Mbunge wa Chalinze, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete ameujia juu uongozi wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa mazingira Chalinze (CHALIWASA) kwa kushindwa kusambaza maji.

Katika kikao cha Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze kilichofanyika katika halmashauri hiyo, mbunge huyo amesema Mamlaka hiyo imeshindwa kusambaza maji huku wakiwa na visingizio visivyo eleweka.

Amesema mradi huo ulitakiwa kukabidhiwa mwezi huu jimboni hapo, lakini unasuasua bila ya kuwapo kwa sababu za msingi zilizoukwamisha.

Amesema tatizo la ukosefu wa maji, bado ni kubwa hivyo inaonekana uongozi wa Mamlaka hiyo umeshindwa kupata njia mwafaka ya kulimaliza tatizo hilo.

“Mpaka sasa hakuna matenki yaliyojengwa na mabomba hayajafukiwa, hivyo ni ndoto za Ali Nacha mradi huo kukamilika mwezi huu,” amesema Ridhiwani.

Amesema Waziri wa Maji anapaswa kulieleza Bunge na wananchi wa Chalinze kwa ujumla zilikoenda fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo.

“Kama mradi huu utaendelea kusuasua, wananchi na wawekezaji wanaokimbilia kuwekeza Chalinze watashindwa kutimiza malengo yao na kuendelea kuishi kwenye adha hii inayowapa wakati mgumu,” amesema Ridhiwani.

Kwa upande wa madiwani, wamesema kama uongozi wa halmashauri umeshindwa kutekeleza majukumu yake ni bora wakawapisha watu wengine wenye uwezo wa kufanya kazi.

Diwani wa Lugoba, Rehema Mwene,aliiomba Serikali imsimamie mjenzi wa mabomba na matenki amalize kazi hiyo kwa muda mwafaka kuliko kumuacha afanye anavyotaka.

Amesema kuna hatari kubwa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya Bwilingu na Chalinze, ambao wanatumia maji yasiyo safi wala salama kukumbwa na magonjwa ya kuambukiza.

Amesema mradi huo wa maji ni kama hauna faida kutokana na wananchi kukosa maji kwa kipindi kirefu, kiasi cha kufikia hatua ya  kukata tamaa.

Diwani wa Chalinze mjini, Hussein Hading’oka, alionesha wasiwasi wake hasa katika kipindi kinachokuja cha mvua za masika na kuongeza kwamba mara kadhaa viongozi wa CHALIWASA wamekuwa wakisema kipindi cha mvua mitambo yao huwa inasumbuliwa na tope na kushindwa kufanya kazi.

Alimshangaa Meneja wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Christer Mchomba, kushindwa kuhudhuria kikao hicho kama alivyotakiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, Edes Lukoa.

“Meneja alitakiwa kwa ajili ya kuwapatia madiwani hao maelezo ya kina kuhusiana na tatizo sugu la maji linalowakabili wananchi wa Halmashauri hiyo kwa miaka mingi sasa,” amesema Husein.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Edes Lukoa, amesema Halmashauri imetenga bajeti kwa ajili ya maeneo ambayo hayafikiwi na CHALIWASA, hivyo Mamlaka hiyo lazima iwe na mpango wake.

Hivi karibuni Waziri wa Mazingira, Januari Makamba, alipofanya ziara ndani ya Halmashauri hiyo, alifika eneo la chanzo cha maji Wami na kutoa maagizo kwa wilaya na mkoa kutatua matatizo ya uvamizi wa vyanzo vya maji.

Alimuagiza  Mkuu wa Wilaya, Alhaj Hemed Mwanga, kuhakikisha wanafanya jitihada za kukutana na uongozi wa Mkoa wa Morogoro kuzungumzia uvamizi unaofanywa na wakulima kutoka wa mkoa huo kando kando ya mto Wami.

By Jamhuri