Ruge Mutahaba umeondoka, umetuachia funzo

Ni wiki moja sasa tangu familia, Clouds Media Group na taifa wampoteze kijana mashuhuri, Ruge Mutahaba. Baada ya wiki moja sasa tangu kifo chake, nashindwa niandike nini? Lakini sikosi cha kuandika, maana maisha ya Ruge yalikuwa kama Msahafu ama Biblia, ambako kila anayesoma anaambulia chochote.

Kwanza nianze na umati mkubwa uliojitokeza katika barabara zote ambazo msafara uliobeba jeneza lake ulipita. Kitendo hicho kikanikumbusha miaka ishirini iliyopita, ambapo nilishuhudia umati kama huo wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipofariki dunia.

Ruge Mutahaba hakuwa hata mjumbe wa nyumba kumi, isipokuwa moyo wake wa dhahabu na kuwatendea mema wanadamu. Wahenga walinena ‘tenda wema uende zako, usingoje shukrani’, ama kweli Ruge alitenda wema na kuondoka zake, shukrani zimeshuhudiwa na familia pamoja na Watanzania wote.

Kwa nini nasema Ruge ameondoka na kutuachia funzo? Ni dhahiri kwamba Ruge amegusa maisha ya watu wengi kwa namna mbalimbali, ndiyo maana utaona siku ya Ijumaa wakati mwili wake umewasili na kupelekwa katika Hospitali ya Lugalo, kina mama walikuwa wanatandika kanga zao ili apite.

 Jambo hilo linaashiria kwamba, Ruge alikuwa mtu aliyegusa maisha ya Watanzania wa hali zote, watu wa aina ya Ruge ni nadra sana kuzaliwa, wengine huzaliwa na kuharibiwa na mazingira. Lakini Ruge aliweza kuhimili kuvishinda vishawishi na kubaki kuwa Ruge! Pumzika kwa amani brother.

Jumanne ya Februari 26, majira ya saa mbili na robo nikiwa narudi nyumbani nikitokea ofisini, nikaona uzi kupitia mitandao ya kijamii kwamba ndugu yangu Rugemarila Mutahaba ametangulia mbele ya haki! Moyo wa binadamu umeumbwa kwa kuogopa taarifa mbaya hasa za kifo, tena cha mtu mnayefahamiana. Nikajawa hofu, huku nikijifariji kwamba Ruge amelala tu, hajafa.

Nikiwa kwenye mshtuko na mtanziko huo, ghafla kwenye simu yangu unaigia ujumbe wa Mfalme! Ujumbe ambao unathibitisha kifo, safari hii si kupitia taarifa za Gerson Msigwa, isipokuwa kupitia kwenye ukurasa wa twitter ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli. Kwa kweli umemwelezea Ruge vizuri sana, machozi yakanilengalenga.

Sikuwahi kufanya kazi na Ruge, isipokuwa nilipata fursa ya kuzungumza naye wakati nimehama kutoka The Citizen, gazeti la Kiingereza na kujiunga Gazeti la Jamhuri. Ninayakumbuka maneno yake, akiniambia nimepata mafanikio makubwa nikiwa The Citizen, na kwamba ilikuwa sahihi kupata changamoto mpya.

Wakati kila mtu akiniona mwendawazimu, Ruge aliniambia: “Brother usiwasikilize watu, hawataacha kusema…wewe songa mbele, kuna kitu kikubwa utaifanyia nchi yako.” Kwangu ujumbe huo unabaki kuwa mtihani mkubwa, maana Ruge amefariki dunia bila kuniambia kwamba kitu hicho kikubwa ni nini?

Pamoja na yote hayo, nikakumbuka jambo moja, mwanadamu awapo duniani na baada ya kuondoka, utakumbukwa kwa jambo gani? Baya ama zuri? Nikakumbuka tena kwamba Ruge hajafa, isipokuwa amelala tu! Maana ameacha alama nyingi ambazo kupitia hizo namwona akiendelea kuishi.

Jina Ruge katika tasnia ya burudani pamoja na mambo mengine ya kijamii ni sawa na maji! Usipoyanywa basi utayaoga, kama usipoyaoga basi hata chooni utachambia. Ruge ulikuwa zawadi kwa familia na ukoo wa Mutahaba, kwa tasnia ya habari ulikuwa nguzo na katika tasnia ya burudani ulikuwa ufunguo!

Tazama zawadi imepotea na nguzo imeanguka, lakini ufunguo umebaki! Kupitia kwako Ruge umewafungulia vijana wengi dunia kuwa wanachotaka! Bila ufunguo wako pengine leo vijana wengi wangekuwa kama kipofu asiyekuwa na fimbo nyeupe! Changamoto zingekuwa nyingi zaidi, lakini tazama leo umelala usingizi mzito lakini ufunguo umetuachia vijana, kikubwa ni kuutumia vizuri ili isije kutulazimu kubadili kitasa.

Kaka Ruge umeondoka, mdogo wako umeniachia funzo moja kubwa, roho ya kusamehe. Roho ambayo nimeona inatoka kwenye familia, maana hata mtoto wako wa kwanza, Mwachi Ruge, wakati anasoma wasifu wako, aliomba radhi kwa niaba yako kwa watu uliowakosea, lakini pia kutangaza msamaha kwa wakiokukosea.

Ruge katika maisha yako haukuruhusu chuki na ugomvi vikutawale, hata pale vilipotokea ulihakikisha vinakwisha na maisha mengine yasonge mbele! Ninakumbuka siku rais anazindua mradi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Hoima, Uganda. Pale ulitoa funzo kubwa kama lile alilolitoa Yesu Kristu akiwa amewambwa msalabani pamoja na wale wanyang’anyi wawili!

Rais alitaka Ruge usameheane na ‘Gavana’ wa Dar es Salaam, bila kinyongo tena kwa sura ya tabasamu ukaonyesha kukubali na kuishi kile ulichokiamini. Sitaki kuzungumzia suala la ugomvi uliokuwapo baina yako na Mbunge wa sasa wa Mbeya Mjini, ambaye baadaye mkashikana mikono na maisha yakaendelea! Moyo wa aina hiyo unapatikana vifuani mwa wanadamu wachache, pengine ulikuwa peke yako Ruge.

Ninasikitika, ninaandika mambo yanayokuhusu wakati hautapata fursa ya kuyasikia, lakini nafarijika kwamba kupitia mafunzo hayo machache kutoka kwako wachache miongoni mwetu tunaweza kujifunza kuwa kama Ruge.

Pumzika kwa amani, ninaendelea kuamini kwamba Mwenyezi Mungu amekuchukua baada ya kumaliza kazi ambayo alikutuma uje kuifanya hapa duniani! Amekuita ukafanye kazi nyingine huko mbinguni.

Jakaya Kikwete amlilia

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliyefika kutoa salamu za pole kwa familia ya Mutahaba, Mikocheni, jijini Dar es Salaam alisema nchi imepoteza mzalendo wa kweli.

Kikwete anasema Ruge tofauti na vijana wengine alikuwa akifanya mambo kwa ajili ya wengine.

“Ukimfuatilia utagundua alikuwa anashughulika tu kwa sababu ya wenzake. Angalia Fursa (semina za uhamasishaji ujasiriamali), Vijana Think Tank na mengine mengi, hakufanya haya kujinufaisha, aliishi vizuri, kwa hiyo sisi tujitahidi kufuata mfano wake,” anasema Kikwete.

January Makamba amzungumzia Ruge

Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Mazingira, January Makamba, anasema utu wa Ruge Mutahaba unapimwa katika yale aliyoacha duniani.

Anasema wengine wanaweza kuwa na vyeo, pesa na mali nyingi lakini asipate heshima kubwa kama aliyoipata aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media, Ruge.

Akitoa salamu za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Ruge, Makamba aliwapa moyo wazazi wa Ruge kuwa msiba huo usiwaumize kiasi cha kumkosea Mungu kwa sababu mtoto wao aliishi matendo mema.

Makamba alisema Ruge ameondoka kabla mambo mengi waliyopanga hayajafanyika.

“Nimelia peke yangu, nimelia kwa sababu sijalipa deni kubwa la heshima uliyonipa, ulinipa upendo wa dhati na tulipanga vitu fulani hivi lakini umeondoka kabla hatujafanya, nimechanganyikiwa,” anasema.

Kiongozi huyo aliyemaliza hotuba yake kwa kuimba wimbo wa ‘Helo Helo Tanzania’, alisema Ruge alipenda na aliagiza siku ya kuondoka duniani tuimbe.

“Ndoto na fursa ndiyo maneno mawili ambayo Ruge aliyapenda, msiba huu umetuunganisha Watanzania bila kujali vyama na msiba huo umetoa fursa ya ndoto yake kudumu.

“Leo tunatua bango la Ruge likisomeka vizuri, jiulize leo ukiondoka bango lako linasomekaje? Sisi kuja kwetu hapa tumekuja kumvisha taji la heshima, wengine tunaweza kuwa na madaraka ya vyeo, pesa nyingi na mali nyingi lakini tusipate heshima hii,” anasema Makamba.

Taarifa ya Clouds

Februari 26 usiku, uongozi wa Clouds Media Group ulitoa taarifa fupi kuhusu kifo hicho.

“Tunasikitika kutangaza kifo cha mmoja wa waasisi na Mkurugenzi wetu wa Vipindi na Uzalishaji hapa Clouds Media Group, Ndugu Ruge Mutahaba.

“Ruge ametutoka leo huko Afrika Kusini alikokuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu. Mioyo yetu imejeruhiwa. Tutaendelea kuwapa taarifa zote kuhusiana na msiba huu mzito,” ilieleza taarifa hiyo.

Rais John Magufuli

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli aliandika: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu, Ruge Mutahaba.

“Daima nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina.”

Historia ya ruge mutahaba

Ruge Mutahaba alizaliwa Mei Mosi, 1970 Brooklyn, New York, Marekani.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Arusha kuanzia darasa la kwanza hadi la sita kabla ya kuhamia Shule ya Msingi Mlimani, iliyopo Dar es Salaam kukamilisha elimu yake ya msingi.

Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam kwa masomo ya awali ya sekondari, kisha masomo ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Pugu.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha San Jose cha nchini Marekani kusomea shahada za kwanza katika masoko na fedha.

Wakati akiendelea na masomo nchini Marekani, mshirika wake kibiashara, Joseph Kusaga, alikuwa akiendesha Klabu ya Disko la Usiku (Night Club Disco), ambayo pia ilijulikana kama Clouds Disco.

Hivyo, Ruge akawa mgavi pekee wa vifaa vya kuendeshea klabu hiyo ya usiku, yaani akiifanya kazi hiyo akiwa nchini Marekani.

Wakati aliporudi Tanzania baada ya kukamilisha masomo yake ya chuo kikuu, aliunganisha nguvu na Kusaga kuanzisha Clouds Media Group (CMG).

Marehemu Ruge ameacha watoto watano.

639 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons