RIPOTI YA RUSHWA YA JAJI WARIOBA – 42

2.     Mapokezi kuu
Mapokezi Kuu ndiyo kitovu cha kupokelea wagonjwa wote wanaopelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi. Wagonjwa hao ni wale ambao maradhi yao yanahitaji utaalamu wa juu au vifaa vya kisasa ambavyo havipatikani hospitali nyingine zaidi ya Muhimbili.
 Wagonjwa wanaopokelewa kutoka hospitali za mikoa na wilaya kwa Mkoa wa Dar es Salaam, hospitali za watu binafsi, mashirika ya umma na ya dini na wale wanaojipeleka wenyewe kutokana na kukosekana kwa hospitali ya Serikali katika maeneo ya karibu na Muhimbili ambao idadi yao ni wachache.
 Kiutaratibu kila mgonjwa anayepelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi anapaswa kuwa na maelezo rasmi kutoka kwa daktari ikieleza ni kwa nini amaeamua kumpeleka Muhimbili.
 Aidha, mgonjwa anatakiwa awe na msindikizaji wa karibu kama vile ndugu na jina na taarifa zake zinaingizwa kwenye rejista ili endapo kutakuwa na tatizo aweze kujulishwa yeye au ndugu wa mgonjwa waweze kujulishwa au wapatikane kwa urahisi. Kwa wagonjwa wanaotoka mikoani wao wanasindikizwa na muuguzi kutoka hospitali inayohusika.
 Kundi la pili la wagonjwa ni la wale ambao wanapelekwa chini ya usindikizaji wa Polisi. Hawa ni wagonjwa wa akili kama vile vichaa, watu wanaookotwa na wale waliopata ajali kama vile za barabarani n.k. kwa upande wa kundi hili polisi anapaswa kuandikwa jina na namba zake kwenye rejista za mapokezi kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji.
 
Utaratibu unaofuatwa
1. Mgonjwa akifika anapokelewa na wauguzi au wahudumu (attendants) ambao humpokea mgonjwa na kumweka kwenye kiti chenye magurudumu au kitanda.
2.     Mgonjwa na msindikizaji wanaandikishwa kwenye rejista ya mapokezi.
3.     Mgonjwa akishaandikishwa anapelekwa kwa daktari kufuatana na hali yake. Wagonjwa ambao hali zao ni mbaya, waliopata ajali na watoto hupata matibabu katika sehemu iitwayo “hot cases” na wale ambao hali zao siyo mbaya sana wanatibiwa sehemu iitwayo “cold cases”.
4.     Mgonjwa anapofikishwa kwa daktari anafunguliwa kadi na hapo anafanyiwa uchunguzi ambao madaktari wanatumia kufanya uamuzi juu ya matibabu yatakiwayo.
5.     Baada ya uamuzi au maelekezo kutolewa, mgonjwa anapelekwa wodini au chumba cha mapumziko kwa ajili ya kufuatilia hali yake au anatibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
 Ingawa utaratibu unaelekeza kuwa mgonjwa ahudumiwe bila kucheleweshwa wapo wagonjwa wanaokaa sehemu ya mapokezi kwa muda mrefu kabla ya kupelekwa kwa daktari. Aidha, baada ya mgonjwa kuandikiwa kulazwa wodini kama hakutoa rushwa hatapata mhudumu wa kumpeleka huko. Wako wagonjwa mahututi wanaokaa sehemu ya mapokezi muda mrefu bila kupelekwa wodini.
 
Wodi za kulaza wagonjwa
 Mgonjwa anayeandikiwa kulazwa wodini anapelekwa huko na wahudumu na kusindikizwa na ndugu au jamaa zake. Wagonjwa hupangiwa wodi kulingana na magonjwa yao. Mgonjwa akishafikishwa wodini anaingizwa kwenye rejista ya wagonjwa waliopokelewa kwa siku ile. Baada ya hapo anapewa kitanda na huduma nyingine kufuatana na maelekezo ya daktari.
 Mgonjwa ataendelea kuwepo wodini hadi hapo daktari atakaporidhika kuwa mgonjwa anaweza kutolewa na kuendelea kujiuguza akiwa nyumbani. Kuna tuhuma kuwa wagonjwa wengine hutolewa wodini na madaktari kabla hali zao hazijawa nzuri kwa sababu hawakupewa hongo.
 Hatua nyingine muhimu katika kuhakikisha kuwa mgonjwa anapatiwa matibabu halisi kwa maradhi yake ni sehemu za vipimo kama vile maabara, X-rays n.k.
 
Utaratibu wa vipimo
(i) Maabara
Hospitali ya Muhimbili ina maabara kuu moja na maabara ndogo ndogo katika kila wodi. Maabara kuu inatoa huduma za vipimo kwa wagonjwa wote wa nje na wale walioko mawodini ambao vipimo vitakiwavyo havitolewi katika maabara ya wodini. Huduma hii hutolewa kwa agizo la daktari. Maabara hizi hutoa huduma kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 2 usiku.
 
Wagonjwa wa wodini
Daktari anapomwona mgonjwa na kuelekeza kufanyiwa vipimo vya maabara, mgonjwa huyu hupelekwa na muuguzi hadi maabara ambapo wataalamu wa maabara watamshughulikia na kisha kurudishwa wodini. Kwa wale wagonjwa wenye hali mbaya, muuguzi huchukua vipimo vyao na kuvipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi. Baadaye muuguzi hufuatilia majibu kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa maabara.
Kutokana na utaratibu wa huduma za hospitali hii, maabara za wodini ni kwa ajili ya wagonjwa walioko mawodini tu. Kwa kuwa maabara hizi zinajulikana ni kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa ndani wapo baadhi ya watu ama kwa kufahamiana au kwa njia ya rushwa hupatiwa huduma katika maabara hizi. Baadhi yao wanakuwa hawajamwona daktari.

Maabara Kuu
Maabara Kuu inawahudumia wagonjwa wa ndani na nje. Maabara hii inatoa huduma kwa saa ishirini na nne kwa wataalamu wake kupangiana zamu.
1. Mgonjwa anapopeleka vipimo vyake anakaa kwenye mstari hadi zamu yake inapofika.
2. Mtaalamu anapokea vipimo pamoja na fomu inayoelekeza uchunguzi utakiwao na kuviweka mezani ambapo huondolewa baadaye na kupelekwa maabara.
3. Mgonjwa ataendelea kusubiri majibu kwa vile vipimo ambavyo havihitaji uchunguzi wa muda mrefu au ataambiwa siku ya kurudi kwa vipimo  vichukuavyo muda mrefu kufanyiwa uchunguzi.
4. Mgonjwa akipata majibu anayarudisha kwa daktari. Kwa wagonjwa walioko wodini majibu yao yanachukuliwa na muuguzi na kuingizwa kwenye jalada la mgonjwa. Kumekuwepo na malalamiko kwamba bila kutoa hongo vipimo havishughulikiwi mapema au majibu hayatoki mapema.
 
II. sehemu ya kupiga picha za X-ray
Sehemu ya kupiga X-ray inatoa huduma kwa wagonjwa waliopo mawodini na wale wa nje. Kiutaratibu ni kuwa wagonjwa waliopo wodini wanahudumiwa kwanza.
 1. Mgonjwa anapoandikiwa na daktari kupiga picha ya X-ray anapeleka fomu yake dirishani ambapo anaingizwa jina lake kwenye rejista na kuelekezwa sehemu inayohusika na picha kulingana na maelekezo ya daktari.
2. Mgonjwa atasubiri mstarini mpaka zamu yake ifike.
3. Mgonjwa anaitwa ndani na kupigwa picha na kisha kupewa picha ambayo huipeleka kwa daktari.
 Katika sehemu hii kuna vitendo vya rushwa vinavyofanyika. Kwanza ni vile vya kutoa upendeleo kwa mgonjwa kwa msingi wa undugu, rafiki au kwa kufahamiana na pili ni kwa kupokea rushwa.
 Utaratibu wa kuomba rushwa ni kwamba mgonjwa anaambiwa daktari anataka Sh. 5,000/- ama anaambiwa hakuna “film” au fanya maarifa ili atoe fedha. Fedha zinatolewa kwa wapiga picha wa X-ray. Kwenye vipimo  vingine vya mionzi kama vile “endoscopy” au “B-meal” mgonjwa anadaiwa fedha kati ya Sh 7,000/- hadi 10,000/- ili aweze kuchukuliwa vipimo hivyo. Fedha zikitolewa mgonjwa hapewi risiti.
 Tuhuma hizi ni ngumu kuzithibitisha bila kufanya mtego kwani mara zote hii ni siri ya mtoa huduma na mhudumiwa.
 Taratibu hizi zinaonekana kuwa fupi na zisizo na hitilafu. Hali sivyo ilivyo kiutendaji. Kutokana  na upungufu mkubwa wa madawa, vifaa na vitendea kazi muhimu wagonjwa wanalazimishwa kutoa rushwa ili wahudumiwe.
 Hali inakuwa mbaya zaidi kwa wale wasio na uwezo wa kuhonga kwa sababu hawapatiwi huduma ipasavyo na endapo atahudumiwa huduma itatolewa kwa masimango kinyume na kiapo walichokula cha kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wao wote.
 
766.  MAPENDEKEZO:
 (i) Sera ya kuruhusu madaktari walioajiriwa katika Hospitali za Serikali kuwa na zahanati na hospitali binafsi iangaliwe upya. Madaktari wasiruhusiwe kuwa na hospitali zao binafsi.
(ii) Wauguzi wanaouza dawa au vifaa wodini watolewe taarifa na kutakiwa kujieleza. Hatua hii iwe ni pamoja na kuwachukuliwa hatua za kinidhamu au kisheria pale inapobidi kufanya hivyo.
(iii) Utaratibu wa nidhamu uangaliwe upya kwa madhumuni ya kuwapa waganga wakuu mamlaka ya kudhibiti nidhamu ya watumishi walio chini yao badala ya wao kuwa wanapeleka mapendekezo yao wizarani.
(iv) Wananchi waelimishwe wazijue haki zao. Hii ni pamoja na kujua sehemu ya kupeleka malalamiko yao wanapodaiwa rushwa na kisha apatiwe huduma anayohitaji bila ya vitisho.
(v) Hospitali na maduka binafsi yanayouza madawa na vifaa vya hospitali ziwe zinakaguliwa mara kwa mara ili kudhibiti wizi wa madawa na vifaa vya serikali.
(vi) Maslahi ya mishahara ya madaktari na watumishi wa Sekta ya Afya yaongezwe aweze kukidhi mahitaji yao ya msingi ili waweze kufanya kazi zao kwa  bidii, uadilifu na uaminifu.
(vii) Watumishi wasisitiziwe umuhimu na athari za kutokuzingatia na kufuata maadili ya kazi zao.
(viii) Watumishi na madaktari wavae vitambulisho ili iwe rahisi kumtambua na kumtolea taarifa mdai au mpokea rushwa.
(ix) Hospitali za wilaya na mikoa ziimarishe kiutaalamu, vifaa na madawa ili Hospitali ya Muhimbili iwe ni kwa ajili ya rufaa tu. Hii itapunguza msongamano wa wagonjwa na hivyo kuimarisha huduma zitolewazo.

Leo tumechapisha sehemu ya 42 na ya mwisho ya Ripoti ya Jaji Joseph Sinde Warioba. Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu uleule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Mwisho. Mhariri.

685 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons