Narudia mada ambayo hunikosesha usingizi mara kadhaa kila mwaka: elimu. Mahsusi ni ugumu wa kuhimiza jamii kuchangia uboreshaji elimu.

Ni suala ambalo nalikabili kila niwapo kazini kwa sababu ya nafasi yangu kama msimamizi wa asasi isiyo ya kiserikali inayogharimia mahitaji ya elimu ya watoto yatima na watoto 150 wanaoishi kwenye mazingira magumu Mkoa wa Mara ya Global Resource Alliance (GRA) – Tanzania. Imesimamia kazi hii tangu 2008.

Tunaweza kubishana kidogo juu ya aina gani ya elimu inafaa kwa wakati upi Tanzania, lakini kwa ujumla siamini kama kuna ubishi juu ya umuhimu na uwepo wa elimu kwa taifa.

Kwa upande mmoja elimu bora ndiyo njia mojawapo muhimu sana ya kumtoa mtoto aliyezaliwa kwenye hali duni kuweza kuinuka na kufikia nafasi nzuri ya kujiendeleza maishani na kuwa na maisha bora kama mtoto mwenzake aliyezaliwa kwenye hali ya neema.

Sehemu kubwa ya msaada ambayo GRA – Tanzania inatoa kwa watoto hawa inatoka nje ya nchi kwa wafadhili ambao wamewafanya watoto wetu kama watoto wao.

Siamini kama ni suala la uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi unaowatuma kufanya hivyo, kama ambavyo matokeo ya tafiti yanaashiria.

Utafiti wa mwaka 2016 juu ya ukarimu wa kutoa unaorodhesha wananchi wa Myanmar wakiongoza wenzao wote duniani kwa ukarimu wao usiyo na mfano. Watafiti wanaamini kuwa nafasi hiyo inatokana na mafundisho yaliyomo ndani ya imani ya dini ya Buddha inayoelekeza kuwakirimu wale wanaoishi maisha ya kitawa.

Katika utafiti huo Wamarekani wanashika nafasi ya pili duniani. Kwa takwimu za mwaka 2019 uchumi wa Marekani ndiyo unaongoza kwa ukubwa duniani. Uchumi wa Myanmar unashika nafasi ya 71. Pato la wastani kwa mwaka la Mmarekani ni zaidi ya dola 65,000 za Marekani wakati wastani huo kwa raia wa Myanmar ni dola 1,380 za Marekani.

Tukirudi kwenye suala la ukarimu Kenya inashika nafasi ya kwanza Afrika na nafasi ya 12 duniani. Kati ya nchi 140 zilizohusishwa kwenye utafiti, Tanzania inashika nafasi ya 57. Nafasi ya Tanzania hainishangazi sana kwa sababu ni matokeo yanayowiana na ugumu ninaokumbana nao kila ninaposhiriki jitihada za kuhimiza kuchangia mahitaji ya elimu kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yangu.

Wanasema ukarimu ni matokeo ya makuzi yanayotokana na mila na desturi. Kwa wananchi wa Myanmar ukarimu huo unaelekezwa ndani ya dini yao ya Buddha. Lakini hata sisi tunazo dini na zinahimiza sana ukarimu. Dini zote kuu hazina upungufu wa aya zinazomhimiza muumini kujitolea kusaidia binadamu wenzake.

Ndani ya Biblia Wakristu wanaaswa kwenye  2Wakorintho 9:6-7: “Kumbukeni: Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.”

Waumini wa dini ya Kiislamu nao wanahimizwa kusaidia wasiokuwa na uwezo. Dhana ya kusaidia kwenye Uislamu inatokana na mafundisho kwamba kila alichonacho binadamu anacho kwa sababu ya baraka za Mwenyezi Mungu. Muislamu anapotoa mfukoni na kuwapa wengine hapotezi kitu, bali anajiongezea baraka.

Hata bila kuhimizwa na dini tunaona kuwa mila na tamaduni zetu ni mifano ya maisha ya kusaidiana na kushirikiana inayowataka wenye uwezo kuwasaidia wale ambao hawana uwezo.

Kwa kifupi, hakuna kipengele cha maisha – iwe dini au tamaduni zetu – ambacho kinamuacha Mtanzania bila muongozo madhubuti wa kumhimiza kusaidia wanajamii wenzake ambao wanahitaji msaada.

Sasa tatizo liko wapi? Tatizo si moja. Mimi naanza kuamini kuwa tatizo mojawapo ni siasa. Mwanasiasa anapoomba kuchaguliwa hutoa ahadi za kila aina zilizojengwa juu ya msingi wa yeye kuleta mabadiliko au maendeleo kadha wa kadha kwa wapiga kura wake.

Na ni kweli, kwamba katika kuchagua kati ya wagombea wawili au zaidi, mpiga kura analinganisha ahadi za wagombea na kuamua kumpa kura mgombea ambaye anaamini atamaliza au kupunguza kero zilizopo.

Lakini kwa kawaida mwanasiasa anaahidi kupunguza au kumaliza tatizo ambalo hajapima vizuri ni kubwa kiasi gani. Na hata anapokuwa ametathmini vyema ugumu wa tatizo njiani anaweza kukumbana na vikwazo vya kuathiri ahadi alizotoa.

Sijasikia kuwapo serikali ambayo imemaliza kero zote za wapiga kura wake. Sijasikia pia serikali ambayo baada ya kuingia madarakani na kupambana na changamoto za kutimiza ahadi ilizotoa kwa wapiga kura ianze kuwaambia wapiga kura kuwa inapunguza ahadi za kampeni mpaka uchaguzi ujao. Hiyo itakuwa ni sawa na kujiwekea kitanzi cha kisiasa shingoni na kujining’iniza.

Na ndiyo maana yangu ya kusema tatizo ni siasa. Mwanasiasa anaingia madarakani kwa kutoa ahadi za maisha mazuri kwa wote wakati wote. Mpiga kura anaweza akachapa usingizi akiamini kuwa serikali itamaliza matatizo yake yote au anaweza akaamka na kutambua ukweli kuwa serikali – popote duniani – haiwezi kumaliza matatizo yote yaliyopo.

Mahitaji ya sekta ya elimu hayajapunguka kwa kiasi kikubwa kwa kuondolewa tu kwa malipo ya karo kwa wazazi. Upo mchango mkubwa ambao jamii inaweza kutoa kuboresha mazingira ya walimu na wanafunzi katika sekta ya elimu.

Lakini utayari wa jamii kuchangia uboreshwaji wa sekta ya elimu unaathirika sana na imani kuwa serikali ipo na itafanya kila kitu.

187 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!