Vyama vya siasa nchini, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali itikadi za vyama vyao, jambo linaloweza kuleta tija kwa Taifa.

Akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Afrika Mashariki, Twaha Taslima, amesema nchi nyingi za Afrika ikiwamo Tanzania, zinatakiwa kuwa na ushirikiano kwani kufanya hivyo kutasaidia kusonga mbele katika masuala ya kimaendeleo.

Amesema kuwa Tanzania kuna mambo mengi yanahitajika kufanyiwa kazi ikiwamo kuhakikisha tunatumia kikamilifu maliasili tulizopewa na Mungu.

“Imefika wakati Watanzania tunapaswa kuungana bila kujali itikadi za vyama vyetu, ili tufanikiwe katika mbio za kuwa na mafanikio,” amesema Taslima.

Amefafanua kuwa kila mtu anaguswa na mambo kadhaa yanayofanywa barani Afrika, ambayo kimsingi si rafiki kwa jamii.

“Awe kiongozi wa chama fulani au mtu yeyote, imefika wakati wa kuacha malumbano ya kivyama kwani hayana tija kwa Taifa,” amesema Taslima.

Taslima ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu, Uongozi Taifa, Chama cha Wananchi (CUF), anaeleza kuwa kazi zozote zinazohusiana na maslahi ya wananchi, zinatakiwa kufanywa kwa uangalifu na umakini mkubwa ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.

Amesema kuwa unyenyekevu na uangalifu, ni msingi unaotakiwa kufanywa na viongozi ambao wamepewa dhamana ya kuwaongoza Watanzania katika nyanja mbalimbali.

“Ukiona maamuzi yanayotolewa na kiongozi kuhusu jambo fulani na matokeo yake wananchi wakawa na malalamiko, basi kuna kila sababu inayoonekana kuna tatizo ndani yake,” amesema Taslima.

Taslima ambaye amewahi kuwa Kaimu Mwenyekiti wa CUF, amesema kuwa Rais John Pombe Magufuli anamwamini kutokana na kile anachosema, wananchi waendelee kumuombea kwa Mungu, pamoja na kuwa na uwezo kufanya vizuri katika shughuli za umma.

Mwanasheria huyo anabainisha, kwa mujibu wa sheria ya masuala ya siasa namba 258 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ibara 11 (1), kila chama kilichosajiliwa kinayo haki ya kufanya kazi ikiwamo kujitangaza na kutafuta wanachama.

Ibara hiyo inafafanua kuwa chama chochote kinaweza kufanya siasa, lakini kwa kufuata sheria ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.

“Kuna watu wanafanya kazi ya kisiasa, inavyotokea hali hiyo wataona kama wametengwa na kutothaminiwa kwa kazi wanazofanya,” amesema Taslima.

Amesema kuwa umoja ni nguvu hasa kwa nchi za Tanzania inayohitaji maendeleo, kwani kutofanya hivyo kunaweza kupunguza upendo kati ya watawala na watawaliwa.

Profesa Abdul Sharif kutoka Zanzibar, amesema kuwa kazi yoyote ya kisiasa inafanywa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameeleza kuwa baadhi ya kauli zinazotolewa na viongozi, zimekuwa zikienda kinyume na Katiba, jambo ambalo baadhi ya vyama vinakuwa na wakati mgumu.

Prof. Sharif amesema kuwa ni vyema busara ikatumika katika kutafuta ufumbuzi katika masuala mbalimbali ikiwamo demokrasia.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyema vya Siasa Tanzania, Magalle Shibuda, amesema kuwa wakati sahihi ukifika watajadili na kufanya mapendekezo ambayo yatakuwa rafiki kwa wadau wa vyama vya siasa.

Amesema kuwa vyama vya Upinzani vinatakiwa kuwa makini kwa kuzingatia umakini wa mabadiliko ya tabianchi ya mfumo wa uwajibikaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Shibuda amesema kuwa Serikali imekuwa na tija na kuvuta hisia za Watanzania, hivyo jamii inapaswa kuondokana vivumishi vya siasa zisizokonga mioyo ya umma.

Amesema kuwa mfumo wa vyama vingi unahitaji kila chama kuwa na uvumbuzi wa kujitambua, udumavu, ubaridi na kuondoa ukondeshwaji wa uchangamfu wa hamasa ya kwenda, sambamba na kaulimbiu ya hapa kazi.

Anabainisha kuwa Baraza la Vyama linatarajia kuwa na mawazo makini ya siasa za maendeleo ukiwamo mfumo wa siasa za maendeleo ambayo zitatiririshwa kwenye vyama vyote, huku vyama vingine vikitakiwa kujipanga upya ili kuleta mageuzi ya kimfumo.

Amesema kuwa anachokiona ni mambo mema yanayofanywa hapa nchini, kwa sababu duniani kote hakuna dhamira njema ya utumishi wa Serikali isiyokuwa na kasoro kutokana kila shari ina heri ndani yake.

Shibuda amesema kuwa furaha ya mwanasiasa ni kutoa maslahi kwa jamii na Taifa, na inapaswa kushangiliwa, uokovu unaotekelezwa na Serikali kwa vilio vya kiu ya jamii kwa ujumla.  

Angependa kutoa angalizo katika kila jambo baya linalokusudiwa kufanywa, kwa sababu Serikali imeendelea kutekeleza majukumu yake na kuvumbua mambo kadhaa ambayo si rafiki kwa jamii.

 “Hivi sasa pana punguzo la urasimu katika utolewaji wa huduma kwa mahitaji ya ustawi wa maendeleo ya jamii ya afya na elimu pamoja na kunufaisha tabaka maalumu la raia wa Tanzania,” amesema Shibuda.

 Amesema kuwa ni vyema Serikali ikaendelea kupongezwa kwa mapambano ya kudhibiti sera za ovu, huku nchi ikiendelea kujengwa na watu wenye moyo na kuepuka wenye maneno.

Anafafanua kuwa Tanzania ilikuwa ya bundi wachawi, walaji wa maliasili na wafujaji wa rasilimali za Taifa, ambao waliitwa vigogo wa kundi maalumu la maisha bora ya kuoteshwa na mbegu ovu.

Amesema kuwa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kutengeneza uendeshaji wa Serikali kwenye Pato la Taifa, ni mfumo salama wa kuwa na kinga dhidi ya nchi yetu.

Amesema kuwa Tanzania ya siasa za mfumo wa vyama vingi ina mamboleo ya vioja vya migongano ya kifikra.

“Na hali hii ndiyo moja ya chemsha bongo kwa wajibu wa utumishi wa Baraza la Vyama vya Siasa. Ikumbukwe kwamba ni fikra ya maendeleo,” amesema Shibuda.

864 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!