Kuanzia wiki iliyopita, Taifa limeghubikwa na hoja tofauti zinazolenga kuunga mkono ama kukosoa hatua ya viongozi wa dini kuzungumzia masuala ya siasa.

Hali hiyo imechochewa zaidi baada ya Askofu Zakary Kakobe wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, kukosoa mwenendo wa utawala na utekelezaji wa misingi ya demokrasia nchini.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari amesema kauli iliyoibua mjadala ni iliyotolewa na Askofu Kakobe kuhusu mwenendo wa Serikali ya awamu ya tano.

Hoja za Askofu Kakobe zimefuatia na karipio la Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali (mstaafu) Projest Rwegasira dhidi ya viongozi wa dini wanaochanganya dini na siasa.

Meja Jenerali (mstaafu) Rwegasira akaonya kuwa ikiwa kiongozi wa dini atajikita katika kujihusisha na siasa kinyume cha madhumuni yaliyomo kwenye katiba iliyosajiliwa, kuna uwezekano wa kufutwa kwa taasisi yake na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Lakini, Profesa Safari amesema ni vigumu kuwafanya viongozi wa dini kutenganisha dini na siasa.

 “Dini ni maisha ya watu na Waislamu wanapokutana kila Ijumaa miskitini, mahubiri yao ni hicho hicho ambacho viongozi wa siasa wanasema wanaingiliwa katika majukumu yao,”amesema.

Profesa Safari amesema ipo haja kwa Watanzania kuwa huru kujadili mustakabali wa siasa na demokrasia nchini, kwa vile maeneo hayo yanagusa maisha ya watu hivyo kuibua fikra na mitazamo inayotofautiana.

Kwa mujibu wa Profesa Safari, viongozi wanaopaswa kutoa tamko kuhusu fikra tofauti zinazogusia demokrasia ya vyama vingi nchini, wamenyamaza na badala yake wasiokuwa na mamlaka wanapata fursa pana ya kujibu hoja husika.

“Jeshi la Polisi tayari wameelewa alichokizungumza Askofu Kakobe na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipohojiwa na Azam Tv amebaki kubabaika tu.

“CCM wamechanganyikiwa sana na hasa pale vyama vya upinzani tulipowasusia chaguzi ndogo ili wabaki peke yao na kujichagua wenyewe,” amesema.

Alichokisema Askofu Kakobe    

Jumatatu iliyopita, Askofu Kakobe akiwa katika mahubiri kanisani kwake, alitoa kauli dhidi ya Rais John Magufuli na mwenendo wa demokrasia nchini, ikakosolewa na baadhi ya watu hususani viongozi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo Askofu Kakobe akasema Rais wa nchi anapaswa kuwa mvumilivu na kuwasemehe watu hasa waliopo ngazi za chini kwenye jamii wanapomkosoa.

Askofu Bagonza

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza anaunga mkono hoja ya ugumu wa kutenganisha dini na siasa, akitoa matukio kadhaa yanayozikutanisha asasi hizo katika utoaji huduma za jamii.

Kupitia mtandao wake wa Facebook, Askofu Bagonza amesema “ wakijenga shule hawaingilii wizara ya elimu, wakijenga haospitali hawaingilii wizara ya afya, wakijenga kisima cha maji hwaingilii wizara ya maji, wakiomba mvua hawaingilii mamlaka ya hali ya hewa…”

Akaendelea, “wakihimiza kilimo hawaingilii wizara ya kilimo, wakitoa msaada wa dawa kwa wagonjwa wanapongezwa, wakihoji kwa nini hakuna dawa hospitalini, wanaambiwa wanachanganya dini na siasa, wakikosoa mfumo wa kisiasa, wanaambiwa wanaingilia siasa! kuna kitu hakiendi sawa.”

Ni dhahiri kwamba ujumbe wa Askofu Bagonza unajikita katika kuwianisha uhusiano usiotiliwa shaka kati ya dini na siasa katika kuitumikia jamii.

Akizungumza na JAMHURI, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, William Mwamalanga amesema si sahihi kwa watumishi wa Mungu kutohusisha masuala ya siasa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba miongoni mwa wajibu wao ni kuonya, kukemea na kukaripia.

“Hapa ndio pameibua hoja na wengine kutoa kauli zenye mwelekeo wa kutafuta sifa kutoka kwa watawala ili kupewa vyeo,” amesema.

Amesema kitendo cha kuwakosoa viongozi wa dini kuzungumzia siasa inaweza kutafsiriwa kuwa kinalenga ‘kuzima midomo’ ili wasikemee pale inapobidi.

Wananchi wengine waliozungumza na JAMHURI ni mkazi wa Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam, Halima Omary (34) amesema viongozi wa dini wanahaki ya kuwaonya kuhusu masuala tofauti ikiwamo ya kisiasa.

Omary amesema wanasiasa wanapaswa kuwa wavumilivu na kutenda haki na sio kuwalalamikia viongozi wa dini kuwa wanawasema ama kuwakosoa kwa kuwaonea.

“Viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika jamii na kuhakikisha wananchi wote wanaishi kwa haki na amani, wanasiasa pia nao jukumu linalolingana na hilo, hivyo sio rahisi kutenganisha siasa na dini.

Naye Cosmas Bosco (53) mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam amesema ni sahihi kuamini kwamba viongozi wa dini wanapoingilia masuala ya siasa wanakosea.

Bosco amesema amesikia taarifa za kuikosoa Serikali kupitia katika mitandao ya kijamii na kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali na CCM dhidi ya viongozi wa dini.

By Jamhuri