SERIKALI YATENGA 4.3bn/- KUJENGA VITUO VYA KUHIFADHI DAMU SALAMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 4.3 ili kujenga vituo vya kuhifadhi damu (satellite blood banks) kwenye mikoa 12.

 

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Njombe. Mingine ni Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu.

 

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge.Bunge limeahirishwa hadi Septemba 4, mwaka huu.

 

Amesema lengo la mpango huo ni kuboresha upatikanaji wa damu hasa kwa akinamama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. “Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara, wodi za wazazi, nyumba za watumishi na wodi za watoto,” amesema.

 

Amesema kukamilika kwa majengo hayo, kutaboresha huduma za uzazi kwa akinamama na watoto wachanga. “Hatua hii itawezesha upatikanaji wa huduma kamili za uzazi na kupunguza vifo vya mama na watoto. Katika mwaka 2018/2019, eneo litakalopewa kipaumbele ni kuimarisha upatikanaji vifaa na watumishi katika vituo 208 vinavyoendelea kuboreshwa,” amesema.

 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi watumishi wa afya, waongeze juhudi ya kuhamasisha wananchi wajitolee damu na pia akawaomba wananchi nao wawe na utamaduni wa kuchangia damu ili kuwezesha upatikanaji wa damu salama itakayohifadhiwa kwenye benki hizo.

 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa nchini kwa kutenga shilingi bilioni 14 ili kuanzisha huduma ya kuchunguza mwili bila upasuaji (PET Scan) katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

 

 

 

 

Amesema kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hicho na kwamba Serikali itaweza takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kulipia wagonjwa waliokuwa wakienda nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hiki.

 

Amesema Serikali itasogeza huduma ya tiba ya saratani katika ngazi ya Hospitali za Kanda ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya Kanda ya Kaskazini KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, jijini Mbeya.

 

“Vilevile, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa tiba na madaktari bingwa. Jumla ya shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha hospitali hizi,” amesema.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for Results – EP4R) itaimarisha miundombinu kwenye shule zenye uhitaji mkubwa.

 

“Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatumia shilingi bilioni 155.58 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe 25, ununuzi wa vifaa vya maabara, ujenzi wa mabwalo 85, vyumba vya madarasa 2,000 na motisha kwa Halmashauri kutokana na ufanisi katika utekelezaji wa vigezo vya EP4R,” amesema.

 

Amesema kwa sasa, Serikali inatarajia kuajiri walimu 4,785 wa shule za msingi zenye uhitaji mkubwa na kwamba tayari imeshatangaza nafasi za ajira kwa walimu 2,000 wa masomo ya sayansi, hisabati na lugha ambao watapangwa kwenye shule za sekondari zenye uhitaji mkubwa.

 

Amesema kuwa Serikali imetangaza nafasi za ajira kwa mafundi sanifu maabara 160 ambao nao pia watapangwa kwenye shule zenye uhaba wa wataalamu hao.

 

(mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

  1. L. P. 980,

41193 – DODOMA.

IJUMAA, JUNI 29, 2018.