Ripoti ya Kamati ya Pili ya Madini

Muhtasari wa ripoti ya kamati maalum ya kuchunguza masuala ya kisheria na kuichumi kuhusiana na mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi.

Utangulizi
Mheshimiwa Rais,
Kama ambavyo Watanzania watakumbuka tarehe 10 April 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk John Magufuli aliteua Kamati Maalum ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya nchi yakiwemo makontena 277 yaliyozuiliwa na serikali katika bandari ya Dar es Salaam.

Wajumbe wa Kamati ni;
1. Prof. Nehemiah Eliakim Osoro (Mwenyekiti)
2. Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara
3. Dr. Oswald Joseph Mashindano
4 Bw. Gabriel Pascal Malata
5. Bw. Casmir Sumba Kyuki
6. Bi. Butamo Kasuka Philip
7. Bw. Usaje Benard Asubisye
8. Bw. Andrew Wilson Massawe

Mheshimiwa Rais,
Katika kutekeleza uchunguzi huo, kamati maalum iliongozwa na hadidu za rejea zifuatazo;

1. Kufanya tathmini ya mchakato mzima wa usafirishajiwa makinikia na kujiridhisha iwapo utaratibu huo unafanyika kwa mujibu wa Mikataba iliyoingiwa baina ya Serikali na Makampuni ya uchimbaji wa madini “Mining Development Agreements” (MDAs) na “Special Mining Licence” (SPL) na kwamba taratibu hizo zinafuatwa kikamilifu. Pamoja na masuala mengine ambayo Kamati itaona ni muhimu kuyafuatilia, Kamati ijiridhishe kuhusu mrejesho wa taarifa za uchenjuaji wa makinikia kutoka nje ya nchi kwa mamlaka za serikali.
2. Kupitia Mikataba husika na kushauri endapo inazingatia kikamilifu maslahi ya nchi ama inahitaji kuboreshwa. Maeneo yenye mapungufu na mapendekezo ya maboresho yabainishwe wazi.
3. Kufanya tathmini ya mfumo mzima wa udhibiti kuhusu biashara ya makinikia kutoka kuchimbwa, kusafirishwa, kuyeyushwa na kuuzwa kwa madini yanayopatikana katika makinikia hayo kwa lengo la kubainisha ufanisi wa mfumo huo katika kuzuia upotevu wa mapato ya serikali yanayotokana na usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.
4. Kupitia taarifa ya Kamati ya Wataalam ya kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo kwenye makontena yenye makinikia ya dhahabu yaliyokusudiwa usafirishwa nje ya nchi, iliyoteuliwa tarehe 29 Machi 2017, hususan, kuhusu aina, kiasi, viwango vya ubora na thamani za madini yaliyomo kwenye makinikia hayo na kubainisha kama Serikali inapata mapato stahiki ya kikodi kutokana na biashara hiyo kwa mujibu wa mikataba na sheria za nchi.
5. Kubaini idadi ya makontena yenye makinikia yaliyosafirishwa kutoka katika migodi ya dhahabu kuanzia mwaka 1998 hadi sasa; na kwa kuzingatia taarifa ya Kamati ya Wataalam iliyotajwa katika aya ya 4, Kamati ifanye makadirio ya kiasi cha mapato ambacho Serikali ingestahili kupata na kulinganisha na kiasi halisi cha mapato kilichopatikana katika kipindi hicho.
6. Kubaini na kujiridhisha kama kuna sababu zozote za msingi za kiuchumi na kiufundi zinazokwamisha uanzishwaji wa kiwanda cha kuyeyusha makinikia nchini na kuishauri Serikali ipasavyo. Taarifa hiyo ibainishe;

