Rais Samia LNG ni dili, tusaini

Na Deodatus Balile

Wiki iliyopita zimekuwapo taarifa za Tanzania kuwa katika mchakato wa kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha gesi ya LNG mkoani Lindi. Mkataba wenyewe ni wa dola bilioni 40, karibu Sh trilioni 70 za Tanzania. 

Leo safu hii ni fupi, hivyo nakwenda moja kwa moja kwenye hoja. Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan nasema msukume Waziri wako wa Nishati, January Makamba, asaini mkataba huu haraka.

Sitanii, mkataba huu umekuwa na maneno mengi miaka mingi. Ni hadithi tulizozisikia hadi zinachusha masikioni. Kampuni ya Shell kwa kushirikiana na Norway na wabia wengine walianza mchakato huu karibu miaka 20 iliyopita na wanaelekea kukata tamaa. 

Ilifika mahala wakaambiwa kuwa mradi huu wausahau. Nimesema mkataba huu usainiwe haraka kwa sababu moja ya msingi ninayoitaja hapa chini.

Marekani kwa kushirikiana na nchi za Ulaya wana mpango wa kufunga utegemezi wa gesi kutoka Urusi baada ya vita ya Ukraine. Urusi inatoa asilimia 40 ya gesi kwa Bara la Ulaya kwa sasa. Nchi hizi zinazoelekea majira ya baridi, gesi kwao si anasa, bali ni hitaji la msingi la binadamu. Gesi inatumika kuchemsha maji yanayotumika kuzalisha joto katika nyumba zao kupitia heater panels.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, wiki iliyopita lisafiri hadi nchini Senegal na Afrika Kusini kutafuta jinsi ya kupata gesi kwa haraka. Hapa kwetu Tanzania hata kama itachukua miaka mitano kuanzia sasa, naamini tukiingia sokoni na lengo la dunia la kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 dunia ianze kutumia gesi badala ya mafuta, tutakuwa tumelamba bingo.

Sitanii, huu ni mradi mkubwa unaohitaji kutengewa hata Wizara Maalumu. Si vibaya tukiwa na Wizara ya Gesi, kwani tukianza kutumia gesi katika magari, kwenye nyumba zetu na kuuza kwa majirani zetu, itakuwa ni sekta kubwa isiyopaswa kuwa idara ndani ya Wizara ya Nishati. 

Kwa uwekezaji huu wa Sh trilioni 70, Tanzania ina uhakika wa kupata kodi mbalimbali zisizopungua Sh trilioni 10 kila mwaka kutokana na gesi. Ni kwa mantiki hiyo, nasema tusisite. Tusaini mkataba huu mara moja, na tusipousaini, vizazi  vijavyo vitatulaani. Mungu ibariki Tanzania.