Sekta binafsi isionekane kuwa ni maadui wa taifa

Wadau wameisikia bajeti kuu ya Serikali. Imepokewa kwa mitazamo tofauti. Wapo waliopongeza, na wapo waliokosoa. Huo ni utaratibu wa kawaida kwani hakuna jambo linaloweza kupendwa au kuchukiwa na wote.

Pamoja na kutoa unafuu kwa maeneo mbalimbali, bado tunaamini Serikali inapaswa kuendelea kujenga mazingira rafiki zaidi kati yake na sekta binafsi. Sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa taifa lolote katika ulimwengu wa leo. Hakutatokea wakati wowote ambao Serikali inaweza kujitenga na sekta hiyo na ikatarajia kukuza uchumi. Hakuna.

Kuna dhana potofu miongoni mwa baadhi ya watumishi na viongozi serikalini kuiona sekta binafsi kuwa si lolote, au chochote katika ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na hadi taifa. Mara kadhaa sekta hii imeonekana au kuchukuliwa kuwa ni ‘wezi’ wanaostahili kukomolewa kwa kuwekewa vikwazo, hasa kodi.

Tunaomba Serikali ihakikishe inafanya kila yanayowezekana ili sekta binafsi iweze kustawi na hivyo kuchochea ukuaji uchumi.

Kuna kodi nyingi zinazolalamikiwa na sekta binafsi, na kwa sababu hiyo baadhi ya wawekezaji- wakubwa kwa wadogo, ama wamefunga, au wanatamani kufunga biashara. Tunayo mifano hali ya baadhi ya wawekezaji waliohama au waliolazimika kupunguza uwekezaji wao na kwenda kuwekeza nchi jirani.

Sasa tunaona baadhi ya malori mengi yenye namba za usajili za nchi jirani, lakini wamiliki wake ni Watanzania. Jambo hili linapaswa kuwafikirisha watunga sera ili waweze kubaini sababu zinazowakimbiza wawekezaji hao, na namna ya kuwabakiza nchini. Hatuamini kama wanakimbia kwa sababu ya kutakiwa kulipa kodi, bali wanafanya hivyo kwa sababu ya ukubwa na utitiri wa kodi nchini mwetu.

Sekta binafsi inapoimarika huo unakuwa mwanzo wa Serikali kukusanya kodi kwa kiwango kikubwa. Tumeona mfano wa wauza ving’amuzi fulani ambao awali bei zao zilikuwa hazishikiki, lakini sasa wamepunguza na hivyo kuwavutia wateja wengi. Kwa njia hiyo tunaamini mapato yao yamepanda.

Tunaishauri Serikali ifanye hivyo. Ipunguze kodi ili watu wengi waweze kufungua biashara na waitikie ulipaji kodi kwa hiari. Tunashauri pia hatua kama hizo zifanywe kwenye viwanja vya ndege ili kushawishi ndege nyingi na kubwa kutua nchini moja kwa moja kuleta watalii.

Matumaini yetu ni kuona mwitikio huu wa Serikali unaelekezwa katika kurekebisha maeneo yote yanayolalamikiwa na sekta binafsi. Bila sekta binafsi kuwa imara uchumi hauwezi kustawi.

 

1183 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons