Siku Ngeleja alipowavaa Mbowe, Zitto

Wiki iliyopita, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), aliikosoa bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kusema kuandaa bajeti ya nchi si sawa na kuandaa bajeti ya harusi.

Niseme tu kwa dhati kabisa kwamba mwezi mmoja na nusu uliopita nilikuwa Waziri wa Nishati na Madini. Kwa namna yoyote ile na kwa hali iliyokuwapo na kwa fursa ambayo nilipewa kuwatumikia Watanzania, ni jambo la kheri kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Kwa niaba ya Watanzania kwa heshima ambayo waliyonipa kwa kuwatumikia Watanzania katika Wizara ya Nishati na Madini kwa zaidi ya miaka mitano, nawashukuru sana. Bado niko imara naendelea kuwatumikia Watanzania kupitia nafasi hii ya uwakilishi wa wananchi. Nawatumia salamu wana-jimbo la Sengerema na familia yangu kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiniunga mkono. Nawashukuru sana wabunge kwa jinsi ambavyo mliniunga mkono na kuniimarisha kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Nasimama hapa kwanza kabisa kuishukuru sana Serikali kuleta bajeti ambayo inajibu matarajio ya Watanzania. Imejielekeza katika vipaumbele ambavyo tumekubaliana Watanzania bila kujali itikadi za vyama, lakini pia inazingatia ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi na inazingatia changamoto zilizopo sasa.  

Hivyo kwa vyovyote vile sina sababu ya kusita kuiunga mkono hoja hii iliyoko mbele yetu. Naiunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Bajeti ni mjadala kuhusu mapato na matumizi na kwa vyovyote vile kwa sababu bajeti hii imejielekeza vizuri kwenye Mpango wa Miaka Mitano tuliyoasisi mwaka juzi ambao unatupeleka mpaka mwaka 2015/2016 na kwa sababu vipaumbele viko wazi, lakini pia imezingatia changamoto za wakati huu zikiwapo hatua zilizochukuliwa na Serikali. Naomba Watanzania kupitia Bunge hili tukufu waiamini Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi na waiunge mkono kwa juhudi zinazofanya.

Tunafahamu kwamba uchumi wa dunia umeyumba na sisi Tanzania ni sehemu ya huo uchumi wa dunia. Lakini Tanzania kama nchi hatutakaa kimya Serikali pamoja na chama pamoja na sisi wabunge tumekaa pamoja kujadili mambo ya kuiokoa nchi hii, kuitoa hapo ilipo na kuisogeza mbele pamoja na changamoto zinazoikabili nchi. 

La kwanza tumeambiwa hali ya maisha ambayo sasa hivi inalikabili Taifa imechangiwa kwa kiasi kikubwa na mambo mawili. Kwanza ni hali ya upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo ya Tanzania. Hilo liko wazi na limesemwa. Lakini la pili ni kutokana na bei za gharama za bidhaa kama mafuta pamoja na masuala ya umeme.

Sasa tumeambiwa hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali. Kwa kipindi kile kwenye upande wa chakula Serikali iliruhusu kuagiza sukari pamoja na kusambaza vyakula katika maeneo ambayo yalikuwa yana upungufu. Lakini jingine kubwa ambalo Serikali ililifanya kwa upande wa nishati ni kuruhusu utaratibu wa kuendelea kupanga bei elekezi na kikomo kwenye mafuta uendelee, na kwa utaratibu huo uliosimamiwa na EWURA, Watanzania tunavyoongea leo kuna unafuu walau wa asilimia 30 kuliko gharama ambazo zingekuwa kama si utaratibu huo.

Lakini mpango wa kudhibiti mgawo wa umeme tuliupitisha hapa bungeni Agosti mwaka jana, na huo ndiyo uliotusaidia kutupatia afueni ambayo tunayo sasa ya huduma ya nishati ya umeme, vinginevyo hali ingekuwa mbaya sana.

Wako watu wanasema eti hata kama juhudi hizo zimechukuliwa hazijaonyesha matokeo mazuri kuliko ambavyo ingekuwa. Lakini tunasema bila juhudi zetu tungekuwa wapi? Serikali imesema ili kuendelea mbele zipo hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa. Tumeambiwa Serikali inakuja na utaratibu wa kuwekeza katika mabonde makubwa ambayo yako ndani ya nchi yetu yanayowezesha uzalishaji mkubwa wa chakula, hili ni jambo la wazi ambalo litatutoa nchi hii kwenda upande wa pili.

Lakini Serikali imesema itapitia vivutio pia na hasa kuhusu rasilimali iliyoko ndani ya nchi yetu na hasa viwanda ambavyo viko hapa vinavyotegemea malighafi za ndani ya nchi, itapitia vivutio hivyo ili kujenga mazingira ya kuviwezesha viwanda vya ndani viendelee zaidi, vitoe ajira, lakini vipunguze mfumko wa bei.

Sasa hapa kuna suala la pamba na naomba ku-declare interest katika eneo hilo. Mimi ni mdau katika eneo la pamba. Wale Watanzania milioni 16 wanaosema kwamba wanategemea kilimo hiki mimi ni mmoja wao. Tunaishukuru Serikali kwa sababu tuna taarifa kwamba inaendelea kupitia jambo hili kwa haraka sana, ili kuhakikisha kwamba bei ya pamba inaimarishwa na kama alivyosema Mheshimiwa Mtemi (Andrew) Chenge, Sh 1,000; hili lililosemwa nadhani ni kwa kuanzia hapo.

Mwendo huo tukienda nao, lakini pia tukarekebisha vivutio vingine kuhakikisha kwamba viwanda vya pamba vinafanya vizuri zaidi kuliko kutegemea fedha kutoka nje, itatusaidia sana. Sasa katika mazingira haya ni vyema Serikali kuikubali kwa juhudi zilizofanywa.

Niongelee deni la Taifa. Yamesemwa mengi sana kuhusu deni la Taifa. Lakini tafiti zote na taarifa za kitaalamu zimeonyesha kwamba deni hili linahimilika na sisi si peke yetu tunaokopa. Zipo nchi kubwa duniani ambazo zinakopa na uwiano wa pato la Taifa na deni tumeonyeshwa.

Tumekumbushwa kwamba Kenya leo uwiano wa deni na mikopo ya nje na mikopo wanayokopa na deni la Taifa ni asilimia 48.9.  Tumeambiwa Marekani ni asilimia 102. Wajapani wana asilimia 229, Ujerumani asilimia 81.5 na Italia asilimia 120. Sasa ni lipi ambalo linashangaza leo uwiano huu wa asilimia 44 kwa pato la Taifa? Mimi nadhani wakati mwingine waheshimiwa wabunge tunakuwa hatuko wakweli na hasa upande wa pili (upinzani) wanapojaribu kuwatia hofu Watanzania kama vile sisi tunaongea peke yetu.

Juzi, kuna waheshimiwa wabunge upande wa pili ambako tunatazamana hapa, mmojawapo alisimama – ni mtani wangu kutoka Iringa – akaongelea kuhusu umakini wa utayarishaji wa bajeti, lakini mheshimiwa mwingine juzi naye akatukumbusha akanukuu msemo wa zamani – Mheshimiwa Mbowe kama Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani – nakuheshimu sana na uhusiano wako na mimi hauna shaka yoyote. Lakini nataka niseme jambo moja tunaongelea habari kubwa, na Kambi ya Upinzani inasimama hapa kujionyesha kama Serikali tarajiwa – mbadala.

Mheshimiwa Mbowe nakuelewa umeleta hotuba ambayo umeisoma hapa na wewe unasema unaleta “elements” za kibinadamu, tunakuelewa vizuri sana. Lakini makosa yako wazi ambayo hayawezi kuvumilika na ni upotoshaji mkubwa kwa Watanzania na nitakupa mfano. Mheshimiwa Mbowe ukienda kwenye hotuba yenu ukurasa wa 24 na 25 mmejichanganya na kuwapotosha sana Watanzania.

Ni bahati mbaya kwamba bajeti yenu imetangazwa mpaka sasa hivi katika magezeti mawili tu – Gazeti la Mtanzania la tarehe 20 na Gazeti la Raia Mwema la jana tarehe 20. Mlitangaza kwanza katika gazeti la Mtanzania tarehe 18, na mkatangaza katika tangazo la Raia Mwema jana tarehe 20 Juni, 2012. Lakini Watanzania wengi kwa sababu mijadala tunayoisema hapa Watanzania wengi wanaitumia kujadili, mmewapotosha Watanzania kwa kiasi kikubwa sana na nitaomba kama nakosea, omba mwongozo wa Spika nisome vifungu hivi.

Wakati wenzetu wanalalamika kwamba bajeti ya asilimia 40 imetengwa kwa wizara ambazo tumezipa vipaumbele, ukurasa wa 25 wanalalamika kwamba tumezitengea fedha kidogo sana. Wanalalamika kwamba bajeti kubwa zimepewa wizara nne, tano ambazo tumezipa vipaumbele. Hotuba imetayarishwa na watu walewale wenye mawazo yale yale wakijadili bajeti ile ile wanapingana na mawazo kwa kusema bajeti ile tumetenga fedha kidogo sana, tutakuelewaje? Mnajiandaaje kuwaandaa Watanzania kwamba ninyi mnaweza kuwa Serikali mbadala?

Lakini nenda ukurasa wa 34 – vyanzo vya mapato. Hii ni patent error, fundamental hatuwezi kuirekebisha hii, tunafanyaje. Mheshimiwa Tundu Lissu kama Mnadhimu Mkuu wa Upinzani kama nakosea sema inakuwaje katika ukurasa 34 hamuonyeshi vyanzo vya mapato ya kodi TRA, mapato yasiyo ya kodi, mapato ya halmashauzi ziro.

Naomba nitahadharishe hapa, ni rahisi sana kupanga bajeti ya harusi ama bajeti ya maandamano. Kupanga bajeti ya nchi ni jambo kubwa linalohitaji umahiri mkubwa. Tusiwapotoshe Watanzania. Mnawanyima fursa ya kusoma habari zenu kwa sababu hawana hii bajeti – imetangazwa katika magazeti – wangapi hawana access (uwezo wa kuipata). Nafahamu katika mjadala huu unaweza kuwa na ajenda, wewe na wenzako, ya kutoka nje ya Bunge hili. Kwa sababu mnaficha aibu, naomba muinue nyuso zenu, Watanzania wawaone kwenye televisheni jinsi mnavyoupotosha umma kwa kutowaambia ukweli.

Kwa nini msingesimama hapa mkaomba radhi. Watanzania kule wanapasuana vichwa kwamba Kambi ya Upinzani imeweka bajeti mbadala. Bajeti mbadala gani ambayo haina vyanzo? Mnawafanya Watanzania hawafikiri sawa sawa. Enzi hizo zimeisha, lazima muwe wawazi. Sina hakika kama kwa Msajili wa Vyama kule hakuna habari ya kufuatilia kujua kama haya ninayosema siyo ya kweli.

Ndiyo maana utakuta mwisho wake kwenye hotuba hiyo, Mheshimiwa Zitto anajinukuu mwenyewe, hivi nyinyi katika uongozi wenu Mheshimiwa Mbowe ama mheshimiwa mwingine hakuna aliyewahi kutoa neno la busara akanukuliwa? Mheshimiwa Zitto anajinukuu tu hapa, yote hiyo ni kutuonyesha umakini katika maandalizi ya bajeti ambayo Watanzania watatarajia kwamba tunajadili mambo makubwa hapa, tunaongea mambo ya msingi na kutoa mwongozo ambao Watanzania kwa pamoja tunasaidia kujenga nchi yetu.

Kwa hiyo nilikuwa naomba Watanzania wasiichambue bajeti hii kwa kuiangalia kwamba tuna bajeti mbadala hapa, hakuna.