe na fursa ya kuvutia wanafunzi kwa kujenga mazingira bora ya kitaaluma na kijamii (mabweni) turuhusu jamii yetu ifanye hivyo.

Iweje Tanzania sisi tujifanye kuwa kisiwa? Duniani kote nchi zinaweka viwango. Kwa mfano Chuo Kikuu Huria kilikuwa kinatoa elimu msingi (foundation courses) kwa taaluma mbalimbali kwa nia ya kuwajenga wahusika waliokosa sifa za kuingia vyuo vikuu kama wahitimu wa kidato cha sita.

Utaratibu huu ulikuwapo tangu enzi ukifahamika kama ‘mature entry’. Ni kwa bahati mbaya Waziri wa sasa mwenye dhamana na masuala ya elimu, Prof. Joyce Ndalichako, amevuruga utaratibu huu. Amefuta ‘foundation courses’. Watu wanaoomba kujiunga na Chuo Kikuu Huria wanachaguliwa hata watoto wasio na uwezo wa kusoma bila usaidizi wa walimu.

Sitanii, napenda kuhitimisha makala yangu na nukuu ya Rais (mstaafu), Benjamin Mkapa. Wakati Prof. Ndalichako alipoanza mageuzi katika elimu. Akaongeza viwango vya ufaulu kuliko uhalisia, Mkapa alisema: “Ni hatari kuacha elimu yetu mikononi mwa mtu mmoja.”

Kauli ya Rais Mkapa ilisheheni mantiki kubwa. Taifa letu limegeuzwa gunia la mazoezi. Leo chini ya utaratibu wa Prof. Ndalichako mwanafunzi aliyepata A, E, E, hawezi kudahiliwa chuo kikuu kwa maana yeye haitambui E kama ‘principle pass’. Amesema mtu kudahiliwa chuo kikuu ni lazima angalau apate D mbili kidato cha VI.

Kwa mkondo huu, ni wazi nchi inaingizwa chaka. Wazazi wengi wamepeleka wanafunzi wao Kenya na Uganda kwa kuona sintofahamu inayoendelea katika elimu yetu. Kwa Rais Magufuli kurejesha mamlaka ya udahili katika vyuo vyenyewe, hakika sasa tutashuhudia ushindani wa kweli na itatolewa elimu ya uhakika. 

Waziri alikosea kupitisha mfumo unaohujumu elimu na sasa tuseme basi. Hongera Rais Magufuli.

1059 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons