Sheria imeruhusu kudai zawadi uchumba unapovunjika

Una mahusiano na mwanaume au mwanamke ambaye kimsingi mpo katika uchumba. Unampa zawadi nyingi naye anakupa zawadi. Mnayo ahadi ya kufunga ndoa na kuishi kama mume na mke. Na kwa sababu hiyo, unajitoa sana kimatumizi kwa mtu huyo.
Lakini katika mazingira usiyoyaelewa unaona sasa mambo hayaendi vizuri. Hayaendi vizuri katika kiwango ambacho sasa mahusiano yamevunjika kabisa. Hakuna tena mahusiano. Au bado yapo lakini kwa mambo unayofanyiwa unaona kabisa hutakiwi tena.
Kumbuka huko nyuma umegharamia sana. Umegharamia kwa fedha na mali. Swali, ni je, vitu hivi haviwezi kurudishwa? Vitu hivi haviwezi kufidiwa ? Na je, sheria imeongelea kuhusu jambo hili?
Majibu ya maswali haya yote ni ndiyo. Ni ndiyo, na gharama pamoja nazo zawadi zinaweza kurejeshwa. Unaweza kushangaa kuona sheria imeongelea hata mambo ya uchumba lakini ndiyo ukweli.
Wengi tunaijua sheria katika kuongelea wizi, dhamana, mikataba, mirathi, ndoa, na mengine. Lakini ni vyema tukajua kuwa sheria ni pana na imeongelea mambo mengi mno. Hili la uchumba nalo ni sehemu ya yaliyoongelewa.

KUVUNJA UCHUMBA
Kifungu cha 69( 1 ) cha Sheria ya Ndoa iliyofanyiwa marekebisho 2010 kinasema kuwa mtu anaweza kufungua shauri na kudai fidia baada ya uchumba kuvunjwa.
Kwa haraka utaona kuwa tafsiri ya kifungu hiki siyo kufungua shauri ili kumlazimisha mtu akurudie, hapana. Mahakama haiwezi kutoa uamuzi kuwa fulani lazima amrudie fulani. Isipokuwa lengo lake ni kumtaka yule aliyeumizwa katika hili kudai fidia kutokana na maumivu aliyoyapata. Hapa hatujaongelea kurudisha zawadi.
Kudai fidia na kurudisha zawadi ni vitu viwili tofauti. Fidia inahusu kulipwa maumivu uliyoyapata kutokana na tukio hilo la kuachwa pamoja na muda uliopoteza na huyo mtu. Wakati zawadi ni kurejesha kile ulichotoa. Kwa hiyo la zawadi tutaliona baadaye.
Aidha, masharti ya kufungua shauri la kudai fidia ni kuwammoja anayefungua shauri awe ni yule aliyeumizwa, pili ahadi ya kuoana lazima iwe ilikuwa imefanyika Tanzania, tatu wakati mnaingia kwenye mahusiano iwe mlikuwa nyote mmetimiza miaka 18 .

2. KURUDISHA ZAWADI
Kifungu cha 71 cha Sheria ya ndoa kinasema kuwa mtu anayo haki ya kufungua shauri kudai kurejeshewa zawadi alizotoa kwa mtu ambaye alikuwa ana ahadi ya kufunga naye ndoa, lakini ndoa haikufungwa.
Zawadi ni pamoja na fedha, nyumba, magari, nguo na kila kitu chenye thamani (valuable). Bila kujali mali hiyo ipo kwenye jina la nani suala la msingi ni kuthibitisha kuwa wewe ndiye uliyetoa hiyo zawadi.
Shauri la namna hiyo unaweza kulifungua mahakama yoyote ya mwanzo, ya wilaya, ya hakimu mkazi au hata mahakama kuu. Itategemea na thamani ya kiwango cha mali unazodai.
Kama mali hizo zitakuwa zimekwishatumika au hazipo tena pengine zimeuzwa au kutolewa zawadi kwa mtu mwingine, basi itatakiwa kulipwa fedha zinazolingana na mali hizo au mali hizo zikanunuliwe tena kwingine ili kumrudishia anayedai.
Ukishindwa kabisa kurudisha basi  mali zako binafsi ambazo hazikuwa sehemu ya zawadi zitauzwa ili kupata kiwango kinachodaiwa, na kama huna mali yoyote ya kuuza utatakiwa kwenda jela kama mfungwa wa madai.
Kwa hiyo, watu wanatakiwa waelewe kuwa uchumba na ahadi za kuoana si jambo jepesi kama wanavyolitamka na kuliahidi.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.