SIMBA SC imeanza vyema michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Gendarmarie Tnare kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Magoli ya Simba yalifungwa na kiungo Said Hamisi Ndemla, Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco na mshasmbulaiji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi.

Kwa ushindi huo Simba itakuwa na kazi nyepesi kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo Djibouti.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alier Michael James aliyesaidiwa na Abdallah Suleiman Gassim na Gasim Madir Dehiya washika vibendera, Simba SC walifunga mabao 3 ndani ya dakika ya 45 za kwanza.

Kiungo Said Ndemla alizindua shangwe za mabao Simba SC dakika ya kwanza tu baada ya kufunga kwa shuti la kiufundi la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20, kufuatia Bocco kuchezewa rafu.
Bocco akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 32 kwa kichwa, akitumia mwanya wa kipa wa GendarmerieTnare kuanguka katika harakati za kuokoa.
Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Bocco akafunga bao la tatu dakika ya 45 kwa kichwa tena akimalizia pasi nzuri ya Emmanuale Okwi.
Kipindi cha pili, Simba inayofundishwa na kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Mohamed Aymen Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzalendo, Muharami Mohamed ‘Shilton’ kocha wa makipa haikuwa na makali iliyoanza nayo.
Na dakika ya 50 Gendarmerie wakapoteza nafasi nzuri ya kupata bao la ugenini baada ya mkwaju wa penalti uliopigwa na Moustapha Moussa kufuati Abdorahim Mohamed kuangushwa ndani yak umi na nane na kiungo Mghana, James Kotei kuokolewa na kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula.
Na baada ya mchezo kupooza kwa takriban nusu saa, Mganda Okwi aliyepoteza nafasi nyingi za kufunga leo, akasahihisha makosa yake kwa kufunga bao la nne dakika ya 90 baada ya kuanzishiwa pasi ya pigo la adhabu ndogo na beki anayemudu kucheza kama kiungo pia, Erasto Nyoni.
Mapema kabla ya kuanza kwa mchezo huo, mgeni rasmi, Rais wa awamu wa pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi ‘aliwatia baraka’ wachezaji wa Simba kwa kuwasabahi uwanjani na kuwatakia kila la heri.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Yussuph Mlipili, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Muzamil Yassin dk72, Said Ndemla/Mwinyi Kazimoto dk75, James Kotei, John Bocco na Emmanuel Okwi.
Gendarmerie Tnale; Bilal Ahmed, Houmaye Ali, Samatar Hassan, Moustapha Moussa/Yabeh Idriss dk58, Mohamed Idris, Moussa Youssouf, Abdorahim Mohamed/Kader Aden dk80, Mohamed Mogbel, Ahmed Aden, Souhaib Ismil/Osman Mohamed dk55 na Andre Rene.

2260 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!