‘Spiderman’ aliyemuokoa mtoto Ufaransa arejea kwao Mali

Mhamiaji raia wa Mali Mamoudou Gassama, ambaye alipata umaarufu kote duniani mwezi uliopita wakati alikwea jengo mjini Paris, Ufaransa kumukoa mtoto, amesema amefurahishwa sana kurudi kwao Mali kutembea.

“Nina furaha sana. Nina furaha sana sana kwa sababu kila mtu alikuja uwanja wa ndege na kisha nikamuona baba yangu na watu wote wa familia yangu. Sikuwa nimemuona baba yangu kwa miaka tisa,” aliiambia BBC.

Video ya Mamoudou Gassam akimuokoa mtoto ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Alivuka kutoka kwenye ubaraza mmoja hadi mwingine kwa muda wa chini ya dakika moja akamvuta mtoto huyo aliyekuwa amekwama na kumsalimisha.

Bw Gassama, 22, alivuka bahari ya Mediterranean kwa mashua ya wahamiaji mwezi Septemba mwaka 2014.

Alijiunga na ndugu yake nchini Ufaransa na kufanya kazi sehemu ya ujenzi kama kibarua.

Tarehe 26 mwezi Mei, alimuona mtoto mdogo akining’inia kutoka ghorofa ya nne kwenye jengo moja mjini Paris.

Alichukua hatua na kukwea jengo hilo na kumuokoa mtoto huyo kwa miaka mine. Alinaswa kwenye video na watu waliokuwa chini na kupewa jina “Spiderman”.

“Sikuogopa. mimi ni kama mtu yeyote yule. Nililipata ujasiri. Ulitoka kwa Mungu. Mungu aliniokoa,” alisema.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron binafsi alimshukuru Bw Gassam na kumuahidi kuwa atapa uraia wa Ufaransa.

Wiki ijayo anatarajiwa kuanza mafunzo kwenye idara ya zima moto mjini Paris.

“Nimefanya uchunguzi wa kiafya. Nitasaini mkataba wangu tarehe 28. Kisha nitaanza mafunzo ya miezi 10,” Bw Gassama aliiambia BBC.

Bw Gassama anayetoka kijiji karibu na Kayes magharibi mwa Mali, atakaa nchini Mali kwa muda wa siku tatu na atakutana na Rais Ibrahim Boubakar Keita.