i. Nini kinahitajika ili teknolojia ya kuchenjua mchanga kuwepo hapa nchini.
ii. Ni gharama kiasi gani zinahitajika ili kuanza uchenjuaji wa makininkia hapa nchini.
iii. Inachukua muda gani kukamilisha ujenzi wa mtambo husika hadi kuanza kufanya kazi.
iv. Nchi ina uwezo au mapungufu gani katika kulitekeleza hilo hasa katika upande wa wataalam na uwekezaji.
v. Aidha, Kamati ibainishe na kujiridhisha kuhusu hatua zilizochukuliwa na kampuni za uchimbaji dhahabu nchini katika kutekeleza sera na sheria za nchi kuhusu uanzishwaji wa kiwanda cha kuchenjua makinikia.
7. Kuchunguza na kulinganisha taarifa za uchunguzi wa kimaabara wa makinikia zinazotolewa na kampuni ya SGS Tanzania Superintendence Company LTD (maabara binafsi inayopima sampuli za makinikia ya kampuni za madini) na Wakala wa Uchungzi wa Madini Tanzania (Tanzania Mineral Audit Agency –TMAA). Aidha, Kamati ibainishe ushiriki na majukumu ya kampuni nyingine ikiwamo SGS kuhusu makinikia.
8. Kubainisha uwepo wa mikataba na maudhui yake kati ya kampuni za uchimbaji madini ya dhahabu Tanzania na kampuni za uchenjuaji wa makinikia yanayosafirishwa ili kijiridhisha kuhusu uhalali wa biashara hiyo na kama kodi na tozo mbalimbali za serikali zililipwa ipasavyo.
9. Kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na mchakato mzima wa usafirishaji wa makinikia, na kutoa mapendekezo ya kuboresha taratibu husika kwa siku zijazo kwa maslahi ya nchi.
10. Kufanya kazi kwa karibu na wataalamu katika sekta ya madini waliobobea katika taaluma zao wakiwemo Wanajiolojia, Wahandisi wa uchenjuaji (Metallurgists), Wakemia (Chemists), Wataalamu wa masuala ya Fedha na Wachumi pamoja na wataalam wa masuala ya sheria na kodi, kadri itakavyoona inahitajika.
11. Endapo itafaa, kuongeza Hadidu za Rejea katika kuboresha utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, kamati itakuwa na mamlaka ya kumwita mtu yeyote au uwasiliana na ofisi yoyote ya Serikali (kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi) kwa lengo la kupata taarifa muhimu zinazohitajika.

Utekelezaji wa majukumu
Mheshimiwa Rais,
Katika kutekeleza uchunguzi huo, kamati ilifanya mambo Yafuatayo;
1. Kuandaa Mpango Kazi, kukusanya na kupitia mikataba, sheria, sera za madini na kodi, hususan mikataba ya utafiti, uchimbaji, usafirishaji na uuzaji wa madini na makinikia, kuchambua na kuhakiki mfumo mzima wa udhibiti wa biashara ya makinikia, na taarifa kupokea taarifa kutoka mamlaka za Serikali nchini na nje ya nchini kuhusiana na uchenjuaji wa makinikia.
2. Kutembelea na kupata taarifa kutoka sehemu na taasisi zifuatazo;
i. Migodi ya Bulyanhulu Gold Mines Ltd (Acacia Gold Mining Plc), Pangea Gold Mine Ltd (Acacia Gold Mining Plc), North Mara Gold Mine Ltd (Acacia Gold Mining Plc), Geita Gold Mine Ltd (AngloGold Ashanti Ltd).
ii. Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa lengo la kuona na kupima uzito wa makontena 277 yenye makinikia yaliyozuiliwa na Serikali.
iii. Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ofisi Kuu ya Takwimu, Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania(TMAA), Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) na Ofisi ya Msajili wa Makampuni (BRELA), Mamlaka ya Masoko ya Hisa na Mitaji (CMSA).
3. Kuwaita na kufanya mahojiano na;
i. Watendaji wakuu serikalini na watumishi wa taasisi za serikali na binafsi.
ii. Watu binafsi wenye ujuzi na uzoefu katika sekta ya madini, usafirishaji wa mizigo na wakala wa meli.
4. Kupata taarifa na kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine zilizofanikiwa katika biashara ya madini na uchenjuaji wa makinikia.
5. Kukusanya na kufanya uchambuzi wa takwimu za makontena ya makinikia yaliyosafirishwa nje ya nchi na takwimu za kiuchumi na kodi ili kubaini kodi halisi iliyolipwa na kodi ambayo ilipaswa kukusanywa kutokana na biashara ya uuzaji wa makininkia nje ya nchi kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2017.
6. Kufanya uchambuzi kuhusu uwezekano wa ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia nchini.
7. Kufanya uchambuzi wa taarifa za kimaabara za makinikia zilizotolewa na kampuni ya maabara binafsi inayopima sampuli za makinikia ya madini (SGS), Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Kamati Maalum namba 1.

Matokeo ya Uchunguzi
Mheshimiwa Rais

1. Uhalali wa Kisheria wa Kampuni ya Acacia Mining Plc
nchini Tanzania.
Kamati imebaini na kuthibitisha kwa mujibu wa nyaraka na maelezo kutoka ofisi ya Msajili wa Makampuni (BRELA) kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc haikusajiliwa (incorporation) nchini Tanzania na wala haina hati ya utambuzi (certificate of compliance) kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212.
Kamati pia imebaini kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc, ambayo inajinasibisha kuwa mmiliki wa makampuni ya Bulyanhulu Gold Mines Ltd, North Mara Gold Mine Ltd na Pangea Minerals Ltd, haikuwahi kuwasilisha nyaraka wala taarifa yoyote kuonesha kuwa kampuni hiyo ni mmiliki wa makampuni hayo wala kuwa na hisa katika makampuni hayo. Kwa kuwa Acacia Mining Plc haina usajili wala utambuzi wa kisheria nchini Tanzania, haina sifa ya kupata leseni, kuchimba wala kufanya biashara ya madini nchini Tanzania.
Hivyo basi, Kamati imebaini kuwa Acacia Mining Plc, inafanya biashara ya madini hapa nchini kinyume cha sheria za nchi.

2. Biashara ya Uuzaji na Usafirishaji wa Makinikia Nje ya
Nchi
Mheshimiwa Rais, Kamati ilibaini kuwa makampuni ya Bulyanhulu Gold Mines Ltd na Pangea Minerals Ltd ndizo wazalishaji na wauzaji wa makinikia nje ya nchi. Kwa mujibu wa mikataba ya mauzo ya makinikia baina ya makampuni hayo na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, makinikia husafirishwa kutoka Tanzania yakiwa yameshauzwa na hupelekwa nje ya nchi kwa madai ya kwenda kuchenjuliwa kupitia Bandari za Dar es Salaam na Tanga.

Makinikia hayo hupelekwa nchi za China, Japani na Ujerumani, yakiwa kwenye makontena yenye urefu wa futi 20 na wastani wa tani 20 kila moja. Wafanya biashara wa makinikia ni makampuni yaitwayo Aurubis AG na Aurubis Bulgaria ADM, Mark Rich Co. Investment AG na Pan Pacific Copper Co. Limited kutoka nchi za Ujerumani, Uswisi na Australia.

Mauzo hayo ya makininkia hufanywa kwa mujibu wa mikataba ya uchimbaji wa madini kati ya Serikali na Makampuni ya uchimbaji madini (Mining Development Agreements-MDAs). Kutokana na taarifa za kiuchunguzi (forensic investigation) kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mauzo ya makininkia hufanyika kupitia Ofisi ya hasibu (Treasury Department) ya makampuni hayo iliyopo Afrika ya Kusini.

3. Utaratibu wa Uuzaji Makinikia Nje ya Nchi
Mheshimiwa Rais, Kamati imebaini kwamba kifungu cha 51 cha Sheria ya Madini kinaruhusu mwenye leseni ya uchimbaji wa madini kufanya biashara ya madini, ikiwa ni pamoja na kuuza nje ya nchi. Kifungu hicho kinamtaka mwenye leseni ya uchimbaji kupata kibali cha kusafirisha madini kutoka kwa Afisa Mwenye Mamlaka atayethibitisha kwamba mrahaba stahiki umelipwa kwa Serikali. Mbali ya kupata kibali kinachoonesha malipo ya mrahaba hakuna utaratibu mwingine maalum katika biashara ya uuzaji na usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Aidha, kisheria makampuni ya madini yanapaswa kutoa taarifa sahihi kwa Serikali kuhusu aina, kiasi na thamani ya madini yaliyomo ili kuiwezesha Serikali kukokotoa na kutoza mrahaba stahiki.

Mheshimiwa Rais, Kwa kuzingatia nyaraka na taarifa mbalimbali za kiuchunguzi, Kamati imeridhika kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali, watumishi na wamiliki wa makampuni ya madini, makampuni ya usafirishaji na upimaji wa madini na makampuni yenyewe yametenda makosa mbalimbali ya kijinai yakiwemo ukwepaji wa kodi, kutoa taarifa za uwongo, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, uhujumu uchumi na kulisababishia taifa hasara kinyume cha;

i. Vifungu vya 18,114 na 115 vya Sheria ya Madini, 2010
ii. Vifungu vya 101 na 106 vya sheria ya kodi ya mapato, 2004
iii. Vifungu vya 79 na 82 vya Sheria Usimamizi wa kodi, 2015
iv. Kifungu cha 24 cha Sheria ya Uwazi na uwajibikaji katika sekta ya Madini Tanzania, 2015
v. Kifungu cha 27 cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi sura ya 200.
vi. Kifungu cha 203 cha Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,2004 kwa kuzingatia nyaraka na taarifa mbali mbali za kiuchunguzi Kamati pia imeridhika kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali, watumishi na wamiliki wa makampuni ya madini, makampuni ya usafirishaji na upimaji wa madini na makampuni yenyewe wamelitia aibu Taifa kwa kutenda makosa mbali mbali yakiwemo, ukwepaji wa kodi, kutoa taarifa za uwongo, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, uhujumu uchumi na kulisababishia taifa hasara.

Mheshimiwa Rais, Kamati pia imebaini kwamba, katika kufanya biashara ya makinikia makampuni ya Bulyanhulu na Pangea yamekuwa yakiuza makinikia nje ya nchi pasipo kufuata utaratibu kwa namna ambayo vitendo vifuatavyo vimedhihirika;

i. Udanyanyifu wa kibiashara na ukwepaji wa kodi
ambao umesababisha;
a. Kuficha idadi, uzito na thamani ya madini yaliyomo kwenye makontena 277 yaliyozuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kiwango cha wastani kuonesha kwamba thamani yake ni TZS 79,939,900,989.49 (TZS 79.94 bilioni), wakati thamani halisi, kwa mujibu wa uchunguzi wa kimaabara uliofanywa na Kamati Maalum Na. I, unaonesha kuwa thamani halisi ya madini yaliyomo, ni kati ya TZS 829,361,455,861 (TZS 829.36 bilioni) kwa kiwango cha chini, na TZS 1,438,760,551,512 (TZS 1.438 trilioni) kwa kiwango cha juu.
b. Mgongano au kusigana kwa taarifa za uzito na idadi ya makontena kati ya nyaraka za kusafirishia makontena (kadhia) ukilinganisha na nyaraka za wakala wa meli (shipping orders). Idadi na uzito wa makontena ikiwa kubwa zaidi kwenye nyaraka za wakala wa meli kuliko kadhia (export entry) zilizotengenezwa na makampuni hayo kwa lengo la kusafirishia makontena nje ya nchi.
c. Kiasi cha mrahaba kilichooneshwa katika vitabu vya hesabu za makampuni ya Bulyanhulu na Pangea zimeonesha kwamba, Dola za Marekani 111,304,561.00 (USD 111.3 milioni) zililipwa Serikalini kama mrahaba kati ya mwaka 1998 na 2017, lakini vitabu vya hesabu vilivyopo Wizara ya Nishati na Madini zinaonesha malipo yalikuwa Dola za Marekani 42,702,727.50 (USD 42.7 milioni). Hali hii inaonesha upungufu wa kiasi cha Dola za Marekani 68,601,833.50 (USD 68.6 milioni) zilizopaswa kulipwa kama mrahaba.
d. Makampuni ya wakala wa meli ya Freight Forwarders (T) Limited, Quick Services Clearing and Forwarding Limited na Walford Meadows Co. Ltd, ziliwasilisha nyaraka za uwongo za usafirishaji wa makinikia kutoka Kahama Mining Corporation, (baadaye Bulyanhulu Gold Mine Ltd) na Pangea Minerals Ltd, katika kipindi cha kati ya mwaka 1998 na 2017.
e. Kutoa taarifa za uwongo za uchenjuaji nje ya nchi wakati makanikia hayo yameuzwa kabla ya kusafirishwa kutoka Tanzania kupelekwa nchi za nje.

ii. Kufanya magendo katika biashara ya makinikia;
a. Makontena 30 ya urefu wa futi 20 yenye makinikia yameelezwa kwenye hati ya usafirishaji nje ya nchi Na.1482 ya tarehe 23.7.2001. Hata hivyo iligundulika kupitia hati ya usafirishaji melini Na. TZGT00000552 kuwa makontena 33 yenye urefu wa futi 20 ndiyo yalisafirishwa na kwa sababu hiyo yakionyesha makontena matatu zaidi ya idadi iliyooneshwa kwenye hati ya usafirishaji melini iliyoandaliwa na wakala wa usafirirshaji, kwa niaba ya makampuni ya uchimbaji madini.
b. Makontena 60 ya urefu wa futi 20 yenye makinikia yameelezwa kwenye hati ya usafirishaji nje ya nchi Na. 1483 ya tarehe 7.8.2001. Hata hivyo, iligundulika kupitia hati ya usafirishaji melini Na. MOL-1 ya makontena hayo hayo, kuwa makontena 67 yenye urefu wa futi 20 ndiyo yalisafirishwa na kwa sababu hiyo, ikiwa ni makontena saba (7) zaidi ya idadi iliyooneshwa na wakala wa usafirishaji, kwa niaba ya makampuni ya uchimbaji madini.
c. Makontena 48 ya urefu wa futi 20 yenye makinikia yameelezwa kwenye hati ya usafirishaji nje ya nchi Na.1487 ya tarehe 27.8.2001. Hata hivyo, iligundulika kupitia hati ya usafirishaji melini Na. Mol-100038 kuwa makontena 67 yenye urefu wa futi 20 yalisafirishwa na kwa sababu hiyo yakionyesha makontena kumi na tisa (19) zaidi ya idadi iliyooneshwa kwenye hati ya usafirishaji melini iliyoandaliwa na wakala wa usafirirshaji kwa niaba ya makampuni ya uchimbaji madini.
d. Makontena 85 ya urefu wa futi 20 yenye makinikia yameelezwa kwenye hati ya usafirishaji nje ya nchi Na.1504 ya tarehe 20.12.2001. Hata hivyo, iligundulika kupitia hati ya usafirishaji melini Na. Mol-01 kuwa makontena 99 yenye urefu wa futi 20 ndiyo yalisafirishwa na kwa sababu hiyo yakionesha makontena kumi na nne (14) zaidi ya idadi iliyooneshwa kwenye hati ya usafirishaji melini iliyoandaliwa na wakala wa usafirishaji, kwa niaba ya makampuni ya uchimbaji madini.

iii. Ukwepaji wa kodi ya mapato kwa njia ya udanganyifu
wa bei ya bidhaa au huduma (transfer price manipulation).
a. Mauzo ya makinikia kwa wafanyabiashara na wachenjuaji nje ya nchi hayakufanyika kwa ushindani kutokana na kuonesha vipindi virefu vya uhusiano wa kibiashara kwa kuzingatia nyaraka za mikataba baina yao.
b. Masharti ya usafirishaji wa makinikia ulionyeshwa kuwa free on board (f.o.b) badala ya cost and freight (c.fr) au cost, insurance and freight (c.i.f) makanikia hayo yaliuzwa kwa wafanya biashara wale wale na wachenjuaji wale wale wenye mahusiano ya kibiashara kama ilivyooneshwa katika mikataba ya mauzo ya makinikia baina yao.
c. Madini yaliyouzwa nje ya nchi hayakuwa makinikia hasa badala yake, yalikuwa ni madini ya aina mbali mbali mahususi yaliyopatikana kutokana na uchenjuaji kwa njia ya ‘carbon–inleach’ (CIL).

iv. Upandishaji wa gharama za uendeshaji migodi; Uchunguzi wa kisayansi wa mifumo ya computa forensic examination kupitia TRA, umebaini kwamba gharama za utafutaji na upembuzi wa miamba yenye madini mejumuishwa kwenye gharama za mauzo na kwa sababu hiyo, kuathiri faida halisi ambayo ilipaswa kutozwa kodi. Hali hii imesababisha faida ya makampuni kutoonekana na kwa sababu hiyo kuathiri msingi wa ukokotoaji kodi ya mapato ya makampuni (tax base for corporate tax).

v. Mrahaba ambao haukukusanywa
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2007, 2011 na 2012 zilizotolewa na PriceWater Coopers, bei ya dhahabu katika soko la kimataifa imekuwa ikipanda na kuwezesha makampuni ya madini kupata faida zaidi ya asilimia 1,400 mwaka 2002 na 2006 ambapo Bulyanhulu na Pangea, zilipata faida ya asilimia 32. Hata hivyo, faida yote iliyopatikana kutokana na kupanda kwa bei ya dhahabu haikuoneshwa kwa madhumuni ya malipo ya mrahaba kwa Serikali.

vi. Uhamishaji haramu wa fedha
Uchunguzi wa kisayansi na mifumo ya komputa kupitia TRA imebainika kuwa faida iliyooneshwa na Kampuni mama Holding Company) iliyopo nje ya nchi ya Tanzania imekuwa ikirudishwa kwenye makampuni ya uchimbaji nchini kama mikopo iliyotolewa na riba zake. Baadaye riba inayotozwa kwenye taarifa za hesabu Kama gharama kwa makampuni ili kutumika katika kukokotoa kodi ya mapato ya kampuni Assessment of Corporate Income Tax).

Thamani ya Madini Yalimo kwenye Makinikia Kwenye Makontena 44,277
Mheshimiwa Rais,Uchunguzi wa Kamati ulibaini kuwepo takwimu mbali mbali za idadi ya makontena yaliyosafirishwa nje nchi kuanzia mwaka 1998 hadi mwezi Machi 2017. Hata hivyo, Kamati iliamua kutumia takwimu kutoka Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa (TRA) kwa kuwa, moja ya majukumu ya idara hiyo ni kukusanya takwimu za bidhaa zote zinazosafirishwa nje ya nchi kupitia bandari, viwanja vya ndege na mipaka ya nchi. Kutokana na chanzo hicho idadi ya makontena yaliyosafirishwa yalikuwa 44,277 kwa kiwango cha chini na makontena 61,320 kwa kiwango cha juu kutoka kwenye vyanzo vyetu vya uchunguzi.

Viwango vya Dhahabu kwenye Makinikia

Mheshimiwa Rais, Viwango vya dhahabu vilikuwa na wastani wa 28 kg za dhahabu kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha dhahabu kwenye kila kontena, makontena 44,277 yatakuwa na dhahabu kiasi cha tani 1,240. Kiasi hiki kina thamani ya TZS 108,062,091,984,000 (TZS 108.06 trilioni), sawa na USD 49,119,132,720 (USD 49.12 bilioni). Kwa kutumia kiwango cha juu cha dhahabu kwa kontena moja (47.5 kg), kiasi cha dhahabu katika makontena 44,277 kitakuwa tani 2,103 ambazo thamani yake ni TZS 183,319,620,330,000 (TZS 183.32 trilioni), sawa na USD 83,327,100,150 (USD 83.32 bilioni).

Viwango vya Madini ya Silver, Copper, Sulphur, Iron, Nickel
na Zinc kwenye Makinikia

Madini ya Silver
Kiwango cha Silver kilikuwa ni wastani wa 6.1 kg kwa kila kontena. Kwa kutumia kiwango hicho kwa kila kontena, makontena 44,277 yatakuwa na Silver kiasi cha tani 270. Kiasi hiki kina thamani ya TZS 329,660,684,232 (TZS 329.66 bilioni),sawa na USD 149,845,766 (USD 149.8 milioni). Kwa kutumia kiwango cha juu katika kontena moja (7 kg) kiasi cha Silver katika makontena 44,277 kitakuwa tani 309 ambazo thamani yake ni TZS 378,299,145,840 (TZS 378.3 bilioni) sawa na USD 171,954,157 (USD 172 milioni).

Madini ya Copper
Kiwango cha copper kilikuwa na wastani wa 5,200 kg kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha copper kwenye kila kontena lenye tani 20, makontena 44,277 yatakuwa na copper kiasi cha tani 230,240. Kiasi hiki cha copper kina thamani ya TZS 2,861,888,172,000 (TZS 2.86 trilioni) sawa na USD 1,300,858,260 (USD 1.3 bilioni). Kwa kutumia kiwango cha juu cha copper kwa kontena moja (6,756 kg), kiasi cha copper katika makontena 44,277 kitakuwa tani 299,135 ambazo thamani yake ni TZS 3,718,253,171,160 (TZS 3.72 trilioni) sawa na USD 1,690,115,078 (USD 1.692 bilioni).

Madini ya Sulphur
Kiasi cha Sulphur kilikuwa na wastani wa 7,800 kg kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha Sulphur kwenye kila kontena lenye tani 20, makontena 44,277 yatakuwa na Sulphur kiasi cha tani 345,360. Kiasi hiki cha Sulphur kina thamani ya TZS 227,937,996,000 (USD 103,608,180). Kwa kutumia kiwango cha juu cha sulphur kwa kontena moja lenye uzito wa 10,160 kg, kiasi cha Sulphur katika makontena 44,277 kitakuwa tani 449,854 ambazo thamani yake ni TZS 296,903,851,200 (TZS 296.9 bilioni), sawa na USD 134,956,296 (USD134.96 milioni).

Madini ya Iron
Kiwango cha iron kilikuwa na wastani wa 5,400 kg kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha iron kwenye kila kontena lenye tani 20, makontena 44,277 yatakuwa na iron kiasi cha tani 239,095. Kiasi hiki cha iron kina thamani ya TZS 368,207,532,000 (USD 167,367,060). Kwa kutumia kiwango cha juu cha iron kwa kontena moja lenye uzito wa 6,100 kg, kiasi cha iron katika makontena 44,277 kitakuwa tani 270,089 ambazo thamani yakeni ni TZS 15,938,138,000 (TZS 415.94bilioni), sawa na USD 189,062,790 (USD 189.06 milioni).

Madini ya Nickel na Zinc

Zinc
Kiwango cha zinc kilikuwa ni wastani wa 5,400 kg kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha zinc kwenye kila kontena lenye tani 20, makontena 44,277 yatakuwa na zinc kiasi cha tani 1,474. Kiasi hiki cha zinc kina thamani ya TZS 8,433,705,852 (TZS 8.43 bilioni) sawa na USD 3,833,503 (USD 3.83 milioni). Kwa kutumia kiwango cha juu ilichopimwa kwa makontena moja (65.8 kg) kiasi cha zinc katika makontena 44,277 kitakuwa na uzito wa tani 2,913 kg ambazo thamani yake ni TZS 16,664,800,152 (TZS16.66 bilioni), sawa na USD 7,574,909 (USD 7.57 milioni).

Nickel
Kiwango cha nickel kilikuwa ni wastani wa 5,400 kg kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha nickel kwenye kila makontena, makontena 44,277 yatakuwa na nickel kiasi cha tani 620. Kiasi hiki cha nickel kina thamani ya TZS 13,228,196,520 (6,012,817). Kwa kutumia kiwango cha juu kilichopimwa kwa makontena moja kiasi cha inickel katika makontena 44,277 kitakuwa tani 1,771 ambazo thamani yakeni ni TZS 37,794,847,200 (USD 17,179,476).

Madini ya kundi la Platinum Rhodium
Viwango vya rhodium vilikuwa na wastani wa 0.034 kg za rhodium kwenye kila kontena. Kwa kutumia kiasi hiki cha rhodium kwenye kila kontena lenye tani 20, makontena 44,277 yatakuwa na rhodium kiasi cha tani 1.5. Kiasi hiki cha rhodium kina thamani ya TZS 105,754,560,707 (TZS 105.75bilioni), sawa na USD 6,012,817 (USD 6.01 milioni). Kwa kutumia kiwango cha juu cha rhodium kwa kontena moja 0.078 kg, kiasi cha rhodium katika makontena 44,277 kitakuwa tani 3.5 kg ambazo thamani yake ni TZS 242,613,403,976 (TZS 242.6 bilioni), sawa na USD 110,278,820(USD 110.28 milioni).

>>ITAENDELEA

1161 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons