Ndugu zangu waandishi wa habari katika Mkoa wa Arusha, wameahidiwa ‘zawadi’ ya kufungia mwaka 2016 na kufungulia mwaka 2017. Wameahidiwa msaada wa pikipiki mbili! 

Sina hakika, ni pikipiki za aina gani, lakini kama ni miongoni mwa hizi zinazosambazwa na uongozi wa Mkoa wa Arusha, basi thamani yake haizidi Sh milioni 3. Laa, ikizidi sana; basi ni Sh milioni 4! 

Wapo wanaomini kuwa zawadi ni zawadi, au msaada ni msaada bila kujali ukubwa au udogo; uchache au wingi wake. Tunaaminishwa kuwa ilimradi kinachotolewa ni zawadi au msaada, anayepewa hana budi kuupokea kwa mikono miwili. Dhana hii si sahihi.

Wapo wanaoweza kuuliza, endapo nchi tajiri kama Tanzania yenye rasilimali za kila aina bado inakuwa radhi kupokea msaada, seuze waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha? Hapo ndipo penye hoja.

Sina hakika kama waandishi wa habari wameomba msaada wa pikipiki mbili! Nashawishika kuamini kuwa ‘msaada’ au hii zawadi imetolewa tu na Mkuu wa Mkoa kwa utashi wake mwenyewe. Naamini Arusha wapo waandishi wa habari ambao wakiamua kuusaidia umoja wao, idadi ya pikipiki itakosa maegesho kwenye ofisi zao! Wanaweza wakawa hawana uwezo wa kununua magari ya kifahari, lakini hili la pikipiki nadhani wameshalivuka.

Nayasema haya kwa sababu kuna dhana kuwa waandishi wa habari ni watu ‘dhooful hal’ – walio tayari kupokea chochote hata kama kinadhalilisha utu na heshima yao. Ndiyo maana wapo wanaowaita waandishi wa habari na kuamua kuwapa ‘bahasha’, lakini humo ndani kilichowekwa huwa ni Sh 20,000 au Sh 30,000.

Mwandishi wa habari anapokadiriwa thamani yake ni kiasi hicho cha fedha, hiyo ni hatari kubwa. Nayasema haya kwa sababu nina uzoefu nayo. Mara kadhaa nimejiuliza, endapo sijamwomba mtu fedha, iweje anipe kiasi hicho? Je, si kweli kuwa hicho anachonipa ninaakisi mtazamo wake halisi juu yangu?

Hili tukio la Arusha limenishawishi niyaseme haya, si kwa sababu ya kuibua uasi, lakini kuhoji uhalali wa mtazamo wa huyu aliyeamua kutoa msaada au hiyo zawadi. Kama waandishi ndiyo wenyewe walioomba wapewe hizo pikipiki mbili, naweza kusamehe maana pengine hilo ndilo hitaji lao kuu.

Lakini kama pikipiki mbili hizi ni zawadi (kwa kazi gani?) au msaada uliotolewa na mhusika kama makadirio yake ya kiheshima kwa wanahabari, nawaomba sana wanataaluma wenzangu wasipokee.

Wanahabari wana mambo mengi ya msingi kabisa wanayoweza kusaidiwa. Kubwa, ni la kutendewa haki wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao. 

Msaada huu wa pikipiki umekuja katika kipindi ambacho mwenzetu alikamatwa na kuswekwa rumande. Baada ya hapo wanahabari kwa umoja wao wakaamua kuonesha umuhimu wao kwa jamii. Kitendo cha mwandishi yule kuwekwa rumande kwa jambo ambalo lingeweza kumalizwa kwa karipio la mhariri wake tu, ni cha udhalilishaji na uonevu. Kama kuna msaada unaostahili kupewa waandishi wa habari ni kuwatendea haki na kuwapa heshima kama sehemu kati ya kundi kubwa la watu walio muhimu katika jamii yetu.

Pikipiki hizi mbili zikipokewa zinaweza kuwa chambo cha kuwafanya wanahabari wawe wanyenyekevu hata pale pasipostahili unyenyekevu. Wajibu wa wanahabari ni kusaidiana na vyombo mbalimbali katika kuibua na kupata suluhu ya matatizo kedekede yanayowasibu wananchi kote nchini.

Kuna maelfu ya wananchi wanaotaabika kwa mambo ambayo mkuu wa wilaya angeweza kuyamaliza kwa dakika tano tu! Kuna watendaji wa Serikali ambao ni miungu-watu; kazi yao kuu ni kuwaonea wananchi. Kuna genge la viongozi wasiowajibika kuwaondolea kero wananchi kama wanavyosisitiza viongozi wakuu wa Taifa letu.

Ni wajibu wa wanahabari kufukua, kuandika na kutangaza shida zinazowakabili wananchi ili mamlaka ziweze kutoka usingizini. Inapotokea kazi hiyo ikathaminishwa na pikipiki mbili za Sh milioni 3; hiyo inakuwa dharau kwa wanahabari.

Waandishi wa habari wanahitaji msaada mkubwa wa kuwakwamua kimaisha. Wanahitaji kupata msaada wa elimu katika vyuo vya ndani na nje ya nchi. Unapomsaidia mwanahabari kupata elimu katika taaluma yake, umemsaidia maisha yake yote. Msaada wa elimu inayokaa kichwani si sawa na wa pikipiki ambayo inaweza kupata ajali siku hiyo hiyo inapotolewa kwenye hafla ya makabidhiano!

Waandishi wa habari wanapaswa watendewe haki kwa kupata maeneo ili wajenge vitegauchumi vyenye kuwasaidia katika maisha yao ya kitaaluma na maisha ya kawaida katika familia zao.

Hii misaada ya pikipiki haiwezi kubadili utendaji kazi wa wanahabari, badala yake ni chanzo cha kuwafanya wawe ‘watumishi’ wa baadhi ya viongozi au watu wenye nguvu fulani fulani.

Wanahabari waige mfano wa Serikali ya Awamu ya Nne ambayo pamoja na unyonge wetu wote, iliweza kusimama imara kukataa misaada yenye masharti ambayo yakitekelezwa, yanaudhalilisha utu wetu kama binadamu, na sana sana kama Waafrika.

Misaada hii ya pikipiki mbili kwa watu muhimu kabisa katika mustakabali wa nchi hii haina tofauti na ile ya kujengewa vyoo kwa ‘hisani ya Watu wa Marekani’! Pamoja na umaskini wetu kama Taifa, kuomba msaada wa kujengewa vyoo ni udhaifu mkubwa mno. Tunapopewa misaada, tupewe misaada kwa kitu au vitu vilivyo nje ya uwezo wetu. Wanaoamua kutupatia msaada, hawana budi kuangalia aina ya msaada wanaotupatia ili kuepuka kutudhalilisha au kutufanya watu dhalili.

Endapo tutaendelea kukubali kupokea msaada ya aina hii, tujiandae pia kutoa malipo makubwa yanayoendana na fadhila hiyo! 

Nayasema haya kwa ndugu zangu wa Arusha, nikiamini kuwa wana uwezo wa kukataa baadhi ya zawadi wanazoona haziendani na hadhi yao.

Pia nayasema haya kwa ndugu zangu viongozi kuacha kuwaona wanahabari kama kundi la watu dhalili ambao chochote wanachopewa wanaweza kukipokea na kumpigia makofi huyo aliyekitoa.

Pikipiki hizi mbili zisigeuzwe peremende zenye vimelea vya kuwafanya wanahabari wazubae na kusahau kitendo alichofanyiwa mwenzetu na mtawala aliyeamua kutumia madaraka yake vibaya.

Wanahabari tunao uwezo wa kuyabadili maisha yetu yakawa mazuri zaidi kwa kukataa baadhi ya misaada. Lingekuwa jambo la maana sana kusikia badala ya pikipiki mbili, wanahabari wamepewa ekari mbili za ardhi kwa ajili ya kujenga kitegauchumi. 

Heshima ya wanahabari itajengwa na wanahabari wenyewe. Si kila zawadi inayotolewa, lazima ipokewe. Nyingine ni udhalilishaji. Nyingine ni mitego. Japo tu maskini, hatujawa wa kupokea kila kinachoelekezwa kwetu. 

987 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!