Rais Samia analiunganisha tena taifa

Na Deodatus Balile

Leo naomba nianze makala yangu kwa kumnukuu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, katika kauli aliyoitoa baada ya tukio la Septemba 7, 2017 alipopigwa risasi 16, na baadaye akawa kwenye matibabu nje ya nchi. Kauli hii tangu wakati huo, Lissu ameitoa mara nyingi akisema: “The President must be a comforter in Chief (Rais anapaswa kuwa mfariji mkuu).”

Sitanii, nimeanza na kauli hii ya Lissu kutokana na matukio makubwa niliyoshuhudia akifanya Rais Samia Suluhu Hassan kwa nia ya kuliunganisha tena taifa letu. Tangu Rais Samia ameingia madarakani Machi 19, 2021, siwezi kuorodhesha yote aliyoyatenda kuponya vidonda vya mpasuko yakatosha katika ukurasa huu, ila nigusie machache.

Mara nyingi Rais Samia amesema bila uficho kuwa Tanzania ni yetu sote, na atahakikisha kila Mtanzania anashiriki katika kujenga taifa imara. Rais amekutana na makundi mengi kuliko wakati wowote. Amekutana na wanasiasa akiwamo Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (ikiwamo kumfutia kesi ya ugaidi), wadau wa vyama vya siasa, taasisi zisizo za kiserikali na wengine wengi.

Rais Samia miongoni mwa wengi aliokutana nao, pia hakusita kukubali mwaliko wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau kushiriki siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD) Mei 3, 2022 ambayo kwa Afrika siku hii imesherehekewa katika Jiji la Arusha, Tanzania. Nikiri, nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na hadi leo salamu ninazopata zinaonyesha siku hii imefana na nchi za Afrika wengi wanatamani kurejea Tanzania.

Wiki iliyopita ameshiriki maadhimisho ya miaka 10 ya Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yaliyofanyika Dar es Salaam. Amekutana uso kwa uso na Onesmo ole Ngurumwa ambaye utawala uliotangulia ulikuwa umemfungia akaunti zote na hati yake ya kusafiria ukaiweka rehani kwa ‘kosa’ la kutetea haki za binadamu.

Sitanii, sekta binafsi hadi sasa imeanza kupata uhai. Hoteli nyingi zilifungwa kwa kukosa wateja. Tulikuwa tunaambiwa kuwa 500 tutaacha kuiita jero. Bila kufahamu kuwa hoteli, gereji na shughuli nyingi za binafsi ndizo zimeajiri Watanzania milioni 24, ilhali serikali imeajiri wastani wa Watanzania 500,000 tu, tulizisonga na kuzikaba koo. Kodi ikaota mbawa.

Naomba niseme hili, ingawa halifurahishi katika masikio ya baadhi ya watu. Nchi yetu kwa mara ya kwanza kimyakimya kabla ya Rais Samia ilionja joto la uteuzi wa kidini na ukabila katika utawala uliopita. Kuna kabila moja ilikuwa kila aliyehitimu kuanzia kidato cha nne anatakiwa apeleke ‘CV’ yake, afikiriwe katika uteuzi. Tulianza kuzoea majina yenye lafudhi fulani katika kila uteuzi na baadhi ya kanda na mikoa zikawekwa kando.

Nafahamu baadhi ya watu hawafuatilii kwa ukaribu. Hebu pekua uteuzi hata katika ngazi ya Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Mwalimu Nyerere na wachache wengine waliofuatia. Kila uteuzi ukikamilika ilikuwa kila mkoa ama una waziri au naibu waziri. Zanzibar na Tanganyika (Tanzania Bara) ziliwakilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa jicho lisilotia shaka.

Sitanii, kama tuna kumbukumbu, hivi karibuni tumeshuhudia Baraza la Mawaziri ambalo Zanzibar hakuwapo waziri kamili hata mmoja. Mikoa kama Kilimanjaro na Arusha, waliwekwa kando kabisa. Naona Rais Samia ameamua kuyafuta haya. Utamaduni huo wa kusambaza uongozi nchi nzima umeiimarisha Tanzania kuliko nchi nyingine yoyote.

Ukiona nchi inafika mahala inapata Waziri Mkuu kutoka Mpanda, Lindi, Musoma au Makamu wa Rais anatoka Kigoma kwa watani zangu wala mihogo, basi ujue hiyo ndiyo kusuka mkeka wa umoja wa kitaifa. Zipo nchi kama Falme za Kiarabu wanayo kanuni isiyoandikwa, Rais anatoka katika Kisiwa cha Dubai. Viko visiwa saba, lakini urithi wa kifalme kiti kiko Dubai.

Sitanii, ilifika mahala wafanyakazi wa sekta binafsi wakaonekana kama raia daraja la 6. Usawa mbele ya sheria ukatoweka. Mtu mmoja unakutana naye anakuuliza: “Utanifanya nini?” Nani anamjua nani, badala ya nani anajua nini ikatawala (technical know-who, instead of technical know-how). Kwa sasa Rais anahubiri mshikamano, ushirikishaji wa sekta binafsi, taasisi mbalimbali, anaheshimu mashirika na viongozi wa dini.

Nafahamu ukurasa huu unapungua hapa nilipofikia. Ameongeza mishahara kwa mara ya kwanza baada ya miaka 6. Wafanyakazi wamepandishwa madaraja. Ameunda Kikosi Kazi kinachochakata hali ya siasa nchini, kwa nia ya kurejesha maridhiano. Ameridhia kukutana na Chadema Ikulu wiki hii kwa mujibu wa Mbowe. Ameweka lengo la kuzalisha umeme megawati 6,000 ifikapo mwaka 2025.

Sitanii, ukiniuliza binafsi nitasema tushindwe sisi. Rais anaweka mazingira wezeshi, ikiwamo kubadili sheria. Ni wajibu wetu sasa Watanzania kufanya kazi kwa nguvu na kutumia fursa hizi zilizojitokeza kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia zetu na kupitia uchumi ulioimarika, tutalipa kodi, ajira zitaongezeka na huduma za jamii kama barabara, maji, elimu, usafiri wa anga, reli na miundombinu ya msingi itajengwa kwa kasi, kwa sababu nchi itakuwa na fedha. Hongera Rais Samia. Tukutane wiki ijayo katika safu hii.