Serengeti Boys mbele kwa mbele

Timu ya Taifa ya Vijana  chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imeendelea kufanya vema katika mashindano ya AFCON yanayoendelea nchini Gabon.
Serengeti Boys imefanya jambo ambalo Watanzania wamekuwa wakilisubiri kwa muda mrefu, kushiriki na kuleta ushindani katika mashindano ya kimataifa.
Timu hiyo imecheza mechi mbili za ushindani mkubwa katika kundi lake, mechi ya kwanza walicheza na mabingwa watetezi timu ya vijana kutoka Mali, mechi ambayo walitoka sare ya bila kufungana, huku mechi ya pili wakiwapiga kumbo Angola mabao 2-1.
Wadau wa soka wamekuwa wakiielezea kama moja ya timu ambazo zimepata maandalizi ya kutosha, pamoja na kukaa pamoja kwa muda mrefu, hali ambayo imewafanya kutengeneza ‘pattern’ ambayo imezaa matunda katika mashindano ya AFCON.
Kabla ya kwenda Gabon, Serengeti Boys ilipata muda wa kufanya mazoezi pamoja na kushiriki mechi tatu za kirafiki, imeshinda mechi mbili za kirafiki dhidi ya Gabon mechi zilizochezwa nchini Morocco ilikokuwa imeweka kambi kabla ya kwenda Cameroon.
Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa kamati ya uhamasishaji wa timu hiyo, Charles Hillary, amesema kazi waliyokabidhiwa inaenda vizuri kama ilivyotarajiwa, Serikali, wananchi wa kawaida na taasisi mbalimbali wanaendelea kutoa ushirikiano mzuri kuhakikisha vijana wanapata mahitaji yote muhimu katika kipindi hiki.
Amesema kamati yake imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kila Mtanzania anahamasika kuwasaidia vijana hawa ambao wengi wao wanalelewa na Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF).
“Umefika wakati kwa Watanzania tukatae kuitwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ na hili litawezekana kwa kuanza kuwekeza katika timu hizi za vijana ambazo tayari zimeonesha uthubutu wa hali ya juu,” amesema Hillary.
Amesema kamati, kwa kushirikiana na mamlaka husika, itahakikisha uhai wa Serengeti Boys na pia timu ya soka ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 23 – Ngorongoro Heroes – inafuzu michezo ya Olimpiki mwaka 2020 zitakazofanyika Tokyo, Japan.
“Tutafanya kila lililo chini ya uwezo wetu kuhakikisha vijana wetu chini ya umri wa miaka 23 wanafuzu katika michezo ya Olimpiki 2020 itakayofanyikia Tokyo nchini Japan,” amesema Hillary.
Katibu wa Kamati hiyo, Mwesigwa Selestine, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TFF, amesema shirikisho litafanya kila liwezekanalo kuhakikisha timu inafanya vizuri nchini Gabon.
“Changamoto iliyo mbele yetu ni gharama kubwa zinazohitajika kuhakikisha vijana wanatuwakilisha ipasavyo ndiyo maana tunawaomba Watanzania wote kuunganisha nguvu kuwasaidia vijana hawa,” amesema Selestine.
Amesema TFF, kwa kushirikiana na Serikali, wadau na wapenzi wote wa mchezo wa soka dhamira yetu kubwa iliyo mbele kwa sasa ni kuhakikisha timu ipo Gabon kutoa ushindani wa hali ya juu na kurejea na Kombe.
 Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga, amesema kama kuna jambo ambalo Watanzania wanapaswa kujivunia katika kipindi hiki ni timu ya Serengeti.
“Wachezaji hawa wameendelea kujijengea hali ya kujiamini kati yao sababu wamecheza dhidi ya  mwenyeji wa mashindano, na wamecheza dhidi ya timu zenye majina makubwa barani Afrika,” amesema Ndolanga.
Amesema kitendo cha kuifunga timu kama Cameroon na Gabon zote za Afrika  Magharibi, imewaongezea  hali ya kujiamini na hili litawasaidia wakati wote wa mashindano yaliyoko mbele yao.
Amesema Watanzania hawana budi kuiunga  mkono timu  kwa kuichangia ili iweze kupata motisha wa kupambana katika mashindano yaliyo mbele yao muda wote watakapokuwa huko.
Amesema asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo waliopo sasa wanalelewa na kutunzwa na TFF, hii ni tofauti na sehemu nyingine kote duniani ambako wachezaji wanatoka kwenye klabu.
“Katika nchi nchi nyingine chama cha soka kazi yake ni kuandaa mazingira mazuri ya timu za Taifa na siyo kutengeneza wachezaji katika hili mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, TFF wanastahili pongezi,” amesema Ndolanga.
Amesema jambo hili lina faida kubwa sana kwa wachezaji hawa  kukaa katika
mazingira ambayo wanafundishwa soka kwa muda mwingi kutoka kwa wataalamu wa soka la vijana waliopo TFF.
Amesema mchezo wa soka kwa sasa ni miongoni mwa michezo yenye utajiri mkubwa duniani, hasa wakati wa kununua na kuuza mchezaji lakini pia ndiyo unaoongoza kwa kuwa na washabiki wengi duniani.
Timu  hiyo ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imebadilishiwa kituo kutoka Port Gentil na sasa imepangiwa mjini Libreville Gabon wakati wa fainali za Afrika kwa Vijana.
Timu hiyo imepangwa kundi B pamoja na timu za Niger, Angola na Mali.

792 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons