ROMA, STAMINA WAITWA BASATA

ZIKIWA zimepita siku tatu tangu wakali wawili wa hip hop Bongo wanaounda kundi la ROSTAM, Roma Mkatoliki na Stamina kuachia wimbo wao mpya wa ‘PARAPANDA’ wakivaa uhusika wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Kingunge Ngombaremwiru, wawili hao wameitwa katika ofisi za Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) leo Agosti 6, 2018 kupigwa msasa wa sheria na kanuni mpya za Baraza hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza amethibitisha taarifa hizo ambapo amedai kuwa Roma na Stamina wameitwa kwa lengo la kujadili kanuni mpya huku akieleza kuwa sio jambo la kushangaza kwani wao ni kama nyumba ya wasanii.

“Ni kweli wamekuja BASATA, na kimsingi hapa ni nyumbani kwao, kama wasanii wengine hapa ni nyumbani kwao na leo tulikuwa tunapitia kanuni na kama kutakuwa na jipya basi tutafahamishana,“ amesema Mngereza na kusisitiza kuwa endapo kutakuwa na jambo lingine BASATA watatoa taarifa zaidi baadae.

Wiki iliyopita Roma Mkatoliki na Stamina waliachia ngoma yao mpya ya ‘PARAPANDA’ ngoma ambayo kwenye baadhi ya mistari kuna sehemu inasema “ROMA – Kwani anayesimamia sanaa ni nani?… STAMINA anajibu- Lipo Baraza ila wasanii wanaishi uwani.“.