TRA ina mianya ya rushwa

 

 

474. Idara hizi hukusanya asilimia 70 – 73 ya mapato yote ya Serikali Kuu yanayotokana na kodi mbalimbali. Hali ya ukusanyaji kodi katika idara hizi kwa kipindi cha miaka mitano imeonyeshwa katika kiambatisho A.

 475. Pamoja na ongezeko katika makusanyo ya kodi bado uwiano kati ya mapato na Pato la Taifa ni mdogo. Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba uwiano kati ya wastani wa kodi ni asilimia 15 za pato la taifa. Hata hivyo kwa kuwa ukadiriaji wa pato la taifa uko chini, uwiano huo ni kati ya asilimia 8 hadi 10 tu ya Pato la Taifa ikiliganishwa na wastani wa asilimia 18-20 ya Pato la taifa kwa nchi zilizo maskini zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hali hii inatokana na mfumo wa kodi kuhamasisha matumizi zaidi kuliko ukusanyajiwa kodi. Kulegalega kwa utaratibu huu kumetokana na utaratibu wa malipo ya kodi kwa awamu na hivyo kusababisha malimbikizo ya madeni. Aidha, madeni haya na hasa yale ya nje yameongezeka kwa kasi kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu.

Serikali imekuwa inachukua hatua za mara kwa mara za kurekebisha mfumo wa kodi nchini ili kuboresha mapato ya serikali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Tume ya Rais ya Kuangalia Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali Mwaka 1992, bila ya mafanikio ya kuridhisha. Uwiano kati ya mapato yatokanayo na kodi na Pato la taifa mwaka 1995 ni sawa na ule wa 1990.

476.  Kutokana na matatizo ya mfumo mzima wa ukusanyaji wa kodi nchini kumekuwepo na kilio miongoni mwa wananchi na hata wafadhili kuhusu kuvuja kwa mapato ya serikali, sheria, viwango vya kodi, taratibu na mfumo uliopo wa kukusanya mapato ya serikali unatoa mianya mingi hasa kutokana na kuzorota kwa uwajibikaji katika vyombo hivi.

 Wafanyabiashara kwa kushirikiana na watumishi wa Idara hizi wamekuwa wanakwepa kodi. Aidha, baadhi ya watumishi  wa idara hizi wamejenga tabia ya kupokea rushwa kutoka kwa wateja na hivyo kuwakadiria kodi ndogo jambo ambao linainyima serikali mapato na hivyo kuzorotesha juhudi za serikali za kuboresha uchumi wetu.

 

IDARA YA FORODHA

 

1 Tanzania Challenge and Reforms, Growth, Incomes and Welfare Vol II W/Bank December, 1995.

477. Idara hii imeanzishwa chini ya Sheria ya Customs Tarriff Act No. 12 ya 1996 ambayo inaruhusu kutoza ushuru bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje. Sheria hii ni ya Muungano na inampa mamlaka Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano kutoa misamaha ya kodi pamoja na vibali vya malipo ya Ushuru kwa awamu pale ambapo mteja anakabiliwa na ukata. Chini ya taratibu za forodha, bidhaa zote zimegawanywa katika Tarriffs mbalimbali kwa kuzingatia Customs Cooperation Council Nimeclature (CCCN) ili kurahisisha ukadiriaji wa kodi.

 

MUUNDO

 478. Idara inaongozwa na Kamishna akisaidiwa na Makamishna Wasaidizi watatu, wanaooogoza Idara tatu za Makao Mkuu na mmoja kwa ajili ya Kanda ya Zanzibar.

 479. Idara hii ina Idara tatu za shughuli za Forodha, Upelelezi na Mashtaka, Utafiti na Sera, Idara ya Shughuli ya Forodha ndiyo inayowajibika na kushughulikia mizigo na ina vitengo vya Import and Export (IMPEX), Tarriffs na Tathmini. Shughuli za Idara zimegawanyika katika Kanda 8 kama ifuatavyo:

 (i) Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya vituo vilivyoko katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma.

 (ii) Kanda ya Tanga kwa ajili ya vituo vya Forodha vilivyoko katika Mkoa wa Tanga.

 (iii) Kanda ya Kaskazini inayoshughulikia vituo vya Forodha vilivyoko katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Singida.

 (iv) Kanda ya Ziwa – inayoshughulika na vituo vya mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Shinyanga.

 (v) Kanda ya Kigoma – inashughulikia vituo vya mikoa ya Kigoma na Tabora.

 (vi) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayoshughulikia mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa.

 (vii) Kanda ya Kusini kwa ajili ya vituo vya mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

 (viii)      Kanda ya Zanzibar inayoghughulikia vituo vya Unguja na Pemba.

480. Tume imefanya uchambuzi wa kina kuhusu shughuli za Idara hii na kubaini kwamba Sheria ya Forodha, Sera ya Kodi ya Forodha na usimamizi wake, kanuni na taratibu za utendaji kazi za Idara hii, zinasababisha mianya ya rushwa ambapo inaipunguzia serikali mapato kama ifuatavyo:

 

WAJIBU NA UWAJIBIKAJI

 481. Huko nyuma baadhi ya Viongozi na Wasaidizi wao katika Idara hizi walitumia nyadhifa zao kupokea rushwa kama ifuatavyo:

(i) Upangaji wa watumishi

Katika Idara hizi kuna baadhi ya sehemu za idara ambazo watumishi huhudumia wateja kila siku. Kwa mfano sehemu ya ukadiriaji wa kodi ya mapato, sehemu ya ukaguzi wa mizigo bandarini na Tarriffs Identification, Transit Goods na Container Terminals ni sehemu nyeti ambapo watumishi wanakutana na wateja wengine mara kwa mara na wana madaraka makubwa sana kuhusu hatma ya mteja.

Kwa kuwa wakubwa katika idara wanajua kwamba hizo ni sehemu ambazo wateja hulazimika kutoa rushwa, hupeleka ndugu au swahiba zao kuongoza sehemu hizo na kuwataka wawe wanawaletea baadhi ya fedha (kick-backs) wanazopokea kutoka kwa wateja kama rushwa. Watumishi katika sehemu hizi ni nadra kuhamishwa na kama hapana budi uhamisho hufanywa na Kamishna mwenyewe jambo ambalo linaingilia shughuli za Idara ya Utumishi.

 

(ii) Uhamisho wa Watumishi

Enzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mtumishi wa Idara ya Forodha alikuwa hakai katika kituo kimoja kwa muda mrefu. Utaratibu huu uliwezesha maofisa wa Forodha kutozoeana na wateja. Siku hizi utaratibu wa uhamisho hasa wa wakuu wa kanda umekufa ama kutokana na uhaba wa fedha au kwa sababu wanatumiwa na  wakubwa wao kama vitega uchumi vyao.

 Matokeo yake ni kwamba watumishi wanawazoea wateja wao kiasi kwamba wanaoneana haya wakati wa kushughulikia mizigo yao.  Aidha ili waendelee kubakia katika sehemu hizo inabidi kuomba rushwa na kuiwasilisha kwa wakubwa wao kama zawadi, michango  n.k.

 (i) Mamlaka ya Mapato imeajiri tu baadhi ya wafanyakazi waliokuwa chini ya Idara ya Forodha baada ya kuwafanyia mchujo. Kwa bahati mbaya zoezi hili lilichukua muda mfupi na mamlaka haikupata muda wa kuajiri na kufundisha watumishi wapya ili kuziba pengo lililojitokeza kabla ya Julai 1996. Kwa  hiyo katika kipindi cha muda mfupi, Mamlaka itakabiliwa na upungufu wa watumishi jambo ambalo linaweza kuleta kero kwa wateja na hivyo kudhania kwamba wanatakiwa kutoa rushwa.

 

482. MASLAHI YA WATUMISHI

Moja ya sababu inayotolewa na wengi kwamba inasababisha rushwa ni kipato kidogo cha watumishi wa Idara. Sababu hii inaweza kuwa kweli kwa wale watumishi wa ngazi za chini, lakini kwa wale ambao wanapokea rushwa kutokana na tamaa ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya maisha sababu hii haina msingi.

Kwa mtumishi wa Longroom aliyezoea kupata rushwa ya Shs 20-30,000 kwa siku, kuongeza mshahara wake hata mara 10 ya kima cha sasa hakutamshawishi aache kudai na kupokea rushwa. Hata hivyo ili kuondokana na kisingizio hiki pamoja na kuhakikisha kwamba kila mtumishi anawajibika kikamilifu katika kazi yake [ni bora kuwaongezea]. Mamlaka imeandaa na kutekeleza mfumo wa mshahara ambao una marupurupu na vivutio vizuri ikilinganishwa na mfumo wa mishahara serikalini.

 483. Katika hali isiyo na kasoro, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipaswa kuanza kazi ikiwa na safu mpya ya viongozi pamoja na wafanyakazi wa ngazi zote. Ukweli ni kwamba TRA imerithi sehemu kubwa ya wafanyakazi waliokuwa wakizitumikia Idara za Kodi inazozirithi. TRA ilitakiwa kuandaa na kutekeleza taratibu za kuwapata watumishi wapya na ambao wangepelekwa mafunzoni kujifunza taratibu  ya ukusanyaji wa kodi na ushuru ili kuchukua nafasi za watumishi waliopunguzwa.

 Pamoja na ahadi zilizotolewa kwa utafiti na upekuzi mkali utatekelezwa ili kuwezesha kubakisha wale wafanyakazi wenye uadilifu wa kutosha, tatizo la muda na hali ya rushwa ndani ya Idara hizo katika miaka hii ya karibuni ilisababisha pia uzorotaji katika taratibu za utunzaji wa kumbukumbu sahihi za wafanyakazi. Kwa hiyo kumbukumbu zilizotumika katika kuwachuja wafanyakazi hao hazikuwa kamilifu na upo wasiwasi kwamba baadhi ya wafanyakazi waliorithiwa sio wazuri na wataendelea kusambaza kansa ya rushwa ndani ya mfumo waw TRA.

 

MAPENDEKEZO

484. Ili kuweza kuziba mianya ya rushwa pamoja na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya serikali yatokanayo na kodi na ushuru, Tume inatoa mapendekezo yafuatayo:

(i) Uwajibikaji wa uongozi wa juu katika maeneo yote ya uendeshaji wa serikali na taasisi zake ndiyo utakaokuwa changamoto la vita dhidi ya rushwa. Kwa hiyo badi Bodi na Menejimenti ya TRA zipewe madaraka kamili ya kuhakikisha kwamba Mamlaka inaajiri watumishi waaminifu na watakaoongozwa na maadili mema katika utendaji wao wa siku hadi siku.

 (ii) Ili kuhakikisha kwamba Kamishna Mkuu na Makamishna wa Idara za Kodi wanawajibika kwa Bodi ipasavyo. Bodi ndiyo iwe chombo cha kuwaajiri badala ya wao kuteuliwa na Waziri wa Fedha. Mamlaka ya Waziri yabakie katika kumshauri Rais juu ya uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi na kuwateua wajumbe wanne wa Bodi hiyo.

(iii) Wizara ya Fedha itunge kanuni mahususi zitakazowwjibisha Wajumbe wa Bodi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka na Makamishna.

(iv) Mamlaka ya Mapato iandae utaratibu ambao utamwajibisha kila mtumishi katika kazi yake na ambao utaiwezesha kuchukua hatua kali na za haraka dhidi ya watumishi watakaojihusisha na vitendo viovu katika ukadiriaji na ukusanyaji wa mapato ya serikali ndani ya mamlaka.

 (v) Moja ya sababu zinazowafanya watumishi wa umma hususan wale wanaohusika na huduma kwa jamii kushawishika kudai na kupokea rushwa ni mazoea ya kuwa karibu mno kati ya watumishi hao na watu wanaowahudumia. Ili kuhakikisha kwamba watumishi wa Mamlaka ya Mapato hawajengi tabia ya kuzoeana mno na wateja, inapendekezwa kwamba utaratibu wa makusudi uwepo wa kuwabadilishia vituo vya kazi watumishi wake katika vipindi maalum.

 (vi) Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wapewe maslahi yatakayowawezesha kumudu maisha ili kuwapunguzia vishawishi vya kudai na kupokea rushwa.

(vii) Idara ya Upelelezi na Mashtaka ya Mamlaka ya Mapato iwe ni kitengo maalum cha Ofisi ya Kamishna Mkuu ili iweze kufanyakazi kwa ufanisi katika idara zote.

 

KANUNI NA TARATIBU ZA KAZI

485. Mauzo Nje

Mfanyabiashara anayetaka kuuza bidhaa nje anatakiwa kujaza fomu za mauzo nje, (CD 3 Form) kutoka Benki Kuu ya Tanzania pamoja na vibali kutoka Wizara zinazohusika, pale ambapo bidhaa hiyo inahitaji kibali na kuziwasilisha Idara ya Forodha. Idara inapitia fomu hizo kuona kama zimejazwa vizuri, hufanya malinganisho ya bei ya kuuza nje na bei ashiria zinazotolewa na Benki Kuu ili kubaini usahihi wake.

Kama bidhaa inayotarajiwa kuuzwa nje ni bidhaa asilia kama kahawa, pamba, tumbaku, chai, korosho, katani na mashudu ya pamba, mteja hutakiwa kulipa kodi ya mauzo ya nje ambayo ni asilia mia mbili ya thamani ya bidhaa hiyo ‘free on board’ au ‘free on road/rail.’ Bidhaa hiyo hukaguliwa na mfanyabiashara anaruhusiwa kupakia bidhaa hiyo kwenye meli kwa upande wa bandari na gari au treni kuruhusiwa kuvuka mpaka katika vituo vya forodha vilivyoko mipakani.

 486. Ijapokuwa utaratibu huu hauna tatizo, kumekuwepo na utata wakati serikali inapokataza mauzo ya bidhaa fulani nchi za nje. Hapo zamani palikuwepo na utaratibu ambapo kama bidhaa fulani inapigwa marufuku kuuzwa nje, Waziri anayehusika alikuwa anawasilisha kwa Kamishna wa Forodha na kumpatia orodha za bidhaa hizo kabla ya kutoa tangazo kwa umma ili kumwezesha Kamishna kuviarifu vituo vyote kabla ya tangazo kutolewa. Siku hizi Kamishna anapata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari. Mtindo huu una athari zifuatazo:

 (i) Mkuu wa Kituo cha mpakani anaweza asipate habari kupitia radio au gazeti na hivyo kuruhusu bidhaa hiyo kuuzwa nje.

 (ii) Mkuu wa Kituo chochote anaweza kupata taarifa kupitia vyombo vya habari lakini kwa kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka kwa Kamishna wake, anaruhusu bidhaa hiyo, lakini baada ya kupokea rushwa kutoka kwa mwenye bidhaa hiyo.

 

PENDEKEZO:

487. Pale  ambapo Serikali inataka kupiga marufuku uuzaji au uagizaji wa bidhaa ya aina fulani hapana budi kumjulisha Kamishna Mkuu wa Mapato ili aweze kuwajulisha maofisa wake katika idara inayohusika na uamuzi huo.

 

UTARATIBU WA KUSHUGHULIKIA BIDHAA ZINAZOAGIZWA KUTOKA NJE

 

488. Long room

Long room ni sehemu inayoshughulikia kadhia zote za Ushuru wa Forodha na kodi ya mauzo, ukusanyaji wa mapato pamoja na kuhasibu mapato hayo kabla ya mizigo kuondolewa bandarini. Watumishi wa Idara wanakusanya ushuru kwa bidhaa zenye thamani isiyozidi USD 5000. Ukadiriaji na ukusanyaji wa Ushuru na Kodi ya Mauzo kwa bidhaa zenye thamani inayozidi USD 5000 unafanywa na makampuni mawili ya kigeni (Preshipment Inspection (PSIs) ya SGS na InchCape.

 

489. Mizigo ya thamani isiyozidi USD 5000

(i) Mteja anawasilisha kadhia, Bill of Lading na Ankara sehemu ya mapokezi ya Idara ya Forodha. Hapa kadhia zinakaguliwa ili kubaini kama mteja ana Import Declaration Form, baadaye zinapigwa mhuri, kuandikishwa na mteja kupewa namba ya mwanzo.

(ii) Kadhia zinapelekwa sehemu ya Uthamini ambapo bei za bidhaa katika ankara hulinganishwa na bei ashiria za Idara.

(iii) Kadhia na fomu zote hupelekwa kwa Mkuu waUthamini ili kuthibitisha kwamba makadirio ya kodi yaliyofanywa na maofisa katika sehemu zote ilikopitia  kadhia ni sahihi.

(iv) Kadhia zinarudishwa tena sehemu ya Declaration ambapo inachunguzwa kama fomu zote zimejazwa kama inavyotakiwa na kupigwa mihuri.

(v) Kadhia hupelekwa sehemu ya malipo ambapo mteja analipa kodi zote na kupewa stakabadhi ya Serikali.

(vi) Kadhia hupelekwa sehemu ambapo hupewa namba na kujazwa kwenye rejesta kulingana na aina ya kodi iliyolipwa. Namba hizi hutumika kwa kila mwezi.

(vii) Kadhia zinapelekwa Pre-Audit ambapo zinachunguzwa kuona kama kodi zilizolipwani sahihi.

(viii) Kadhia hupelekwa sehemu ya ‘manifest’ ambapo wanachunguza kuona Kama ni kweli mzigo uko kwenye meli iliyoonyeshwa katika Bill of Lading.

(ix) Kadhia hupelekwa sehemu ya Central Distribution Office kuchunguzwa kama zimepitia sehemu zote zinazohusika na kodizote kulipwa.

 

Bandari

(x) Kadhia hupewa mhudumu wa Idara ambaye huzipeleka kwa Mkusanyaji Mkuu aliyeko Bandarini ambaye anazifanyia tena uchunguzi ili kuona kama zimepitia sehemu zote la Long room.

 (xi) Kadhia hupelekwa kwa Mkusanyaji Mkuu ambaye huzigawa katika sehemu zinazohusika na mizigo ya aina mbalimbali bandarini. Fomu nyingine za D&DO zinapelekwa katika ofisi za bandari ili mteja aweze kulipa gharama za mamlaka.

(xii) Mkaguzi Mkuu au Afisa Forodha chini yake hukagua mzigo ili kuhakikisha kwamba aina na idadi ya bidhaa inalingana na maelezo katika kadhia. Pale ambapo mzigo ni mkubwa kuliko ilivyoandikwa katika kadhia, Afisa Forodha anaweza kuongeza kiwango cha ushuru na kodi ya mauzo na mteja kutakiwa kulipa tofauti ya makadirio mapya na ile iliyolipiwa Long room au anaweza kumfungulia mashtaka ya udanganyifu ili alipe tofauti ya ushuru pamoja na adhabu.

 

490. Bidhaa zenye thamani ya zaidi ya USD 5000

(i) Mfanyabiashara anapotaka kuagiza bidhaa anapata Ankara Kifani (Proforma Invoice) kutokakwa muuzaji/mzalishaji.

(ii) Mfanyabiashara anachukua Ankara Kifani hadi Benki yake ambapo ananunua Import Declaration Form (IDF) kwa bei ya asilimia 1.2 ya gharama ya bidhaa anazoagiza FOB. Malipo haya huitwa Pre-shipment Inspection/Tax Assessment Programme Fee.

(iii) Benk inawasilisha Import Declaration Form pamoja na Ankara Kifani kwa kampuni ya Ukaguzi na ukadiriaji wa mizigo ofisi ya SGS au InchCape ambao huagiza ofisi zao huko nje kukagua mizigo hiyo.

(iv) Makampuni hufanya Pre-shipment Inspection ya mizigo hiyo na kuandaa Clean Report of Finding na kuiwasilisha Ofisi ya Dar es Salaam.

(v) PSI inayohusika hukadiria kodi zote zinazotakiwa kulipwa na kujaza fomu ya Tax Assessment Note (TAN) na kupewa mteja.

 (vi) Mteja anachukua TAN na kwenda kulipa kodi hizo Benki ya Taifa ya Biashara.

(vii) Baada  ya malipo mteja anachukua TAN pamoja na IDF na kuambatisha fomu ya malipo na kuziwasilisha sehemu ya mapokezi ya long room ambapo kadhia inafuata utaratibu ule wa kadhia za mizigo yenye thamani isiyozidi USD 5000  mpaka mzigo unapochukuliwa bandarini.

491. Mkusanyaji Mkuu au Afisa Forodha aliyeko chini yake anatakiwa kufanya ukaguzi wa mizigo yote kabla ya kuruhusu Mamlaka ya Bandari kumpatia mteja mizigo yake. Pale ambapo mizigo ni mingi kwa mfano makasha 5 hadi 10, Afisa Forodha  anafanya ‘random sampling’ ya kontena 2 na 3 na kufanya ukaguzi wa mizigo iliyopo. Kwa kuwa kontena moja inaweza kuwa na mizigo mingi, Afisa Forodha anakagua baadhi tu ya mizigo hiyo na akiridhika huruhusu mizigo yote iondolewe bandarini.

Pale ambapo mizigo ni mingi kuliko ilivyoonyeshwa katika kadhia Afisa Forodha anaweza kongeza kodi inayotakiwa kulipwa au anamfungulia mashtaka ya udanganyifu ili aweze kulipa kodi sahihi pamoja na adhabu ya faini. Pale ambapo bidhaa zinatakiwa kulipiwa kodi kwa awamu, bidhaa hizo hupelekwa katika bohari maalum zilizoteuliwa na serikali ‘bonded warehouses’ na mteja kutakiwa kulipa kodi kadri anavyouza bidhaa zake.

492. Vituo vya mipakani

Mizigo inayoagizwa kupitia vituo va mipakani, mwenye mzigo anafuata utaratibu unaotumika Long room ambapo hujaziwa kadhia za Forodha na Afisa wa Forodha, mizigo kukaguliwana mwishowe kuingizwa nchini.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anaizungumziaje Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika eneo hili la ushuru na utaratibu unaotumika? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

By Jamhuri