Serikali imesema kasi ya ongezeko la idadi ya watu jijini Dar es Salaam, inatisha. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na watu milioni 4.3.

Ongezeko la watu si Dar es Salaam wala mijini pekee. Wala si Afrika pekee. Ongezeko la watu mijini ni suala lililogusa kila taifa na kila Bara. Tofauti na Tanzania na Afrika, mataifa mengi ya Ulaya, Marekani na Asia (mfano China), Serikali za mataifa hayo zimejiwekea mipango ya kukabiliana na hali hiyo.

 

China, ambayo miaka kadhaa idadi kubwa ya watu ilikuwa vijijini, sasa inaelekea kuwa kinyume. Hali hiyo imetokana na ukuaji uchumi na kufunguliwa kwa fursa mbalimbali za kijamii.

 

Kwa kulitambua hilo, hata kabla ya mabadiliko ya sasa ya kiuchumi, China iliweka sheria ya familia kuwa na mtoto. Sasa wamelegeza mambo kidogo – wanaruhusu familia kuwa na watoto wawili, lakini wawe wa jinsi ya kike. Wamefanya hivyo ili kukabiliana na uhaba wa wanawake nchini humo.

 

Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba ni aibu kwa viongozi wa Serikali na wadau wengine kusimama na kutamka maneno mepesi ya, “Ongezeko la idadi ya watu inatisha”.

 

Haya ni maneno mepesi kwa jambo ambalo ni muhimu sana. Miaka michache baada ya Uhuru, Tanzania ikiwa bado haijafikisha idadi ya watu japo milioni 12, iliona hatari inayoinyemelea. Kulianzishwa kampeni maridhawa iliyohamasisha uzazi wa mpango. Walioweka mpango huo hawakuwa mbumbumbu. Walitambua kwamba kasi ya ongezeko la idadi ya watu isipokwenda sambamba na ukuaji uchumi, matokeo yake yanaweza kuwa mabaya zaidi katika jamii.

 

Serikali imeacha wajibu wake wa msingi wa kuhamasisha uzazi wa mpango. Matokeo yake sasa kuna vidume vilivyoamua kugeuka kuwa mitambo ya kuzalisha watoto. Kuna watoto wengi mno mitaani. Hawa wana baba zao.


Sheria zetu bado butu katika kuwabana wazazi wanaozaa na kutelekeza watoto. Madhara yake ni haya ya kuwa na watoto wanaoitwa ‘wa mitaani’ kana kwamba mitaa nayo ina uwezo wa kutia au kutunga mimba.


Kwa upande wa Dar es Salaam kulemewa na idadi kubwa ya watu, hili ni jambo lililotarajiwa. Haiwezekani mipango mingi ya nchi ipelekwe Dar es Salaam, halafu utarajie kuwa na uhaba wa watu katika jiji au mkoa huo. Athari hizi za kurundika mambo pamoja zinaonekana Dar es Salaam kwenyewe.


Ofisi nyingi na muhimu za Serikali zinajengwa upande mmoja wa jiji. Matokeo ya hali hiyo ni haya ya misururu ya magari isiyomithilika. Watu wenye mtazamo wa kawaida kabisa wanajiuliza, kwanini Serikali na taasisi zisijenge ofisi Mbagala, Mbezi, Kimara na kwingineko nje ya jiji?

 

Watu wanajiuliza, kama mji mkuu wa Tanzania ni Dodoma, iweje kila mwaka zitolewe fedha za kukarabati na kujenga ofisi mpya jijini Dar es Salaam? Kwanini wakubwa hawataki kuhamia Dodoma? Kwanini mambo mazuri mazuri yote yanapelekwa Dar es Salaam?

 

Vijijini hakuna umeme. Hakuna maji ya uhakika. Viwanda vimeuawa. Miradi ya mashamba, ushirika, viwanda vidogo vidogo vijijini vimekufa. Si viongozi wote wanaoshituka.


Huduma nzuri za tiba zinapatikana mijini. Katika mazingira ya aina hii, kwanini watu wasikimbilie mijini, hususan Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na kadhalika? Kijana gani anayetaka kubaki kijijini ambako haoni mwanga wala matumaini ya kuboresha maisha yake? Nani anataka kubaki kijijini wakati wabunge wanapotoka Dodoma wanaishia mijini?


Nihitimishe kwa kusema wazi kuwa suala la ongezeko la idadi ya watu nchini, na hasa mijini, ni jambo kubwa sana. Ongezeko la watu lisilowiana na hali ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, ni bomu.


Sote kwa pamoja tunapaswa kushiriki kueneza kampeni ya uzazi wa mpango.  Kuzaa watoto wengi tusioweza kuwapatia huduma muhimu za elimu, afya na lishe ni kukaribisha balaa na machafuko katika nchi. Serikali haipaswi kuwa upande wa wanaoshangaa ongezeko hili. Inastahili kuwa sehemu muhimu ya utatuzi wa jambo hili.

By Jamhuri