RIPOTI YA RUSHWA YA JAJI WARIOBA – 40

Miti: Taratibu zinakiukwa

 

Upigaji marufuku baadhi ya vifaa vya uvuvi

709. Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mfumko mkubwa wa wafanyabiashara wengi wa samaki baharini na kwenye maziwa yetu. Hivyo wafanyabiashara huajiri vijana wa kuwavulia samaki kwa kutumia makokoro ambayo hunasa samaki wengi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na samaki wachanga.

Uvuvi wa kutumia makokoro unaharibu maeneo ya kuzaliana na kukulia samaki na umepigwa marufuku. Hatua hii imezua manung’uniko kutoka kwa wafanyabiashara. Hata hivyo, hivi sasa samaki wanaopatikana ni wakubwa.

Aidha, elimu kwa umma kuhusu athari za uvuvi wa kutumia makokoro imesaidia kuwaelimisha wananchi hali halisi ya upatikanaji wa samaki na hivyo kupata ushirikiano mzuri wa kuhifadhi mazingira ya samaki. Pale ambapo wahalifu wanapatikana wanatoa rushwa ili wasikamatwe.

 

Kutofuatwa taratibu zilizowekwa

710. Miaka ya nyuma wawekezaji wengi katika sekta ya uvuvi walikuwa siyo raia wa Tanzania. Wengi wao na hasa wavuvi wa kamba ni Wagiriki. Kwa sasa wazalendo nao wanajihusisha na sekta hii hasa kwa kuingia ubia na Kampuni za nje.

Kutokana na kuchanganyikana kwa watu wenye mitizamo tofauti mfano Wagiriki ambao wanaamini kuwa Tanzania sheria hazitumiki, kumekuwepo na ukiukwaji wa taratibu hasa pale rasilimali iliyopo ni chache. Hatua zinazochukuliwa za kudhibiti rasilimali zinaonekana kama ni mbinu ya kuwaangusha kibiashara, hivyo nao hutoa rushwa ili kukwepa taratibu zilizowekwa.

711. Baadhi ya waombaji wa leseni za uvuvi hupenda kutumia mawakala badala ya kuzishughulikia wenyewe. Kutokufuata utaratibu wa maombi ya leseni kumesababisha waombaji kukosa leseni, kuchelewa kupata leseni au hata kutapeliwa fedha zao kwa kisingizio kuwa mtoaji leseni anataka kitu kidogo ndipo atoe leseni.

Kutotolewa leseni za kuuza nje ya nchi samaki wavuliwao ukanda wa bahari

712. Yamekuwepo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara dhidi ya uamuzi wa Idara kukataa kuwapa leseni za kuuza nje ya nchi samaki wabichi wavuliwao baharini. Kulingana na taratibu za Idara kusitishwa kutolewa kwa leseni hizo kumezingatia mambo yafuatayo:

(i) Kiasi cha samaki wanaovuliwa ni kidogo ulikinganisha na mahitaji ya walaji hapa nchini.

(ii) Bei ya samaki hapa nchini ni kubwa hivyo wafanyabiashara wanahimizwa wauze hapa nchini.

(iii) Samaki hawa wanavuliwa na wavuvi wadogo wadogo na ndiyo chanzo cha kitoweo kwa wananchi wengi.

(iv) Mwekezaji anahimizwa kuuza nje ya nchi bidhaa za samaki (value added fish products) na siyo samaki wabichi ili kuipatia nchi fedha za kigeni na kuongeza ajira. Hata hivyo kuna baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara ambao huvua samaki usiku na kuwapeleka kuwauza nchi jirani bila kujali mahitaji ya wenyeji.

Hiki ni kitendo cha wazi cha uvunjaji wa sheria za nchi na pia ni cha hujuma kwa taifa. Tatizo la udhibiti wa biashara hii  linakuwa gumu zaidi kwa kuwa Idara haina boti za kufuatilia mienendo ya wavuvi katika maeneo ya kuvulia.

Zaidi ya haya tatizo hili limeongezeka kwa kuwepo na baadhi ya watumishi wa Idara wasio waaminifu ambao hujali maslahi yao binafsi kwa kusimamia upande wa wafanyabiashara kuliko kuangalia maslahi ya Taifa.

 

Kukosekana uwiano kati ya viwanda na rasilimali iliyopo

713. Hivi karibuni Ukanda wa Ziwa Victoria umeshuhudia mfumuko mkubwa wa kuanzishwa kwa viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Hadi sasa kuna viwanda vipatavyo kumi na saba (17). Athari ya kufunguliwa kwa viwanda hivi bado haijawa ya kutisha, lakini katika kipindi kifupi kijacho hali ya kuwepo kwa rasilimali ziwani itakuwa hatarini sana.

Baadhi ya aina za samaki zitatoweka kabisa na wale watakaokuwepo uzalishaji wao utakuwa mdogo sana. Kwa mfano miaka ya nyuma kulikuwa na sangara wengi sana wakubwa na wenye uzito mkubwa. Pamoja na ripoti za wataalamu kwamba kiasi cha samaki walioko ziwani hawataweza kuhimili malighafi ya viwanda hivyo, wawekezaji wanaendelea kuruhusiwa kujenga viwanda kwa kuzingatia mapendekezo ya wanasiasa.

 

Mgongano wa mamlaka

 714. Kiutendaji Afisa Uvuvi wa Wilaya yuko chini ya Halmashauri inayohusika na wakati huo huo anapaswa kusimamia Sheria ya uvuvi wilayani kwake. Kumekuwepo na miingiliano na migongano ya kiuendaji katika mamlaka hizi mbili na hivyo kumpunguzia Afisa huyu uwezo wake wa kuwajibika kwa (sheria ya uvuvi) Idara ya Uvuvi.

715. Pamekuwepo na kutoelewana na kati ya maofisa uvuvi na uongozi wa Halmashauri hasa katika kutoa leseni za biashara ya mazao ya uvuvi na kudhibiti ubora na wingi wa mazao yanayohusika. Kwa mfano, mwaka huu 1996 ugomvi uliotokea kati ya uongozi wa  Halmashauri wa Wilaya ya Rufiji ambapo uongozi huo ulimkataa Afisa Uvuvi wa Wilaya kutokana na msimamo wake imara katika kusimamia sheria na kanuni za uvuvi wa kamba. Afisa huyo alihamishiwa Bagamoyo.

 

Mgawanyo wa Mapato

716. Katika kuendeleza shughuli za uvuvi katika wilaya, katika makubaliano ya mgawanyo wa mapato kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, Halmashauri za Wilaya huchukua sehemu kubwa ya mapato yanayotokana  na shughuli za uvuvi pamoja na biashara ya samaki, lakini Halmashauri hizo hazitengi fedha zozote za uendeleza sekta hii katika maeneo yao kama vile kuiimarisha vituo vya kupokelea samaki au kutenga fedha kwa ajili ya doria.

Msukumo mkubwa kwenye Halmashauri umekuwa ni kukusanya kodi kwa ajili ya kulipa posho na marupururu ya uongozi wa Wilaya pamoja na madiwani. Katika baadhi ya wilaya, maofisa uvuvi wamekuwa wanakaa muda mrefu (hadi miezi 6) bila kulipwa mishahara.

 

Uuzaji/uvushaji samaki nje ya nchi

717. Vituo vya mipakani, viwanja vya ndege na bandari vinahusika katika kudhibiti bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi. Kwa kutoa rushwa kwa maafisa forodha wasio waadilifu, wauzaji samaki nje ya nchi hupitisha mizigo bila hati hizo kutumika kupitisha mizigo zaidi ya mara moja pamoja na kuidhinisha mizigo kusafirishwa nje ya nchi bila ya kuwa na hati halali.

 

Uhaba wa vitendea kazi

718. Upungufu wa vitendea kazi hasa katika Halmashauri kunaleta usumbufu kwa waombaji wa leseni na hivyo kuweka mwanya wa rushwa. Maafisa wasio waaminifu wameutumia uhaba huu kama njia ya kujipatia kipato cha nyongeza kisicho halali.

 

MAPENDEKEZO

719. Tume inapendekeza kama ifuatavyo:

(i) Maslahi ya watumishi yarekebishwe ili yalingane na gharama za maisha. Hatua hii itawahamasisha kutekeleza majukumu kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

(ii) Idara ipewe vitendea kazi vya kutosha ili kuwezesha huduma kutolewa kwa haraka.

(iii) Miiko na maadili ya kazi yafuatwe.

(iv) Vyombo vya serikali vishirikiane katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa.

(v) Ushauri wa wataalamu kuhusu uwezekano au hali halisi ya kushuka kwa uzalishaji uzingatiwe. Aidha, wanasiasa wawe na mwelekeo wa kukubali ushauri wa kitaalamu. Suala hili linahusu pia vibali vitolewavyo na kituo cha uwekezaji. Hii ina maana kwamba uwekezaji uende sambamba na uzalishaji. Pamoja na haya, sera ya kuhifadhi mazingira iwe ni wajibu kwa wote.

(vi) Uandaliwe utaratibu na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata nafasi ya kuvuna rasilimali ya majini kufuatana na ushauri wakitaalamu. Pili wataalamu wetu watenge ama maeneo na kuainisha ukubwa wa vyombo vya uvuvi au njia nyingine yoyote ambayo inampa mwananchi upendeleo wa kuvuna rasilimali kwa chakula na biashara. Uwekezaji wa wageni katika eneo hili ufanywe kufuatana na kuzingatia ushauri huu wa wataalamu. Ushauri huu wa wataalamu uzingatie vile vile maoni ya wavuvi wananchi.

(vii) Wanaopewa leseni za kuuza samaki au kamba nje ya nchi wangedhibitiwa kwa karibu ili kuhakikisha kwamba malipo yanafika nchini. Hii inaweza kufanyika kwa kuhakikisha kwamba malipo yote yanafanyika kwa kupitia “designated account” ya mhusika ambamo “Letter of Credit’ zote zitatakiwa kupitia.

(viii) Wafanyabiashara wa nje wanaopewa leseni wakiwa na meli za uvuvi wapewe masharti kuwa waendapo kuvua wawe na Afisa Mdhibiti wa Serikali ndani ya meli mpaka warudi bandarini. Afisa huyu atawajibika kutoa takwimu sahihi za uvuvi unaofanyika baharini. Shehena ya kupelekwa nje ipitie  utaratibu wa “Export Procedures” na “designated account” za mhusika. Hii itahakikisha kuwa “exports” za sekta hii inachangia kwenye uchumi wa nchi ipasavyo.

(ix) Mamlaka zote zinazohusika katika miliki ya rasilimali za majini popote nchini zisiruhusiwe kufanya maamuzi yoyote bila ya kuzingatia ushauri wa Afisa Uvuvi. Maafisa wanaohusika wahimizwe kuwa waadilifu katika ushauri wao na kuwajibishwa pale inapobidi.

(x) Sheria za Uvuvi na Kanuni zake zirekebishwe pale inapohitajika kubana wale wanaotumia mianya ya sheria kuinyima nchi mapato.

(xi) Usimamizi wa kubana wahalifu katika uvuvi haramu uimarishwe na kutiliwa mkazo. Pia mamlaka zote zinazohusika ziandae mpangilio mzuri wa elimu kwa umma kuhusu athari za uvuvi haramu, kama wa kutumia mabomu,  makokoro na njia nyinginezo.

(xii) Kuwa na doria inayoaminika katika Bahari na maziwa – “Coast Guards.” Hiki kitengo, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kitajumuisha kazi za kipolisi, ushuru, ulinzi na usalama, ambacho kitachukua nafasi ya Polisi wa Majini na KMKM.

 

C: Idara ya Misitu na Nyuki

720. Idara ya Misitu na Nyuki ina jukumu la kusimamia na kuendeleza misitu na matumizi ya mazao ya misitu hapa nchini. Utekelezaji wa majukumu haya unafanywa na Idara kwa kufuatana na Sheria za Misitu Sura 389 na Sheria za Usafirishaji wa mazao ya Misitu Sura 288.

721. Majukumu mengine ya Idara hii ni kutoa leseni na vibali vya kutumia misitu au mazao yake. Jukumu la utoaji wa leseni na vibali kisheria ni la Mkurugenzi wa Misitu na Afisa yeyote ambaye amepewa mamlaka hayo na Mkurugenzi wa Misitu. Chini ya Sheria hii Halmashauri za Wilaya zimepewa mamlaka ya kutoa leseni za matumizi ya misitu au mazao yake katika hifadhi za Halmashauri ambayo yanaimiliki na kuitunza. Aidha, mameneja wa mashamba ya miti na misitu iliyohifadhiwa wamepewa mamlaka ya kutoa leseni na vibali vya kuvuna miti na mazao ya misitu katika mashamba wanayosimamia.

 

Aina za Misitu

722. Chini ya Sheria za Misitu Na. 389, misitu imegawanywa katika sehemu kuu tatu:

(i) Misitu ya Serikali Kuu (Central Government Forest Reserves)

(ii) Misitu ya Halmashauri ya Wilaya (Local Government Forest Reserves)

(iii)Misitu isiyohifadhiwa (Unreserved Forest Areas)

 

Aina za Leseni

723. Vifungu 15 mpaka 17 vya Sheria za Misitu Sura Na. 389 vinatamka wazi kwamba mtu yeyote ambaye anataka kuvuna miti, kuishi au kufanya shughuli yoyote ile katika misitu iliyohifadhiwa na isiyohifadhiwa ni lazima awe na leseni au kibali halali.

Leseni ya kukata, kukusanya na kutoa mazao ya misitu (licence to collect and remove forest produce FD Licence No.1)

724. Leseni hii inahusu uvunaji wa mazao yote ya misitu yaliyopo ndani ya misitu iliyohifadhiwa au maeneo yasiyohifadhiwa (unreserved forest areas). Mwombaji hapana budi awe na leseni ya biashara kabla ya kupata leseni hii.

 

Leseni ya kuishi katika eneo la msitu uliohifadhiwa kisheria (Licence to reside FD Licence No. 4)

725. Leseni hii inamhusu mtu anayeomba kuishi kwa muda kwa shughuli maalumu katika eneo lililopo ndani ya msitu uliohifadhiwa kwa mfano watafiti na inadumu kwa muda wa mwaka mmoja.

 

Leseni za kulisha mifugo katika misitu iliyohifadhiwa kisheria (Licence to graze FD Licence No. 2)

726. Leseni hii inamhusu mtu anayeomba kufuga au kulisha mifugo kwa muda katika misitu iliyohifadhiwa na hutolewa na Idara baada ya kudhihirika kwamba uchungaji hautaathiri mazingira. Leseni hii hutolewa kwa mwezi.

 

Leseni ya kulima katika misitu iliyohifadhiwa (FD Lecence No. 3)

727. Leseni hii inahusu idhini kwa mtu anayeomba kulima kwa muda katika eneo la msitu unaohifadhiwa. Baada ya kuvuna miti kwenye mashamba ya miti waombaji huruhusiwa kulima kwenye mashamba hayo wakati yanasubiri kuoteshwa miti mingine na hutolewa kwa msimu wa kilimo.

 

728. Vibali

Idara ya Misitu na Nyuki inatoa vibali vifuatavyo:

 

Vibali vya mauzo ya Mazoa ya Misitu nje ya nchi

(i) Hiki ni kibali cha kuruhusu aina ya mazao yatakayosafirishwa nje (Approval for Export of  Forest Products). Kibali hiki kinatoa utambulisho wa mazao ambayo mwombaji ameomba na yamekubaliwa kusafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi.

 

(ii) “Permit for export of graded timber

Kibali hiki kinathibitisha kukaguliwa na kutoa idhini ya zao hilo kusafirishwa nchi za nje.

729. Vibali vya kuweka viwanda vya kupasua mbao katika mashamba ya miti au kupewa leseni kwa mwombaji kuvuna katika mashamba ya miti.

730. Vibali vingine vinahusu utaratibu wa kuruhusu kuingia katika misitu iliyohifadhiwa au mashamba ya miti kwa shughuli ambayo haihusu uvunaji kama utafiti, camping, ujenzi wa mabomba ya maji n.k.

 

Taratibu za upatikanaji vibali

731. Kama ilivyo katika utoaji wa leseni, utoaji wa vibali hivi unatolewa na Mkurugenzi wa Misutu au mtu aliyepewa mamlaka hayo kwa niaba yake.

732. Masharti ya kupata vibali hivi ni sawa na masharti yanayotumika katika upatikanaji wa leseni, kama ilivyoelezwa hapo nyuma.

 

Masharti ya Matumizi ya Leseni na Vibali

733. Kila leseni ina masharti yake nyuma, ambayo mwenye leseni anapaswa kuyafuata.

 

Matatizo yaliobainishwa na uchambuzi wa Tume

Ongezeko la watu na mahitaji yao

734. Ongezeko la watu nchini limesababisha kuwepo kwa ongezeko la mahitaji mbalimbali ya mazao ya misitu. Kwa mfano kumekuwapo na ongezeko la mahitaji ya miti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi, kuni, mkaa n.k. Hali hii imesababisha kuwepo kwa ugumu wa kutoa leseni kwa wote wanaoomba na katika sehemu wanazozitaka.

 

Umaskini miongoni mwa wananchi

735. Umaskini uliopo miongoni mwa wananchi umewafanya waone kuwa misitu ni chanzo cha mapato. Hivyo wananchi wengi wanatumia misitu kwa shughuli mbalimbali kama vile kukata kuni, fito, mbao, kuchoma mkaa n.k. hali hii inaleta shinikizo kubwa katika matumizi ya misitu.

 

Udhaifu wa usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu

736. Kisheria Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki ndiye msimamizi mkuu wa maliasili ya misitu na nyuki kwa nchi nzima. Kutokana na muundo ambao umegawa mamlaka ya kushughulikia misitu katika makundi matatu yaani Serikali Kuu, Mikoa na Halmashauri za Wilaya kumefanya kusiwe na mshikamano mzuri katika kusimamia maliasili hii.

Kumekuwepo na usimamizi duni wa shughuli za misitu na utoaji leseni na vibali mbalimbali miongoni mwa mamlaka hizo. Aidha, kumetokea migongano ya madaraka kati ya maafisa maliasili na maafisa misitu wa wilaya katika kusimamia shughuli za misitu kwani Afisa (W) anawajibika kwa Halmashauri ya Wilaya wakati huo huo anapaswa kusimamia Sheria za Misitu wilayani mwake.

 

Upungufu wa watumishi na vitendea kazi

737. Idara inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa nyenzo za kufanyia kazi na hivyo kupunguza uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake. Hii ni pamoja na kushindwa kwenda kukagua eneo linaloombea leseni ya kukata miti.

738. Upungufu wa watumishi na watumishi wenye uwezo na ujuzi wa kutosha hasa waliopo wilayani umeathiri utendaji wao wa kazi kwa ufanisi.

 

Taratibu za udhibiti

739. Sheria ya Misitu inahusu misitu ya hifadhi. Misitu isiyohifadhiwa inalindwa na sera ya kuhifadhi mazingira ambayo haina makali ya kudhibiti uvunaji haramu katika misitu hiyo. Upungufu huu wa kisheria umeleta athari kwa nchi nzima kwani misitu mingi isiyohifadhiwa kisheria imekuwa ikivunwa bila udhibiti kutoka kwenye mamlaka zinazohusika.

 

Maeneo yenye mianya ya rushwa

740. Mianya ya rushwa iko katika utoaji wa leseni au vibali vya kulima katika mashamba ya miti yaliyopo katika mikoa yenye uhaba wa ardhi kama Kilimanjaro na Arusha.

 741.  Kuna ulegevu na usimamizi hafifu katika uvunaji na hasa kwa kuruhusu uvunaji bila leseni au kwa malipo madogo. Kinachofanyika hapa na Afisa Misitu kutoa kibali cha uvunaji kwa mtu asiyekuwa na leseni na kisha kupokea malipo kwa ajili yake binafsi bila kujali hasara anayoliingizia taifa.

742. Maafisa Misitu huruhusu uvunaji bila ya leseni au kuongeza eneo la uvunaji bila kuwasilisha mapato serikalini.

743. Pale ambapo mfanyabiashara anakamatwa kwa kosa la uvunaji bila ya leseni au kibali hutoa rushwa ili asichukuliwe hatua za kisheria.

744. Baadhi ya Maafisa Misitu kujipangia maeneo  ya kuvuna miti bila leseni halali au kwa malipo madogo ya leseni isiyostahili. Aidha, maeneo hayo yanaweza kugawiwa kwa wateja kwa kutoa malipo ambayo nayo hayawasilishwi serikalini.

745.Vibali vya uvunaji miti katika mashamba ya migazi ya Longuza na Mtibwa vimekuwa vinatolewa baada ya waombaji kutoa chochote kwa Maafisa Misitu – Makao Makuu.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alipendekeza nini katika kudhibiti uvunaji holela wa mazao ya misitu? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu uleule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.