Serikali imeingilia kati kulinusuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya ofisi zake kufungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushindwa kulipa kodi ya shilingi bilioni 1 inayodaiwa kwa miaka mingi.

Deni hilo lilitokana na TFF kushindwa kuwalipia kodi makocha wa kigeni, Mbrazili Marcio Maximo, Jan Poulsen na Kim Poulsem, raia wa Denmark, walioajiriwa kuzifundisha timu za Taifa za wakubwa na wadogo kati ya mwaka 2007 hadi mwaka 2012 kwa nyakati tofauti.

Akizungumza na JAMHURI mara baada ya kurejea kutoka Morocco kwenye kambi timu ya Serengeti boys, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, amesema Serikali imeamua kuingilia kati na kuamuru TRA kufungua ofisi za TFF.

Amesema kwa kulitambua hilo, Waziri Harrison Mwakyembe alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake akutane na Katibu wa Wizara ya Fedha  na Mipango kwa pamoja wakakae na Kamishna wa TRA kuangalia namna ya kulimaliza tatizo.

Amesema madeni mengine yaliyosababisha kufungiwa kwa akaunti za benki za TFF ni madeni yaliyobainika baada ya ukaguzi – kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mechi kati ya Taifa Stars na Brazil mwaka 2010.

Kuhusu kambi ya timu ya Serengeti boys iliyoko nchini Morocco, amesema yanaendelea vizuri chini ya benchi la ufundi japokuwa kuna baridi kali ikilinganishwa na hali ya hewa ya hapa nchini.

 “Vijana wapo vizuri kiafya na kiakili japo changamoto kubwa ni hali ya baridi kali iliyoko nchini Morocco, hata hivyo vijana wameahidi kutowaangusha Watanzania,” amesema Malinzi.

Mkurugenzi wa huduma na elimu ya mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo, ameliambia JAMHURI tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi baada ya Serikali kuingilia kati na kuziamuru pande husika kulimaliza.

Amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa michezo hasa katika kipindi hiki ambacho Serengeti Boys inakabiliwa na mashindano makubwa, imeona ni vema suala hilo likamalizwa kwa njia nyingine itakayowapa nafasi TFF kutekeleza majikumu yao.

“Ni kweli tulichukua uamuzi wa kuzifunga ofisi za TFF, tukilenga kushinikiza kulipwa kwa deni wanalodaiwa kwa miaka mingi lakini bahati nzuri wahusika wameingilia kati na kulimaliza,” amesema Kayombo.

Mwenyekiti wa kamati ya kuhamasisha Serengeti Boys, Charles Hilary, amesema tayari wameanza kutekeleza baadhi ya majukumu waliyokabidhiwa na Waziri kwa niaba ya Watanzania.

Amesema wameanza kwa kuyatembelea makundi mbalimbali ya watu, makapuni ya Serikali, watu binafsi lengo likiwa ni kuwahamasisha kuichangia timu kila mmoja kwa uwezo alionao na kwa nafasi yake.

“Moja kati ya majukumu tuliyokabidhiwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha vijana wanafanya vizuri katika kila mechi watakayoshiriki kuanzia sasa,” amesema Hilary.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime, akihojiwa na baadhi ya vyombo vya habari kutoka Morocco amesema, kikosi chote kipo imara kisaikolojia na anaamini watafanya vizuri katika mashindano yanayowakabili mbele ya safari.

“Tulipanga kucheza mechi saba mpaka tisa za kirafiki, mpaka tunakuja hapa Morocco tulikuwa tumecheza mechi tatu, kwa hapa tunatarajia kucheza mbili, Cameroon tutacheza mbili kabla ya kwenda nchini Gabon,” amesema Shime.

Mwaka jana, pia TRA ilifunga akaunti za TFF zilizokuwa na zaidi ya Sh milioni 150 kwa kushindwa kulipa deni wanalodaiwa la Sh bilioni 1.6 lakini inadaiwa walilipa kiasi cha Sh milioni 400 tu.

Serengeti Boys ipo kambini kwa mwezi moja nchini Morocco ikijiandaa na fainali zitakazofanyika nchini Gabon kuanzia Mei 14 ambapo timu nne zitakazofikia hatua ya nusu fainali zinakata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini India Novemba mwaka huu.

Timu hiyo ilifuzu kuingia katika fainali hizo baada ya kushinda rufaa yao dhidi ya timu ya Congo Brazzaville kumchezesha mchezaji aliyezidi umri wa miaka 17, tofauti na kanuni za mashindano na kujikuta wakiondolewa katika mashindano hayo.

Timu hiyo imepangwa kundi B lenye timu za Angola, Niger na Mali. Kwa sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limewafungia baada ya Serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya soka na kuwafukuza viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo – FEMAFOOT.

Awali, fainali hizo zilitakiwa kufanyika nchini Madagascar lakini Gabon, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou wa Cameroon, alisema nchi hiyo haikukidhi vigezo vya kuandaa mashindano  na kujikuta wakipokonywa nafasi hiyo.

929 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!