Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Hamid Njovu akiwasilisha taarifa ya msitu wa Malangali uliopo Sumbawanga Mjini Kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa agizo la kukamatwa kwa waliokiuka amri ya mahakama na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye msitu wa Malangali Mjini Sumbawanga

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa agizo la kukamatwa kwa waliokiuka amri ya mahakama na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye msitu wa Malangali Mjini Sumbawanga katika Mkutano wa hadhara. 

 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameagiza kuwasaka na kuwakamata wananchi wote waliokiuka amri ya mahakama ya kutoutumia msitu wa hifadhi ya Malangali kwaajili ya matumizi ya kibinadamu.

Amesema kuwa pamoja na kukamtwa, wananchi hao wasimamiwe kuhakikisha kuwa wanapanda miti maeneo ambayo wameyaharibu na kusisitiza kusakwa kwa wale wote waaofanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo vya maji huku akitaja bonde la mto lwiche.

“Mpite shamba kwa shamba, kamateni watu wote ambao wamevamia kule, ule msitu uache kama ulivyo, vyanzo vyetu vya maji vitakauka, Mkurugenzi fanya msako wa bonde lote hilo kwa wale wote ambao wameanza kufyeka na kulima, kamata. DC simamia hili, tunataka kukomesha uharibifu wa mazingira wa aina yoyote ile,” Alisisitiza.

Ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara alioufanya baada ya kutembelea msitu huo wa malangali uliopo kata ya Malangali, Wlayani Sumbawanga na kujione namna wananchi hao walivyoharibu msitu huo uliojaa miti ya miombo ambayo inakatwa na kugeuzwa mkaa.

Msitu huo wa Malangali ulianzishwa rasmi mwaka 1986 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa huo Mh. Tumainieli Kihwelu wenye eneo la ekari 278 kwa lengo la kupunguza mmomonyoko na vimbunga.

Wakati akisoma taarifa ya Msitu huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbwanga Hamid Njovu amesema kuwa baada ya miaka 29 wananchi waliwasilisha malalamiko ya kupokonywa ardhi na kufanywa msitu shauri lililofikishwa mahakamani na kuamuliwa wananchi hao kulipwa fidia huku hukumu ya kesi hiyo ikisitisha shughuli zote za kibinadamu kutofanyika katika msitu huo.

“Tarehe 28/4/2016 hukumu ilitolea na kuamuliwa Manispaa ya Sumbawanga kulipa fidia huku Hukumu hiyo ikisitisha shughuli zote za kibinadamu ndani ya msitu lakini bado wananchi hao walirudi kufyeka miti na kulima na tarehe 13/11/2017 Manispaa ilitoa maelekezo kwa wananchi kutoutumia msitu kwa shughuli za kibinadamu,”Alimalizia.

Mmoja wa wadau wa Mazingira Mzee Zeno Nkoswe amesema kuwa usalama wa mji wa Malangali unatokana na msitu huo na kwamba endapo utaendelea kuharibiwa mji huo utafunikwa na mmomonyoko wa udongo.

 

IMETOLEWA NA 

OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA 

By Jamhuri